The House of Favourite Newspapers

ZIJUE NJIA ZA UZAZI WA MPANGO WA MUDA MREFU

Kuna njia nyingi za uzazi wa mpango, hizi zifuatazo ni baadhi ya njia za uzazi wa mpango ambazo zinafaa kutumika:

SINDANO (Depo – Provera) Hii ni dawa maalumu anayopewa mwanamke kwa njia ya sindano ili kuzuia mimba. Ni njia salama kwa anayependa kupanga uzazi. Inafaa kwa mwanamke yeyote aliyeanza kushiriki tendo la ndoa na hajawa tayari kushika mimba.

Sindano hiyo hufanya yai la mwanamke lisipevuke, husababisha ute mzito kwenye shingo ya mji wa mimba na hivyo kuzuia mbegu za kiume zisipite kirahisi. Inafanya mji wa mimba kuwa na mazingira yasiyoruhusu mimba kutunga.

NANI ANAYESTAHILI KUTUMIA SINDANO

Mwanamke yeyote anayependa kupanga uzazi au aliyeanza kushiriki tendo la ndoa na hajawa tayari kushika mimba anastahili kutumia sindano hizi.

ASIYESTAHILI KUTUMIA SINDANO

Mwanamke yeyote anayetokwa na damu ukeni isiyo ya kawaida na ambaye tatizo lake halijabainishwa kitalaamu hatakiwi kutumia sindano hizi.

FAIDA ZAKE

Njia hii ni ya uhakika kwa kuzuia mimba na ni ya usiri wa hali ya juu. Haihitaji utumiaji wa kila siku pia haipunguzi maziwa ya mama wakati wa kunyonyesha.

MAUDHI MADOGOMADOGO

Kupata hedhi kidogo, au matone matone au kukosa hedhi kabisa. Baadhi ya wanawake hutokwa na damu nyingi wakati wa siku za hedhi. Njia hii inaweza kuchelewesha kupata ujauzito kwa baadhi ya wanawake baada ya kuacha kutumia.

KUMBUKA:

Wanawake walio wengi huendelea na hali zao kama kawaida pamoja na kutumia sindano. Maudhi madogomadogo ni kwa baadhi tu ya wanawake.

VIPANDIKIZI (Norplant)

Vipandikizi au Norplant ni njia itumikayo kwa wanawake ambayo iko katika muundo wa vijiti vidogo vya plastiki vyenye dawa ya kuzuia mimba kwa muda wa miaka mitano.

Hivi huwekwa na mtalaamu kwenye sehemu ya juu ya mkono chini ya ngozi kwa kutumia kifaa maalumu. Njia hii hufanya yai lisipevuke na hufanya mji wa mimba uwe na mazingira yasiyoruhusu mimba kutunga. Aidha husababisha ute mzito kwenye shingo ya mji wa mimba na hivyo husaidia mbegu za kiume zisipite.

ANAYESTAHILI KUTUMIA VIPANDIKIZI

Mama anayependa kupumzika kuzaa kwa muda mrefu au ambaye hupata matatizo akitumia vidoge vyenyewe kichocheo cha ‘oestrogen’ anastahili kutumia.

ASIYESTAHILI KUTUMIA VIPANDIKIZI

Ni yule mama anayependa kupata mimba karibu au ambaye hatapendelea mabadiliko ya siku zake za hedhi.

FAIDA ZAKE

Inazuia mimba kwa muda mrefu – miaka mitano, inapunguza siku za hedhi, haipunguzi maziwa kwa mama anayenyonyesha, mama anaweza kupata mimba mara tu vinapotolewa vipandikizi na haingiliani na tendo la kujamiiana.

MAUDHI MADOGOMADOGO.

Baadhi ya akina mama hupata maudhi yafuatayo hasa katika miezi mitatu ya kwanza. Kupata hedhi kidogokidogo, kukosa hedhi kabisa na wengine hutokwa na damu kwa wingi wakati wa siku za hedhi na mwili kuongezeka uzito au kupungua kidogo.

KITANZI (Loop)

Njia hii ya kuzuia mimba huwa ni kifaa kidogo cha plastiki ambacho huwekwa kwenye mji wa mimba ili isitunge. Huzuia yai la mwanamke lisikutane na mbegu za mwanaume.

ANAYESTAHILI KUTUMIA

Mwanamke anayehitaji kupumzika kupata mimba kwa muda mrefu au mwenye mume mmoja mwaminifu. Pia kwa mwanamke asiyeweza kutumia dawa za uzazi wa mpango zenye vichocheo.

ASIYESTAHILI KUTUMIA

Mwanamke anayetokwa na damu nyingi wakati wa hedhi, au aliyewahi kutunga mimba nje ya mji wa mimba. Au mwanamke aliyewahi kupata uambukizo kwenye pango la uzazi katika miezi mitatu iliyopita.

FAIDA

Ipo faida ambayo ni uwezo wa kuzuia mimba mpaka miaka kumi na hakiathiri tendo la kujamiiana. Kifaa hicho kinaweza kuondolewa kirahisi wakati wowote mwanamke anapotaka kupata mimba. Njia hii ni nzuri kwa akina mama ambao hawawezi kutumia njia zenye vichocheo na mama wanaonyonyesha.

MAUDHI MADOGOMADOGO

Kuongezeka kwa damu wakati wa hedhi na pia kuongezeka kwa siku za hedhi. Kutokwa matone ya damu mwanzoni lakini tatizo hili huisha baada ya muda mfupi.

NJIA ZA KUDUMU ZA UZAZI WA MPANGO

Kuna njia mbili za kudumu za uzazi wa mpango. Njia hizi ni kufunga kizazi mwanaume, kufunga kizazi mwanamke, kufunga kizazi mwanaume au mwanamke kunahitajika oparesheni ndogo, njia zote mbili ni za kuaminika salama na ni za kudumu pia ni njia inayomshirikisha mwanaume katika kupanga uzazi.

KUFUNGA UZAZI MWANAMKE NI NINI?

Ni njia ya kudumu ya uzazi wa mpango kwa mwanamke. Hii ni njia inayotumika kwa mama ambaye kwa hiari anaridhika na idadi ya watoto alionao.

FAIDA ZAKE : Njia hii hufanyika mara moja na huduma huchukua muda mfupi sana. Mteja hahitaji kulazwa hospitali na ni ya uhakika na salama pia haiingiliani na unyonyeshaji na mteja halazwi usingizi.

USHAURI NA UJUMBE MUHIMU

Hata hivyo, wake kwa waume watambue kuwa njia hii haiwezi kuzuia maambukizo ya Ukimwi. Wengine wanaweza kuzuia mimba kwa kufuata njia asili, yaani kufuata tarehe kama unavyoona pichani.

Comments are closed.