The House of Favourite Newspapers

Zitto Kabwe Aanika Alichojionea Nairobi kwa Tundu Lissu

0
Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe.
MBUNGE wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe amefunguka na kudai amerudi nchini akiwa na unyenyekevu mkubwa zaidi kwa sababu ya nguvu na ujasiri alioonyeshwa na Mbunge Tundu Lissu pindi alipokwenda kumjulia hali katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya.
 
Zitto ameeleza hayo kupitia ukurasa wake wa Facebook asubuhi ya leo na kusema japo Lissu ameumizwa sana lakini hakuacha kumuonyesha ucheshi licha ya kuwa na maumivu makali aliyokuwa nayo.
“Siku mbili hizi nilizoenda kumuona Lissu zimeniacha nikiwa na mawazo sana, nimerudi nchini nikiwa kwenye unyenyekevu zaidi kwa sababu ya nguvu na ujasiri ambao ndugu yangu amenionyesha licha ya kuwa kwenye maumivu makali. Siyo mara nyingi hapa nchini kusikia tukiongelea ujasiri lakini namfikiria Lissu na vile nilivyojisikia nikiwa pamoja naye Nairobi, najua hivyo ndivyo alivyo.
“Waliomshambulia wamemuumiza kweli na bado wakati tuliokuwa naye amenionesha shukrani, ari na pia ucheshi. Huo ni ujasiri, alichopitia na anachoendelea kupitia Lissu siyo kitu rahisi kwa mtu yeyote kutafakari. Kufikiria hali ile kungeniacha niumie moyo kama asingesema maneno haya kwangu kuwa  ‘tumeshinda. Tumeshashinda”, ameandika Zitto.
Mbunge Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa Makao Makuu ya nchi mjini Dodoma na baadaye kusafirishwa kwenda jijini Nairobi Kenya kwa ajili ya kupatiwa matibabu kufuatia majeraha aliyopata, ambapo mpaka sasa yuko huko kwa matibabu.
Leave A Reply