The House of Favourite Newspapers

Chura ya Snura Yauzwa Kama Njugu!

0

snuramushiSnura Mushi.

STORI:WAANDISHI WETU, WIKIENDA
DAR ES SALAAM! Majanga! Wimbo wa Chura wa msanii anayekuja juu kwa kasi, Snura Mushi licha ya kusitishwa matumizi yake kwa kupigwa marufuku kusikilizwa hadharani au kuonesha video yake, sasa wajanja wametoa CD yake na inauzwa mfano wa njugu mitaani, kwa Sh. 4,000, Wikienda  limeinasa.

Mei 4, mwaka huu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliifungia video ya wimbo huo kwa madai kwamba haiendani na maandili ya Kibongo huku Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) likimtaka msanii huyo kuurekebisha wimbo huo na yeye mwenyewe kujisajili kwenye baraza hilo ili aweze kutambuliwa.

BasataKatibu Mtendaji wa Basata Godfrey Mngereza

WIKIENDA LATONYWA
Wiki mbili zilizopita, baadhi ya wasomaji wa Wikienda walipiga simu chumba cha habari na kuuliza kama video ya Wimbo wa Chura imeruhusiwa kuuzwa au kuoneshwa madukani, kwani kumbukumbu zao, ulizuiwa na hakuna maamuzi ya kinyume na zuio hilo.

Wikienda: “Ile video bado ipo ndani ya zuio, kwani vipi kaka?”
“Sasa mbona CD (VCD) inauzwa mitaani, tena mbaya zaidi si mtaani tu hata kwenye baadhi ya maduka ya Kariakoo pia inauzwa,” alisema msomaji huyo aliyesema anaishi Kimara Suka, Dar. Siku tatu nyuma, msomaji mwingine alipiga simu na kusema makazi yake ni Mabatini jijini Mbeya
naye alisema habari kama hizo, kwamba, Video ya Chura ameiona ikiuzwa kwa siri mitaani.

WIKIENDA LAFANYA UTAFITI
Kufuatia taarifa hivyo, timu ya Wikienda ilizama mitaani na madukani, hasa Kariakoo ili kujiridhisha na madai hayo mazito. Kweli, katika baadhi ya maduka ya kuuza tv Kariakoo, Wikienda lilishuhudia video hiyo ikioneshwa kwenye ‘flat screen’ kubwa huku baadhi ya wapiti njia wakiwa wamepiga kambi kuiangalia huku wakizozana juu ya wimbo wenyewe. Wapo waliotaka itolewe kwa kuwa ilishapigwa marufuku.

Baadhi ya watu waliokuwa wakitoka kwenye duka moja Kariakoo walisikika wakilaani kuoneshwa kwa wimbo huo wakisema kuwa, kama ilipigwa marufuku hakukuwa na sababu ya msingi ya wauza CD hao kuionesha video hiyo kwani ni kukaidi agizo la serikali.

CD YAPATIKANA SINZA
Wikienda liliendelea kufanya uchunguzi wake ambapo liliweza kuipata CD hiyo kwa muuzaji mmoja aliyekuwa akipitisha bidhaa zake nje ya Baa ya Way Side.

WIKIENDA NYUMBANI KWA SNURA
Ili kumsikia Snura mwenyewe anasema nini kuhusu ishu hiyo, Wikienda lilifunga safari hadi nyumbani kwake, Mwananyamala jijini Dar na kuzungumza naye kwa kina kuhusu kuwepo kwa biashara hiyo na kama kuna mkono wake. Kwanza, Snura alionekana kushangazwa sana na kitendo
hicho ambapo alisema hakuwa anajua, lakini akaanika anachokijua yeye.

“Mimi nilitii agizo la Basata na ndiyo maana hata kwenye YouTube niliifuta, ila wajanja waliiwahi kuichukua na kupiga pesa kupitia mgongo wangu. “Watu wakikamatwa huko na polisi mimi simo, maana Chura nimeshamfungia ndani, sasa wao wanaendelea kumuhangaisha awape majanga, naomba nisiunganishwe maana sijui lolote.

“Najua wengi walibani (kuchoma) CD hivyo wanapiga pesa kupitia kazi yangu na hao wanaoitana Chura waache mara moja maana nimesikia wengine wamekamatwa na polisi kwa kuitana Chura,” alisema Snura.

KIONGOZI WA BASATA
Kufuatia sekeseke hilo, juzi gazeti hili lilimtafuta Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mungereza ambaye simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

YALIYOTOKANA NA YATOKANAYO
Kufuatia wimbo huo kuzua sintofahamu kutokana na wanenguaji wake wanavyocheza na maumbo yao, baadhi ya vijana wa kiume wakaanzisha utani wa kumwita mwanamke yeyote Chura jambo ambalo si la kiungwana hivyo, Mei 26, mwaka huu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala liliwataka wanawake kutoa taarifa vituo vya polisi wanapoitwa Chura na vijana pale wanapopita kwenye mitaa yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lukas Mkondya alisema jijini Dar hivi karibuni kuwa, jeshi lake halijapokea malalamiko lakini kama kweli mambo hayo yapo basi aliwataka vijana kuacha mara moja tabia ya kuwaita wanawake Chura na wale watakaoitwa kutoa taarifa.
Imeandaliwa: Hamida Hassan, Mayasa Mariwata na Gladness Mallya.

Leave A Reply