The House of Favourite Newspapers

Jini Mauti-21

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Nikaanza kuangalia huku na kule mle chumbani nilimokuwa peke yangu. Nikaanza kuvuta kumbukumbu ilikuwaje mpaka nikafika pale. Endelea…

kwani nilichokikumbuka ni kwamba ulipita mwaka wa nne sikuwa nimeumwa ugonjwa wowote.
Hapo ndipo kumbukumbu zangu zilipoanza kurudi nyuma kabisa, nikaanza kukumbuka kipindi kile nilichofika shuleni ambapo wanafunzi wenzangu walikuwa wakilia, baada ya hapo wote wakaanza kuninyooshea vidole, kilichoendelea ni kwenda darasani, baada ya hapo, sikujua kitu gani kiliendelea.

Wakati nikifikiria hayo ndipo mlango ulipofunguliwa, mwanamke mmoja, alikuwa mtu mzima akaingia ndani ya chumba kile, alivalia koti jeupe, lilikuwa kubwa na hapa kifuani, upande wa kushoto kulikuwa na kibati kidogo kilichoandikwa Dk. Lucy.
“Umerudiwa na fahamu, kweli Mungu mkubwa,” aliniambia daktari yule huku akiachia tabasamu pana usoni mwake.

“Nipo hospitali gani?”
“Mtakatifu Tabitha,” alinijibu.
“Ipo wapi?”

“Hapa Manzese,” alinijibu tena.
Nilikaa hospitalini hapo nikimsubiri mama aje, wala haikuchukua saa nyingi mama akafika hospitalini hapo, aliponiona, alionekana kufurahi sana na ndipo aliponiuliza ni kitu gani kilitokea mpaka kuwa kwenye hali hiyo.

Sikumficha, nikaanza kumuhadithia kila kitu kilichotokea, alisikitika mno, kila nilipomwangalia, nilijisemea kwamba muda wowote ule angeweza kumwaga machozi yake kitu ambacho kingeniuma sana kwani sikutegemea kuyaona machozi ya mama.
“Pole sana Davina…” aliniambia.

“Asante mama. Baba yupo wapi?” nilimuuliza.
“Amekwenda kazini, tukirudi utamuona,” aliniambia.
Hakukuwa na mwanafunzi yeyote aliyekuja kuniona, nilijisikia mpweke sana hata marafiki zangu wawili niliowategemea, Maria na Anita hawakuweza kufika hospitalini hapo. Moyo wangu uliniuma mno, sikuamini kama mimi ndiye niliyekuwa nikipitia yale au mtu mwingine. Wakati mwingine nilitamani kila kitu kilichokuwa kinaendelea kiwe ndoto na baada ya dakika kadhaa niamke kutoka usingizini.

Ilipofika saa sita mchana nikaruhusiwa kurudi nyumbani. Njiani nilitembea kwa unyonge, kila mtu niliyekuwa nikimuona niliamini kwamba na yeye aliambiwa juu ya kile kilichokuwa kimetokea hivyo watu wote kuniona mchawi.
“Mama….” nilimuita.

“Abee mwanangu.”
“Mudi amekufa?” niliuliza huku nikionekana kutokuamini.
“Ndiyo! Kazi ya Mungu haina makosa,” aliniambia mama, nikaanza kulia.

Ukweli ni kwamba nilimpenda sana Mudi, baada ya Thomas kufariki dunia, mtu ambaye aliuteka moyo wangu vilivyo alikuwa Mudi tu. Sikuamini kilichokuwa kimetokea, kitendo cha kumpoteza Mudi muda mchache baada ya kuanza kufanya mapenzi hakika iliniuma sana.

Wanafunzi na walimu hawakutaka kuwa nami, hawakutaka kunifariji kwani walijua ni kwa jinsi gani nilikuwa karibu na Mudi, matokeo yake, badala ya kunifariji ndiyo kwanza wakanitenga na kuniacha shuleni nikiwa peke yangu.

Baada ya kufika nyumbani, saa moja baadaye mzee Abdallah, baba wa kambo alipokuja mama alimwambia kile kilichotokea. Baba hakuamini kama kweli walimu na wanafunzi, pamoja na elimu yao walikubaliana na maneno kwamba nilikuwa mchawi. Waliona kwamba ninasingiziwa na hata hao watu waliokufa ni kwamba siku zao zilifika.

“Hawa walimu ni wapumbavu sana,” alisema baba huku akionekana kukasirika.
“Tena sana, yaani umtenge mtoto kisa tu mnasema yeye ni mchawi,” alisema mama, wote kwa pamoja walionekana kuwa na hasira mno.

Japokuwa mama alionekana kunitetea sana lakini alikuwa na wasiwasi mno, kila nilipomuona akiwa peke yake, mawazo yalimsonga na alionekana kufikiria mambo mengi sana. Ukweli ni kwamba mama alikuwa na wasiwasi mwingi, kila kitu kilichokuwa kikitokea kilimfanya kuwa na mawazo mno.
“Davina…” aliniita.
“Abee mama.”
Itaendelea wiki ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply