The House of Favourite Newspapers

 Jinsi ya Kuepuka Upungufu wa Nguvu za Kiume!  

MIONGONI mwa matatizo yanayowatesa wengi kwa sasa ni nguvu za kiume.  Tatizo hili hulalamikiwa ama na mwanaume au mwanamke kwa kutofikishwa kileleni na kutofurahia tendo hasa kwa walio kwenye mapenzi.

 

Zipo sababu nyingi kama tutakavyokuja kuona, lakini matatizo haya humuathiri mtu kisaikolojia anapohisi anashindwa kutimiza wajibu wake au mwanamke kujihisi hapati haki yake ya kufurahia tendo.

 

Mtu anaweza kuwa na tatizo dogo ambalo kama ni mshtuko na anapopata mshtuko huo hujikuta tatizo linazidi, hivyo kujikuta mgonjwa yaani ana tatizo. Kwa hiyo ni vema unapotokewa na tatizo hili usikimbilie kutumia dawa hasa za asili na hata za madukani, bali waone madaktari wakufanyie uchunguzi.

 

AINA ZA MATATIZO YA NGUVU ZA KIUME

Tatizo la nguvu za kiume limegawanyika katika makundi mawili; Kwanza ni tatizo la kuzidi kwa nguvu za kiume ‘priapism’.

 

Watu wengi wamezoea kusema tatizo la nguvu za kiume ni upungufu, lakini lipo hili la kuzidi isivyo kawaida na kujikuta mtu anashindwa kufikia mwisho au mshindo. Hali hii tutakuja kuiona kwa undani. Tatizo la pili ni upungufu wa nguvu.

 

Hili ndilo tatizo lililozoeleka miongoni mwa wanaume wengi. Upungufu wa nguvu za kiume ‘impotence’ unaweza kuwa mdogo au mkubwa nao una sababu zake, tutakuja kuziona.

KUONGEZEKA NGUVU ZA KIUME ISIVYO KAWAIDA ‘PRIAPISM’

Hali hii kitaalam huitwa ‘painful abnormal erection of the penis’. Mwanaume mwenye hali hii hulalamika maumivu makali ya uume pale unaposimama na hushindwa kumaliza tendo. Hali hii inaweza kuwa ya muda tu au ikatokea mara mojamoja na wakati mwingine inaweza kuendelea kwa muda mrefu.

 

Chanzo cha tatizo hili ni matatizo au magonjwa ya mfumo wa fahamu, kulazimisha uume usimame kwa kutumia madawa au njia yoyote ile, uwepo wa mawe kwenye kibofu cha mkojo, maambukizi katika njia ya mkojo, maambukizi ya tezi dume, kuziba kwa mishipa ya damu ya vena inayotoa damu kwenye uume kurudisha mwilini na hii huwatokea zaidi wagonjwa wa sikoseli au selimundo. Matatizo ya mfumo wa damu hasa yanayoambatana na kansa ya damu au magonjwa yanayoathiri mfumo wa damu.

MATIBABU

Tiba sahihi ya tatizo hili ni kutafuta chanzo cha tatizo la uume kusimama kwa muda mrefu hadi mtu anapata maumivu. Endapo hali kama hii inatokea, basi epuka kuvaa nguo za kubana au nguo za ndani. Jifunge tu shuka au msuli na endapo utavaa nguo kama suruali au bukta, basi hakikisha uume unauzungushia pamba ya kutosha ili usikwaruze kwenye nguo ngumu na ikaleta kikwazo kitachoongeza maumivu.

 

Mgonjwa apelekwe hospitalini haraka ambapo atapatiwa matibabu. Wengi hutokewa na hali hii kwa kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume bila ya ushauri wa daktari.

 

JINSI YA KUEPUKA UPUNGUFU WA NGUVU ZA KIUME

‘Impotence’. Hali hii huitwa ukhanithi. Hapa mtu anashindwa kabisa kufanya tendo la ndoa kwa kutokuwa na uwezo. Nguvu hupungua sana au zinakwisha kabisa. Upungufu wa nguvu za kiume hutofautiana na ugumba. Katika suala la ugumba, mwanaume huwa hawezi kumpa mwanamke mimba kwani mbegu zake za kiume huwa hazina ubora.

Itaendelea wiki ijayo.

Comments are closed.