The House of Favourite Newspapers

Kwa nini unatapika wakati wa ujauzito?

0

pregnant-womanKutapika wakati wa ujauzito ni hali inayowatokea wajawazito wengi. Ni mojawapo ya dalili za mwanzo za ujauzito. Hali hii hutokea hasa wakati wa asubuhi na hivyo kuitwa Morning Sickness kwa Kiingereza. Hujulikana kama Emesis Gravidarum kwa kitaalam.

Pamoja na kutapika, hali hii huandamana na hali ya kusikia kichefuchefu na kutopenda harufu za baadhi ya vyakula.

Harufu au baadhi ya vyakula huchangia kwa mjamzito kutapika wakati mwingine. Kutapika na kichefuchefu hutokea hasa katika miezi ya mwanzo ya ujauzito, kadiri ujauzito unavyokua hali hii hupungua na kuacha. Kwa wajawazito wengi hali hii huacha ujauzito unapofikisha miezi 4 (wiki 16 – 18), wachache wakienda mpaka miezi 5.

Kutapika huku huwa ni kwa kawaida na hutokea hasa wakati wa asubuhi, hupungua kadiri siku inavyoendelea. Mara nyingi huambatana na hali ya kichefuchefu. Baadhi ya vyakula au harufu huweza kusababisha  kutapika. Mjamzito huweza kuendelea na shughuli zake zingine na kupata milo ambayo haimsumbui. Baadhi ya wajawazito hupatwa na hali ya kutapika sana zaidi ya kawaida. Kutapika huko kunaambatana na kudhoofu mwili.

Kutungwa kwa mimba huleta mabadiliko mbalimbali ya kihomoni mwilini mwa mjamzito. Mabadiliko haya huuwezesha mwili kumtunza mtoto aliyepo tumboni. Sambamba na mtoto kukua, homoni hizi huleta hali ya kujisikia kichefuchefu na kutapika.

TIBA

Ni vigumu kuitibu na kuindoa hali hiyo kabisa hivyo ni muhimu kwa mjamzito kupata mlo na maji ya kutosha kwa ajili yake na mtoto. Anywe maji kwa wingi au vinywaji vyenye maji kwa wingi. Anaweza akachanganya au akatengeneza juisi ya matunda ili impe ladha aipendayo.

Mjamzito apate mlo wa kutosha ili mwili upate nguvu na virutubisho muhimu. Anaweza akawa anakula chakula kidogo kidogo mara nyingi zaidi hasa pale anaposumbuliwa sana na kichefuchefu.

Mjamzito aepuke harufu au vyakula vinavyomletea kichefuchefu na kutapika. Ikiwa majamzito anatapika sana ni muhimu aonane na daktari.

Leave A Reply