The House of Favourite Newspapers

Magufuli kanikata stimu, dah!

0

Dah nimechanganyikiwa kabisaaa. Akili haifanyi kazi, yaani dah hata sijui nianzie wapi. Picha imekuwa chengachenga kabisa. Unajua kiukweli, nilikuwa nimepanga kuwa nianze wiki hii mipango ya harusi yangu, nilikuwa nataka harusi iwe mwezi wa sita mwaka kesho, nilishatayarisha bonge ya plani, nilikuwa nimeipanga kisayansi kabisa. Sasa mambo yanaharibika mbele yangu na sina la kufanya, nimechanganyikiwa.

Kuna mtoto mmoja wa kike mtaani kwetu, wengi mnamfahamu maana anaonekana kwenye runinga karibu kila wiki na kwenye magazeti ndiyo hakosi, mtoto anawaka, guu guu, sauti kama kinanda, shepu ya katalogi. Sasa huyo ndiye niliyepanga kumuoa, nilipanga harusi iwe ya kiwango cha kimataifa, yaani jambo hili lingetikisa vyombo vya habari kwa muda mrefu.

Hata baada ya harusi vyombo vya habari vingetufuatilia sana, mtoto wetu naye angekuwa maarufu, tungemtumia kwenye matangazo na kukusanya mkwanja wa kueleweka, picha nilikuwa nimeipanga kwa kuangalia mipango ya muda mfupi na muda mrefu. Yaani kila kitu nilikwishakipanga vizuri sana sasa dahh picha inaungua taratibu.

Yaani ilipotangazwa tu kuwa mjomba wangu kashinda Ubunge, nikajua sasa maisha yangu yanabadilika, nilianza kuimba ule wimbo wa Vijana Jazz Band unaitwa Umaskini Bye Bye. Mimi na mjomba tuko karibu sana tangu nikiwa mdogo, mjomba wangu alikuwa akinipenda sana.

Niliona wazi kabisa kuwa mjomba wangu atachaguliwa kuwa waziri, tena ikawezekana hata kuwa waziri mkuu. Sasa kasheshe lilianza baada ya kuona kwanza mjomba amekwisha ukosa uwaziri mkuu, na sasa nimemsikia rais kafuta safari za nje za mawaziri kabla hata hajawataja, yaani ndoto ndiyo imeharibika kabisaaa.

Unajua huyu mtoto kwa kweli sijaongea naye, nilikuwa nangoja mjomba akichaguliwa kuwa waziri ndiyo nimuibukie na kumhakikishia kuwa maisha ya kifahari akikubali tu kuolewa na mimi. Harusi yetu yetu ingekuwa Uswisi, hanimuni Australia, na kote huko mjomba angekuwa mgeni rasmi, sasa mkuu wa nchi katangaza hakuna safari za nje, tena kaanza hata kupunguza gharama za sherehe, ni wazi ndoto yangu haitatimia hata mjomba akipata zari la kuwa waziri. Ndiyo mjue sioi tena hivyo, dahh, kweli Hapa Kazi Tu!

Leave A Reply