The House of Favourite Newspapers

(Malaika wa Giza)-52

0

Watoto wawili mapacha, Arianna na Brianna wanazaliwa katika familia ya Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa. Kwa bahati mbaya wakati wakiwa bado wadogo, familia yao inakuwa miongoni mwa watu wanaokumbwa na shambulio baya la kigaidi linalotokea kwenye kituo kikubwa cha biashara nchini Kenya, Kikuyu Mall.

Wazazi wao wote wawili wanapoteza maisha katika tukio hilo na huo unakuwa mwanzo wa mapacha hao kutengana. Arianna anarudishwa jijini Dar es Salaam wakati Brianna anakulia kwenye mtaa wa watu maskini wa Mathare jijini Nairobi.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kumuoa lakini Arianna anakula njama na Diego na tayari wamefanikiwa kumuibia mfanyabiashara huyo mamilioni ya fedha na kutengeneza mazingira ionekane kama wamevamiwa na majambazi.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Ulikuwa wapi wakati nyumba inavamiwa?”

“Afande mimi sielewi chochote maana usiku kucha nipo kwenye lindo langu kama kawaida na sijaona dalili zozote za majambazi. Kama ni kuvunja si wangeanzia hapa kwenye geti kubwa?”

“Kwa hiyo unataka kusema hii milango imejivunja yenyewe? Na hizi damu zimetoka wapi? Mke wa Msuya ametekwa, fedha zimeporwa halafu wewe unatoa majibu mepesi, lazima utakuwa unajua kilichotokea, utakaa ndani mpaka utakapoamua kusema ukweli. Muwekeni ndani huyu, anatuletea mzaha,” mkuu wa kituo kikuu cha polisi alitoa maagizo ya mlinzi wa nyumba hiyo kuwekwa nyuma ya nondo.

Kwa jinsi mazingira yalivyokuwa, hakuna ambaye angeweza kumuamini mlinzi huyo, ni kweli usiku kucha alikuwepo eneo lake la kazi japokuwa alipitiwa na usingizi kwa saa chache baada ya kuvuta sigara aliyopewa na Diego wakati familia hiyo ikirejea nyumbani kutoka kwenye Hoteli ya Amazon walikoenda kula chakula cha usiku na watoto wa bilionea huyo pamoja na mfanyakazi mmoja wa ndani.

“Hebu mleteni huyo kijana aliyetoa taarifa,” alisema mkuu wa kituo, Diego ambaye bado alikuwa akiendelea kuandikisha maelezo kaunta, akiwa na wafanyakazi wote wawili wa familia hiyo pamoja na watoto wa Msuya, aliingizwa kwenye chumba maalum cha mahojiano.

“Bila shaka wewe ndiye uliyetoa taarifa polisi muda mfupi baada ya tukio.”

“Ndiyo afande.”

“Hebu tuambie ilikuwaje?”

“Nikiwa nimelala chumbani kwangu, nilisikia kishindo kikubwa cha mlango kuvunjwa kisha wanaume sita wenye silaha, walioziba nyuso zao wakaingia na kunizunguka pale kitandani,” Diego alidanganya huku akiwa makini asijichanganye kwenye maelezo yake.

“Ikawaje?”

“Wakawa wananishinikiza niwaoneshe chumbani kwa Msuya vinginevyo wataniua. Kwa kuwa walikuwa na silaha, sikuwa na namna zaidi ya kukubali.”

Nilipowaelekeza, mmoja kati yao aliniweka chini ya ulinzi wale wengine wakavunja mlango mkubwa na kuingia ndani. Nikawa naendelea kusikia vishindo vya milango kuvunjwa ndani.

“Baadaye nikasikia kilio cha mke wa bosi ndani, wale majambazi wakatoka naye huku wakiwa wanamburuza na kuondoka naye kwa kutumia ngazi waliyokuwa wameiegamiza kwenye ukuta wa fensi, hata siamini kama nimenusurika,” alisema Diego na kujikamua machozi ya uongo, askari aliyekuwa amekaa pembeni ya mkuu wa kituo akawa anaandika kila kitu kwenye faili la rangi ya khaki.

“Wewe ni shahidi muhimu kwenye hii kesi, hutakiwi kusafiri kwa sasa kwa sababu tunaweza kukuhitaji muda wowote na ni lazima uwepo. Tumeelewana kijana?” mkuu wa kituo alimwambia Diego, kauli iliyomchanganya sana kichwa chake. Tayari alishakuwa na mpango wa kutokomea siku hiyohiyo na kwenda kuungana na Arianna ili watoroke pamoja.

Baada ya kutoa maelezo hayo, Diego na watoto wa Msuya pamoja na wafanyakazi walirejea nyumbani wakiongozana na walinzi wa kampuni ambayo ndiyo iliyokuwa na mkataba wa kulinda nyumba hiyo. Taratibu za kumtaarifu Msuya kilichotokea nyumbani kwake baada ya yeye kusafiri zikaanza kufanywa mara moja.

***

“Haloo!”

“Haloo! Bila shaka wewe ni Msuya!”

“Ndiyo! Nipo safarini nje ya nchi, nani mwenzangu?”

“Unazungumza na kamanda mkuu wa kampuni ya Nyati Security inayolinda nyumbani kwako.”

“Eeh! Nambie kamanda, mbona leo unanipigia simu? Kwema huko?”

Kuna taarifa mbaya, nyumbani kwako kumevamiwa usiku wa kuamkia leo na mkeo ametekwa, hivi tunashirikiana kwa karibu na jeshi la polisi kumtafuta na kuhakikisha waliohusika wanakamatwa.”

“Unasemaje? Hebu acha masihara bwana. Haloo! Haloo!” Msuya aliyekuwa nchini Marekani akiendelea na biashara zake, akiwa ametoka kwenye duka kubwa la vito vya thamani, The Market NYC alikopeleka mzigo mkubwa wa madini ya Tanzanite aliyotoka nayo nchini Tanzania, alichanganyikiwa mno baada ya kusikia taarifa hizo.

Akawa hataki kuamini kwamba alichokuwa anakisikia ni kweli kimetokea. Akiwa anahangaika kutaka kuipiga tena ile namba ya mtu aliyempa taarifa, simu yake ilianza tena kuita, alipotazama namba ya mpigaji, ilikuwa na ‘code’ iliyoonesha kuwa nayo inatoka nchini Tanzania. Harakaharaka akapokea.

“Haloo!”

“Haloo shemeji! Ni mimi Diego, kuna matatizo huku nyumbani.”

“Diego! Diego, eti ni kweli mke wangu ametekwa?”

“Ni kweli shemeji, nimekupigia simu ili nikupe hizo taarifa, tumetoka polisi kutoa maelezo sasa hivi,” alisema Diego, kauli iliyozidi kumchanganya Msuya, akakata simu na kutafuta sehemu ya kukaa kwani alikuwa akihisi kizunguzungu kikali. Alitamani kama angekuwa na mabawa aruke muda huohuo mpaka nyumbani kwake lakini hilo halikuwezekana.

K

utokana na uzito wa ishu yenyewe, ilibidi Msuya avuje ratiba zake zote, muda huohuo akaanza maandalizi ya safari ya kurejea Tanzania kwa dharura. Kwa bahati nzuri, alipata ndege lakini alitakiwa kusubiri kwa saa nne kabla ya safari kuanza, muda ambao kwake aliuona sawa na miaka kadhaa. Hatimaye saa nne ziliisha na safari ya kurejea nchini Tanzania ikaanza huku Msuya akionesha kuwa na mawazo mengi ndani ya kichwa chake.

***

Baada ya kufanikiwa kuondoka na mzigo wa mamilioni ya fedha pamoja na madini ya Tanzanite, Arianna aliondoka na gari dogo walilokuwa wamelikodi maalum kwa ajili ya kumsafirisha na kumvusha mpaka ng’ambo ya pili ya mpaka kati ya Tanzania na Kenya.

Kwa jinsi walivyokuwa wamekubaliana, ilitakiwa avuke mpaka usiku huohuo na kwenda kumsubiri Diego upande wa pili wa mpaka, ili akishatengeneza mazingira ya kuonesha kwamba wamevamiwa na majambazi na msichana huyo kutekwa, watoroke pamoja na kwenda kuanza maisha mapya sehemu ambayo haitakuwa rahisi kwa mtu yeyote kujua walipo.

Kila kitu kilienda vizuri, kwa kuwa dereva waliyemkodi alikuwa na uzoefu wa kufanya biashara za magendo mpakani, alifanikiwa kumvusha salama Arianna mpaka Namanga ya Kenya bila kuonekana na polisi.

Kwa kuwa tayari alishalipwa nusu ya fedha zake alizokuwa anadai, Arianna alimmalizia kiwango kilichobakia kisha akateremka kwenye gari na kuagana naye.

Kwa kuwa Diego alikuwa na uzoefu wa kufanya ‘dili feki‘ za namna hiyo, alimuelekeza Arianna kwamba akishashushwa na dereva teksi huyo, atafute gari jingine ambalo litampeleka mji unaofuatia ili hata akiamua kuwachoma kwa polisi, isiwe rahisi kukamatwa.

 

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

Leave A Reply