The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu 09

6

WATOTO wadogo Kevin na Catarina wamejikuta katika penzi zito kwenye umri mdogo, jambo ambalo wazazi wao hawakubaliani nalo kabisa, wanafanya kila njia kuzuia jambo hilo.Wanamhamisha Catarina nchini Uganda kwa masomo na Kevin anapelekwa Shule ya Bweni ya St. Joseph jijini Dar es Salaam.

Kitendo hiki hakikufanikiwa kulizuia penzi linalochipuka kwa kasi mioyoni mwao, Catarina aliporejea nchini kwa mapumziko, jambo la kwanza alilolifanya ni kumtembelea Kevin shuleni kwao ambako alizuiwa kumwona, akaamua kusubiri mpaka wanafunzi watoke.

Akamwona akiwa ndani ya basi la shule na kumwita, Kevin akaamua kuruka basi likiwa kwenye mwendo kasi na kupiga kichwa chake ardhini alipoanguka! Ameumia ubongo na kupasuka bandama, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wamemfanyia upasuaji mkubwa, yupo wodini akiwa hajitambui na matumaini ya kupona ni kidogo.

Wazazi wa Kevin hawataki kabisa kumwona Catarina wala kumruhusu akifikie kitanda cha mtoto wao, hata hivyo Catarina anatumia mbinu na kufanikiwa kumtembelea Kevin kitandani, akamwombea na kuweka kadi pamoja na maua akimwomba muuguzi aliyemsaidia asiwaeleze wazazi wa Kevin kuwa yeye alikuja na pia kadi isifunguliwe na mtu yeyote mpaka Kevin akirejewa na fahamu zake.
Je, nini kitaendelea?SONGA NAYO…

ALIONDOKA chumba cha wagonjwa mahututi moyo ukiwa umepondeka sababu ya maumivu aliyokuwa nayo, taswira ya Kevin akiwa hajitambui, uso ukiwa umevimba na kichwa kimefungwa bendeji nzito, ilimfanya Catarina awe na maumivu yasiyoelezeka. Moyoni mwake alikuwa akisali kimyakimya kumwomba Mungu anusuru maisha ya Kevin, alitamani muujiza mmoja tu wa kurejea hospitali siku iliyofuata na kumkuta Kevin ameketi kitandani, uso umejawa tabasamu, anyanyuke na kumkumbatia.

“God make it happen!”(Mungu fanya hilo litokee!) aliwaza akikaribia stendi ya teksi.
Akachagua moja iliyokuwa mbele ya nyingine na kuingia ndani, ikatokea kwamba alikuwa ni dereva yuleyule aliyembeba mara ya mwisho alipoondoka hospitali ya Muhimbili, wakakumbukana na kumwomba ampeleke nyumbani, baada ya hapo hakuongea kitu kingine tena mpaka dereva alimpomshtua.
“Ni kulekule Masaki?”

“Hapana, nenda Victoria, unapafahamu Abla Apartments?”
“Ndiyo, kwa Shehe Nassor pale?”
“Kama unapafahamu basi ni hapohapo.”

Dereva ambaye tayari alishafika taa za Salenda alikata kushoto kuingia barabara ya Ali Hassan Mwinyi na kusonga mbele mpaka Morocco, akavuka taa akipita eneo la Regent Estate hatimaye Maghorofa ya Abla Apartment yakaanza kuonekana kwa mbele, alipoyafikia akakata kulia na kuingia hadi ndani, Catarina akamlipa na kumshukuru kisha kushuka na kuingia kwenye lifti na kumpeleka hadi ghorofa ya sita.

Wazazi wake walikuwa hawajarejea kutoka kazini, kwani saa ya ukutani ilisomeka saa saba na nusu tu, akaingia chumbani kwake baada ya kuwasalimia wafanyakazi wa ndani, huko aliendelea kufanya kazi yake ya kila siku; kusoma kumbukumbu ambazo Kevin aliandika kwenye daftari lake ili kufahamu ni kiasi gani kijana huyo alimpenda lakini alishindwa kusimama kama mwanaume katika nafasi yake na kuzielezea hisia alizokuwa nazo moyoni.

“Akirejewa na fahamu tu, nitakuwa mtu wa kwanza kufungua mdomo wangu na kumweleza ninampenda, sitaona aibu na sitajali kama ataniona ni mhuni au la! Nampenda Kevin, kwa nini niitese nafsi yangu? Yeye peke yake ndiye anatakiwa kuwa mume wangu wa maisha yote, wazazi hata wafanye kitu gani hawawezi kuzuia jambo hili kutokea, namwomba tu Mungu wangu amnusuru Kevin na kifo, nitaumia mno akifa kwani nitakuwa nimesababisha kifo cha mtu ninayempenda!” aliwaza Catarina akipitia daftari la kumbukumbu ya Kevin.

Jioni wazazi wake walirejea kutoka kazini na kuendelea kumfariji, hawakujua kabisa kwamba alitoka kwenda hospitali ya Muhimbili na Catarina hakuwa tayari kuwaeleza kilichotendeka wakiwa kazini, alijua hakuna ambaye angemuunga mkono katika jambo hilo.
“Umeendeleaje leo?”
“Naendelea vizuri!”

“Endelea kuwa imara, usiwaze wala kulia kupita kiasi, Mungu anajua yote!” baba yake ambaye alikuwa rafiki mkubwa wa Catarina alisema.
“Nitafanya hivyo baba!”

Wazazi wake walijitahidi sana kumpa nasaha, walipoona zao hazitoshi walilazimika kumtafutia mtaalam wa saikolojia kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili ambaye alikuja kila siku jioni kuzungumza naye katika kumjenga ili asiathirike zaidi, ambacho wazazi wake hawakukifahamu ni kwamba kila siku iendayo kwa Mungu, Catarina wakiwa kazini, aliondoka nyumbani kwenda Muhimbili kumwona Kevin.

Alichokifanya akiwa Muhimbili ambacho kiligeuka kuwa desturi yake ni kununua kadi, maua na kwenda nayo chumba cha wagonjwa mahututi ambako wauguzi karibu wote walimzoea na kumpenda wakawa tayari kumpa kila aina ya ushirikiano amwone Kevin kitandani kwake.

Maua hayo pamoja na kadi, aliyaweka kando ya kitanda kwenye meza ndogo, akampiga Kevin busu shavuni kisha kumwita mara kadhaa ili aamke lakini kama ilivyotokea siku ya jana yake; Kevin wala hakujitingisha, macho yake yalikuwa yameangalia darini yakiwa hayafumbi wala kupiga kope. Mwisho kabisa alipiga magoti chini na kumwomba Mungu amrejeshe Kevin duniani ili waweze kutimiza ndoto zao.

Kwa siku ishirini na tano Catarina alikwenda hospitalini na kufanya hivyo, maua yalipoharibika yalitupwa lakini kadi zilikusanywa zikitunzwa mpaka Kevin ambaye kwa mujibu wa madaktari uwezekano wa kurejewa na fahamu ulikuwa mdogo, azinduke na kurejewa na fahamu zake ndipo angezifungua kadi hizo na kuzisoma.

Siku ya ishirini na sita na kuendelea Catarina hakuonekana tena hospitali, wauguzi wakaanza kuulizana ni kwa nini alikuwa hafiki lakini hapakuwa na mtu yeyote mwenye jibu la swali hilo! Siku ya thelathini na moja tangu Kevin alazwe hospitalini, kitanda chake kikiwa kimezungukwa na ndugu waliofika kumjulia hali mchana huo wa saa nane,

LIFUNGUA MACHO!
“Heee! Amefumbua macho au nimeona vibaya?” mama yake aliongea kwa sauti ya juu.
“Macho yako hayakudanganyi kweli?” baba yake aliuliza, watu wote wakageukia kwenye kichwa cha Kevin kuhakikisha kilichodaiwa kutokea.
“Hee! Kweli! Muone! anapiga kope!” mmoja wa ndugu akajikuta akitamka maneno hayo kwa furaha.

“Nesi! Nesi! Nesiiii!” mama yake Kevin aliita kwa sauti ya juu.
Wauguzi wakaja wakikimbia mpaka kwenye kitanda na kuuliza kilichotokea, walipoelezwa na wao kuthibitisha waliamua kumpigia simu Dk James Mabula aliyefika kitandani hapo ndani ya dakika kumi na kushuhudia Kevin akizungusha macho yake huku na kule ndani ya wodi ya wagonjwa mahututi bila kuongea chochote.

“Ninyi mnasali dhehebu gani?”
“Lutherani!”
“Huwa mnasali?”
“Ndiyo.”

“Basi Mungu wenu ana nguvu kubwa san…” daktari hakuimaliza sentensi yake mpaka mwisho akasikia kelele kutoka mdomoni mwa Kevin akijitupa huku na kule kama mtu aliyetaka kuruka kutoka kitandani.

“Unajua huyu anakumbuka kilichotokea siku alipopata ajali, hebu mshikilieni!”
“CATARINAAAAA! CATARINAAAA! NJOOO! NAKUPENDA SANAAAAA!” yalikuwa ni maneno kutoka mdomoni mwa Kevin.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Ijumaa katika Gazeti la Championi Ijumaa, usisahau kukata kuponi yako ya Shinda Nyumba, huu ni ukweli, wewe ndiye unaweza kuwa mshindi wa nyumba hii, ukajikuta unamiliki nyumba ya kisasa jijini Dar es Salaam.

6 Comments
  1. Donnie says

    Kaazi kweli kweli….

  2. breckii says

    huu mfumo c mzuri hadithi zingine hazipatikani

    1. Global Publishers says

      zote zinapatikana

      1. Erickson says

        hazpatikani kama mwanzo

        1. Global Publishers says

          ingia kwenye makala, click kwenye mikasa utazipata zoteeee

  3. Urio says

    Even though I didn’t follow it from the bigining, I wish to bigin it coz it’s very interesting story.

Leave A Reply