The House of Favourite Newspapers

Mtoto wa mjini naishi kama digidigi!

1

Ukisikia sentensi imeanza na Wahenga walisema…usiipuuze. Hawa wazee wa zamani walitunga misemo enzi hizo wakati hata baiskeli hawaijui, lakini maneno yao mpaka leo kwenye ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia yana uzito uleule.

Mimi hapa bosi wa mabosi, pedeshee wa mapedeshee ambaye katika kila nyimbo nne za nchi hii lazima tatu zinitaje, leo hii nikisikia jina langu likitajwa najificha uvunguni mwa kitanda, presha inapanda. Mimi, niliyekuwa hata maji lazima ninywe yaliyotoka nje ya nchi, leo naogopa hata kununua juisi ya Kibongo.

Kweli wahenga walikuwa sawa waliposema hujafa hujaumbika. Yaani tangu wiki iliyopita nashindwa hata kutoka nje ya nyumba yangu, simu nazima mchana kutwa nawasha usiku tu maana naogopa ntaulizwa maswali au ntaitwa na vyombo vya dola, sina hamu kabisa na maisha, nimekonda utadhani nilikuwa mgonjwa, nguo sijabadili wiki sasa, harufu ya kijasho inanisindikiza.

Labda nijitambulishe, mimi nilikuwa mmojawapo wa watoto wa mjini, naweza kusuka mpango nikapiga dili la bilioni kwa wiki, pesa kwangu siyo ishu, ishu ni namna ya kuitumia. Naweza kutumia kwa starehe tu hata milioni tano kwa siku, chochote nilichotaka nilipata.

Mabinti watano maarufu wanaishi kwenye nyumba za gharama nilizowapangia, na wanaendesha magari ya kisasa niliyowanunulia, achana na wale zaidi ya kumi ambao nilishawapiga kibuti, nikawaachia na vigari vyao. Ukumbi gani wa starehe ambao hawanijui?

Nina nyumba zangu nyingi mjini hapa, hivyo silali nyumba moja siku tatu mfululizo. Lakini mambo yamebadilika ghafla. Kaja mtu mmoja anaitwa mtumbua majipu, kaharibu cheni zangu zote za madili, jamaa zangu wengine wamo ndani, wengine wameingia mitini, ni wazi wakati wowote jina langu litatajwa.

Nimekuja kujificha huku uswahilini kwenye nyumba ya mjomba wangu, mjomba mwenyewe kaninunia eti nilikuwa simjali, kitu ambacho ni kweli nisikatae.

Kinachoniudhi kuliko yote, hawa mabinti niliokuwa nawapa raha utadhani hawasomi magazeti, nikifungua simu ni meseji zao tu, huyu anataka kwenda Dubai, huyu eti twende Sauzi wikiendi, mwingine anataka kufanya birthday na wenziye kwenye hoteli Bagamoyo, hivi hawajasoma alama za nyakati?

Huyu mwingine nasikia kaenda kuringishia gari nililomnunulia kwenye magazeti, gari lenyewe lina magumashi, nampigia simu aachane na mchezo huo anasema lazima awanange wenziye, yaani angejua huku mwenziye tumbo la kuhara limenibana angelichoma moto lile gari.

Kweli hujafa hujaumbika, niombeeni mwenzenu yakipita haya salama sirudii tena, ntarudi kwetu nikalime mananasi.

1 Comment
  1. Donnie says

    Hahahah…

Leave A Reply