The House of Favourite Newspapers

Neema yazidi kumfuata Ngoma Yanga

Sweetbert Lukonge na Nicodemus Jonas

NEEMA imezidi kumfuata straika wa Yanga, Donald Ngoma, baada ya klabu nyingine kutoka Uswisi nayo kuonyesha nia ya kumhitaji, ukiachana na Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini.

Katibu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, ameiambia Championi Jumamosi kuwa, amesikia taarifa za Mamelodi kumtaka Ngoma, raia wa Zimbabwe, lakini bado haijawa rasmi kwani haijamfikia mezani kwake.

“Hata mimi nasikia tu kuhusu hizo habari za Ngoma kutakiwa na Mamelodi, lakini bado hawajawasiliana nasi rasmi ili kuanza mchakato wa usajili,” alisema Tiboroha.

Wakati Tiboroha akisema hayo, taarifa nyingine kutoka ndani ya Yanga zilizotoka jana zimedai klabu nyingine ya Uswisi nayo imeonyesha nia ya kumhitaji Ngoma kwa ajili ya majaribio ya kucheza soka la kulipwa.

“Hiyo klabu ya Uswisi inayomtaka Ngoma ni ya Ligi Kuu Uswisi, hii ndiyo iliyokuwa ya kwanza kumhitaji straika huyu lakini nashangaa taarifa ya kwanza imekuwa ile ya Mamelodi,” kilisema chanzo chetu.

Hata hivyo, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, ameshasisitiza kutokuwa tayari kumuachia Ngoma aondoke kikosini mwake kwani ana mpango naye wa muda mrefu katika michuano ya kimataifa.

“Tuna ligi kuu, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya, unamuachiaje mtu kama Ngoma kwa wakati huu? Ngoma haondoki na sitakuwa tayari kumuachia jueni hivyo,” alisema Pluijm, raia wa Uholanzi.

Comments are closed.