The House of Favourite Newspapers

Pluijm: Jamani ehee sasa basi

0

pluijm1

Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm.

Nicodemus Jonas, Dar es Salaam

YANGA kesho Jumapili inacheza na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kupata sare moja na kufungwa mara moja, sasa kocha wake Hans van Der Pluijm amesema inatosha na kilichobaki ni ushindi tu.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara wanaingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kuambulia pointi moja tu katika mechi mbili ilizocheza nje ya Dar es Salaam hivi karibuni.

kocha-wa-yanga-hans-van-der-pluijm-kulia-na-msaidizi-wake-juma-mwambusi_ljoz3t1bxy5u1wsl6o34xdnmm

Yanga ilianza kwa kupoteza dhidi ya Coastal Union ilipofungwa mabao 2-0 wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, halafu katikati ya wiki hii ililazimisha sare ya mabao 2-2 na Prisons jijini Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine.

Katika kuhakikisha Yanga inarejea kwenye njia ya kusaka ubingwa, Pluijm ameliambia Championi Jumamosi kuwa, sasa ni muda wa kusawazisha makosa waliyoyafanya katika mechi mbili zilizopita.

“Ni mchezo ambao lazima tushinde, sikupendezwa na matokeo ya mechi mbili zilizopita, nataka tusawazishe makosa yale maana kidogo yaliondoa hali ya wachezaji kujiamini.

“Kulikuwa na makosa ambayo yangeweza kuepukika na lazima yafanyiwe kazi kabla ya mchezo na JKT ambayo siyo vema kuyaweka wazi kwa umma. Muhimu ni kuhakikisha mchezo huo tunashinda ili kurudisha ari ya kikosi,” alisema Pluijm ambaye juzi Alhamisi alikuwa uwanjani kushuhudia wapinzani wake wakilala mbele ya Mbeya City kwa mabao 2-1.

Kocha wa JKT Ruvu, Abdallah Kibadeni alisema: “Japokuwa kikosi changu kinalegalega, tutapambana na Yanga tupate pointi, Yanga haina tofauti sana na Simba kiuchezaji, hivyo tunajiandaa kuhakikisha hatufungwi kizembe.”

Kesho pia kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya kutakuwa na mchezo wa upinzani wa jadi ambapo Mbeya City itacheza na Prisons.

Mbeya City ipo nafasi ya tisa ikiwa na pointi 17 katika mechi 17 wakati Prisons ipo nafasi ya saba ikiwa na pointi 28.

Kocha wa Prisons, Salum Mayanga, alisema: “Ligi ni ngumu na kila mchezo ni mgumu, hivyo tunaingia uwanjani tukiamini tunakwenda kukutana na ugumu.”

Kocha Msaidizi wa Mbeya City, Mohamed Kijuso, alisema: “Akili yetu tunaihamishia katika mchezo wetu dhidi ya Prisons, huu ni mchezo mgumu lakini tutapigana kuhakikisha tunaendeleza kasi ya ushindi.”

Mjini Shinyanga, kesho Jumapili, Simba inayoshika nafasi ya pili katika ligi ikiwa na pointi 39, itacheza na Kagera Sugar inayoshika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 15 kwenye Uwanja wa Kambarage.

Kocha wa Simba ambaye amewahi kuinoa Kagera Sugar, Jackson Mayanja, alisema: “Kagera wanaweza kuwa wanazijua mbinu zangu, sasa nipo Simba kuna mbinu nyingine tofauti kabisa, tutapambana tushinde ugenini.”

Kocha wa Kagera, Adolf Rishard, amesema: “Sisi hatuangalii Simba imefunga idadi gani ya mabao, tumetega mitego yetu ambayo tunaamini watanasa. Hatutaki kupoteza mechi.”

Leo katika ligi hiyo kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, African Sports watacheza na Stand United, wakati kesho Jumapili: Ndanda V Mtibwa Sugar (Nangwanda), Toto Africans V Coastal Union, Majimaji V Mgambo na Azam V Mwadui.

Leave A Reply