The House of Favourite Newspapers

Simba Hii Tishio, Azam Yagoma Kucheza Nayo

0

SIMBA DAY (19)

Mshambuliaji mpya wa Simba, Mrundi Laudit Mavugo.

Nicodemus Jonas, Dar es Salaam
KIWEWE? Katika kile kinachoonekana kuwa Simba ni tishio msimu huu, uongozi wa Azam umewasilisha barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutaka mechi yao dhidi ya Simba ya mzunguko wa tano ipigwe kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Chamazi badala ya Taifa.

Makamu Mwenyekiti wa Azam, Iddrisa Nassor ‘Father’ amefunguka kwa mapana kuhusu barua yao hiyo ambayo pia msemaji wa TFF, Alfred Lucas amekiri kuipokea, wakisema kuwa safari hii wanataka kukwepa mazingira ya kuzibeba Simba na Yanga ambazo hucheza mechi nyingi nyumbani kuliko timu nyingine.

SIMBA DAY (2)

Kikosi cha Timu ya Simba.

Simba na Yanga zinacheza jumla ya mechi 19 kwenye Uwanja wa Taifa (nyingine zitacheza Uhuru) badala ya mechi 15, ambazo zinatakiwa kuchezwa kwa kila timu kwenye uwanja wake wa nyumbani kutokana na mechi za Azam, JKT Ruvu, African Lyon na Ruvu Shooting kuchezwa nyumbani kwao .

Father aliongeza kuwa wao wanalindwa na sheria mpya ya leseni ya klabu ‘club license’ inayozitaka timu zote kuwa na uwanja wake wa nyumbani unaotambulika na akasisitiza kuwa kama TFF watapuuzia ombi lao, mechi ya mzunguko wa tano dhidi ya Simba hawataingiza timu uwanjani.

SIMBA DAY (15)

Wachezaji wa Simba wakimuomba Mungu baada ya kushinda bao katika moja ya mechi za Ligu Kuu Bara.

“Imefika wakati tunataka tuwe na ligi ya haki na usawa. Tumewapa barua TFF kuwataarifu mechi zetu zote tunataka msimu huu zichezwe Chamazi.

Tutaanza na mechi yetu na Simba, tutaingiza kikosi Chamazi, wao wasipokuja shauri yao, tunalindwa na sheria ya Fifa,” alisema Father.

Lucas amelithibitishia Championi Jumatano, kuwa siyo Azam tu, pia wanajeshi wa JKT Ruvu na Ruvu Shooting ya Masau Bwire wamefikisha barua kutaka mechi zao zote dhidi ya Simba na Yanga kupigwa Mlandizi.

SIMBA DAY (8)

Mashabiki wa Simba wakiendelea kufanya yao Taifa.

“Wamefikisha barua lakini ni jambo lisilowezekana kutokana na mazingira ya viwanja na usalama wa mashabiki. Sheria iko wazi, kanuni No 6 inasema timu mwenyeji ama msimamizi (TFF) inaweza kuhamishwa uwanja kwa sababu za msingi.

Angalia uwanja kama Mlandizi, uwanja una uzio wa mabati na uwanja wenye uwezo wa kubeba watu 7,000 tu, unafikiri nini kitatokea katika mechi kama ya Simba ama Yanga itachezwa hapo?” alihoji Lucas na kusema kuwa hawawezi kukubaliana nao.

Azam imekuwa ikitumia Chamazi katika mechi zote za kimataifa ambapo tayari timu kama Etoile du Sahel (Tunisia), El Marreikh (Sudan), Bidvest ya Afrika Kusini zote zimecheza pale, hoja inayoshikiliwa na Azam katika kusaka haki yao.

Hata hivyo, chanzo cha ndani kinasema kuwa Azam ambao mchezo wao na African Lyon, wikiendi iliyopita ulikuwa na figisufigisu nyingi, inahofia kasi ya Simba ambayo ilionyesha kiwango kizuri kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Ndanda.

Simba ambao waliifunga Ndanda mabao 3-1, imekuwa ikiogopeka baada ya kufanya vizuri kwenye mechi zao za kirafiki wakati wa maandalizi yao kwa kucheza mechi sita na kushinda nne, sare moja na ilipoteza moja.

“Simba hii ni tishio, hiyo yote ni hofu tu, wanajua kuwa tuna usajili mzuri hivyo wanawahofia kina Laudit Mavugo, Shiza Kichuya na wengine ambao wamekuwa wakitoa maangamizi.
“Tunajua kuwa wanataka kuleta mbinu za kupata ushindi kule kwao, waje hapa Taifa au Uhuru ambapo ni peupe waone moto wetu, Uwanja wa Chamazi ni mdogo mashabiki wetu hawataingia wote.” kilisema chanzo kutoka Simba.

Leave A Reply