The House of Favourite Newspapers

The world you left behind- 40

0

Na Eric Shigongo

Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa na kufanya roho yake iwindwe kwa udi na uvumba.
Wanaomuwinda ni viongozi wenzake na wafanyabiashara waliokuwa wakimuona kama kikwazo kutokana na tabia yake ya kukemea ufisadi.
Mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake unaandaliwa na kwa bahati nzuri, Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha, anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kunusuru maisha yake.
Hatimaye siku ya tukio inawadia na kwa utaalamu wa hali ya juu, Grace anamuokoa Magesa huku watu wengine wote wakiamini kwamba waziri huyo amekufa kwenye ajali hiyo. Wawili hao wanatorokea mafichoni Mombasa, Kenya ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.
Grace anasafiri kuelekea Israel kikazi na Magesa anaitumia nafasi hiyo kumpekua mwanamke huyo akitaka kuujua ukweli wa maisha yake. Anachokutana nacho kinamshangaza sana. Hatimaye Grace anarejea na Magesa anambana kwa maswali magumu, hali inayosababisha mwanamke huyo apasue jipu na kueleza ukweli.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Ivan, mtoto mkubwa wa ‘marehemu’ Magesa, hakuacha kwenda kituo kikuu cha polisi kufuatilia mwenendo wa uchunguzi wa mauaji ya baba yake. Hata hivyo, kama ilivyokuwa mwanzo, kila alipokuwa akienda kuulizia, majibu yalikuwa ni yaleyale; ‘bado uchunguzi unaendelea.’
Hakuishia hapo, akawa pia anaenda ofisini kwa baba yake mara kwa mara kutaka kujua kama kuna taarifa zozote mpya zimepatikana kuhusu wahusika wa kifo cha baba yake. Alitamani sana kuona wahusika wanakamatwa, wanapelekwa mbele ya sheria na hatimaye wanahukumiwa kulingana na makosa waliyoyafanya lakini hilo lilionekana kuwa gumu.
Hata hivyo, alijiapiza ndani ya moyo wake kwamba ataendelea kufuatilia, hata kama itachukua muda mrefu kiasi gani lakini ni lazima wahusika wa kifo cha baba yake wapatikane na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.
Kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele ndivyo tabia ya mama yake mzazi, Vivian ilivyokuwa inazidi kubadilika. Akawa siyo Vivian yule ambaye kila mtu alikuwa akimheshimu kabla mumewe hajafikwa na mauti. Alibadilika mno, akawa ni mtu wa starehe kila siku, hakujali tena kuhusu wanaye, akawa ni mtu wa kujirusha siku zote saba katika wiki. Katika utafiti wake, Ivan aligundua kwamba katika siku zote ambazo mama yake alikuwa akichelewa kurudi nyumbani, kuna gari ambalo lilikuwa likimleta mpaka nyumbani. Mara kwa mara alikuwa akijaribu kutazama ni nani aliyekuwa akiendesha gari hilo lakini alikuwa akishindwa kumuona kutokana na ukweli kwamba lilikuwa na vioo vya giza (tinted).
“Lakini mbona lina namba za serikali?” alijiuliza Ivan usiku mmoja akiwa amekaa kwenye dirisha la chumba chake, ikiwa tayari ni saa saba za usiku. Mama yake aliteremka kwenye gari akiwa anapepesuka, akionesha kuzidiwa na kilevi.
Alichokifanya Ivan ilikuwa ni kuchukua kalamu na karatasi, wakati dereva wa gari hilo la serikali, Toyota Land Cruiser V8 akihangaika kuligeuza, yeye alikuwa makini kuzitazama namba za usajili za gari hilo, akaziandika kisha harakaharaka akafunika pazia akiogopa mama yake asije akamuona.
Muda mfupi baadaye, mlango mkubwa ulikuwa ukigongwa, kama kawaida yake akatoka na kwenda kumfungulia mama yake aliyekuwa amelewa chakari.
* * *
Miezi mitatu tangu kifo cha Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Daniel Mwampashi, ripoti ya uchunguzi wa kina juu ya kifo chake ilikuwa tayari imeshakamilika.
Kazi nzuri iliyofanywa na timu ya wapelelezi kutoka jeshi la polisi, vitengo maalum vya Forensic Investigation na Crime Scene Investigation (CSI) kwa kushirikiana na maafisa usalama, iliwezesha kupatikana kwa taarifa nyingi kuhusu tukio hilo ambazo zilikuwa zinachanganya sana.
Kama ilivyo utaratibu wa kushughulikia kesi nzito kama hizo, baada ya timu hiyo kukamilisha uchunguzi wake, ripoti ilikabidhiwa sehemu husika ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Usalama wa Taifa, Ephraim Mandiba, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, Pius Kasekwa na Mkuu wa Upelelezi, Inspekta Jordan Ngai walikutana haraka kwa kikao cha dharura na kuanza kuijadili ripoti hiyo.
“Kuna harufu ya mchezo mchafu hapa, ripoti inasema maganda ya risasi yaliyookotwa nyumbani kwa marehemu sambamba na risasi zilizotolewa kwenye mwili wa marehemu, zina namba zinazoonesha kwamba bunduki zilizotumika ni mali ya serikali.”
“Unataka kusema silaha za jeshi la polisi ndizo zilizotumika?”
“Siyo mimi ninayesema, ripoti ndiyo inayoeleza hivyo na ni mapema kusema kwamba silaha zilizotumika ni za jeshi la polisi kwa sababu si polisi pekee wanaotumia bunduki za serikali.
“Si hivyo tu, ripoti inazidi kueleza pia kwamba wauaji hawakuchukua chochote zaidi ya ‘laptop’ ya marehemu pamoja na nyaraka zake za siri. Pia inaonekana kwamba usiku ambao mauaji yalitokea, ndiyo usiku huohuo ambao ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliteketea kwa moto,” alisema Kasekwa wakati akisoma ripoti hiyo.
Akaendelea kuichambua ripoti hiyo ambapo uchunguzi ulionesha kwamba ofisi hiyo haikuungua kutokana na shoti ya umeme kama taarifa za awali zilivyoonesha bali ilichomwa moto kwa makusudi na watu wasiofahamika.
Ripoti iliendelea kueleza kwamba kabla ya watu hao kufanya tukio hilo, walivunja milango ya ofisi, wakaingia mpaka kwenye chumba maalum kunakohifadhiwa mafaili yenye nyaraka nyeti za serikali, ikiwemo ripoti ya ukaguzi wa hesabu za serikali.
Huko walichukua mafaili kadhaa kisha wakanyofoa vifaa maalum vya kutunza kumbukumbu kwenye kompyuta kadhaa ndani ya ofisi hiyo viitwavyo ‘hard disc’, wakamwaga petroli nyingi jengo zima kisha wakaliwasha moto na kutokomea kusikojulikana.
Majadiliano yaliendelea wakati viongozi hao wakubwa katika sekta ya usalama wakiichambua ripoti hiyo ambapo maazimio kadhaa yalifikiwa. Jambo la kwanza, ilionesha kwamba kifo cha Mwampashi kilikuwa na uhusiano mkubwa na kazi yake kwa sababu wauaji walishambulia sehemu mbili, nyumbani kwa marehemu na ofisini kwake.
Pia ilibainika kwamba wakati tukio hilo linatokea, zilikuwa zimesalia saa chache kabla ya kusomwa kwa ripoti ya ukaguzi wa hesabu za serikali na kwamba wauaji hao walipovamia nyumbani kwa marehemu, walichukua laptop yake iliyokuwa na ripoti hiyo sambamba na nyaraka kadhaa za ukaguzi.
“Inaonesha waliofanya tukio hilo ni wataalamu sana katika kazi hiyo, hawakuwa majambazi wa kawaida bali watu waliotumwa kufanya kazi maalum kwa maslahi ya watu fulani.”
“Ni kweli kabisa, na jambo la kwanza ambalo inatakiwa kulivalia njuga, ni kuhakikisha ripoti hiyo inapatikana, tunaipitia kwa kina na kuona ni mambo gani yalikuwa yameandikwa ndani yake.”
“Lakini tutawezaje kuipata wakati laptop imeibwa na ‘hard disc’ zote zilikuwa zimenyofolewa?”
“Inawezekana kabisa, inabidi tuwasiliane na kitengo chetu cha teknolojia ya mawasiliano (IT) kujaribu kuitafuta laptop iliyoibiwa ipo sehemu gani. Kwa kuwa vifaa vyote vya serikali vinaunganishwa na GPS ni rahisi sana kuipata, pia inatakiwa kwenda kwenye tume ya mawasiliano kuangalia marehemu alikuwa akiwasiliana na nani siku za mwisho za uhai wake,” alisema Mandiba.
Wakagawana majukumu ambapo bila kupoteza muda, walitawanyika na kazi ikaanza mara moja. Mazingira ya matukio yote yaliashiria kwamba kuna jambo kubwa lilikuwa linafichwa nyuma ya pazia, kila mmoja akaweka nadhiri ndani ya moyo wake kuhakikisha wanaupata ukweli.
Je, nini kitafuatia? Usikose kufuatilia siku ya Ijumaa kwenye Gazeti la Uwazi Mizengwe ya Uchaguzi.

Leave A Reply