The House of Favourite Newspapers

Unending Love-82

5

Penzi zito linachanua kati ya vijana wawili wadogo, Jafet na Anna. Kutokana na Jafet alivyokuwa akimpenda msichana huyo, anaamua kukataa kusomea upadri kwa lengo la kutaka kuja kuoana na Anna, binti kutoka familia ya kitajiri.

Siku zinazidi kusonga mbele, Anna na Jafet wanazidi kukua na kupendana, wanaahidiana mambo mengi mazuri. Kwa bahati mbaya, Anna anapatwa na matatizo ya figo zake moja kushindwa kufanya kazi.

Jafet anaamua kujitolea figo yake moja na kumpa Anna. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa msichana huyo, wazazi wa Anna wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi.

Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani. Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William ambaye baadaye anampa ujauzito na kumkataa.

Anna anarejea nyumbani kwao, Mwanza ambako wazazi wake wanamtoa ujauzito kihalali na huo unakuwa mwanzo wa kulipuka upya ugonjwa wake wa figo. Anasafirishwa tena mpaka nchini India.

Jafet anafuatwa na baba yake Anna na kupelekwa India kutokana na shinikizo la msichana huyo. Jafet anapowasili India, japokuwa Anna alikuwa na hali mbaya, hali yake inaanza kuimarika kwa kasi na kumshangaza kila mmoja. Ndani ya muda mfupi tu, anapata ahueni kubwa ambapo baadaye anaruhusiwa kutoka hospitalini hapo.

Wanafunga safari ya kurejea Tanzania na hatimaye wanawasili jijini Mwanza ambapo mjadala mkubwa unaendelea kuhusu hatima ya wawili hao wanaoonesha kupendana kwa dhati. Wazazi wa Anna wanafikia muafaka wa kuwatafutia wote wawili chuo kingine nchini Marekani, wazo ambalo Jafet alilikubali na sasa wanafunga safari kuelekea kijijini kwa wazazi wa Jafet.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Siku hiyo ilipita vizuri, kama walivyokubaliana, kesho yake waliianza safari ya kuelekea kijijini Rwamgasa, nyumbani kwa wazazi wa Jafet. Kama kawaida, baba yake Jafet ndiye aliyekuwa akiendesha huku mkewe akiwa pembeni yake.

Siti za nyuma walikaa Anna na Jafet ambao muda mwingi walikuwa wakipiga stori za hapa na pale, huku mizigo mingi ikiwa imehifadhiwa kwenye buti kama zawadi kwa wazazi wa Jafet.

Safari iliendelea, baba yake Anna na mkewe wakawa wanaendelea na mazungumzo yao huku Anna na Jafet nao wakiendelea na mambo yao, mara wakumbatiane, mara wasikilize muziki kwenye simu ya Anna kwa kutumia ‘headphones’, kila mmoja akiwa amechomeka sikio moja, mara wasimuliane hadithi za zamani, ilimradi tu muda wote walikuwa na furaha.

Baada ya kusafiri kwa saa nyingi, wakati mwingine wakilazimika kupita kwenye barabara mbovu kabisa, hatimaye waliwasili kijijini Rwamgasa, kama ilivyokuwa kawaida, wanakijiji wakakusanyika kwa wingi, watu wazima kwa watoto wakilishangaa gari wakati likikatiza mitaa kuelekea nyumbani kwa akina Jafet.
“Mbona machozi yanakutoka Jafet!” Anna aliuliza baada ya kumuona Jafet akiwa katika hali isiyo ya kawaida.

“Nakumbuka mengi sana nikiwa nyumbani, nakupenda sana Anna ‘please’ nakuomba usiniumize tena,” alisema Jafet kwa sauti ya chini, kauli iliyouchoma sana moyo wa Anna. Akamkumbatia na kutoa kitambaa kwenye pochi yake, akaanza kumfuta machozi huku akimbusu sehemu mbalimbali za mwili wake.

“Nakuahidi Jafet, nimejifunza kutokana na makosa na nakuahidi nitakupenda, kukuheshimu na kukujali mpaka kifo kitakapokuja kututenganisha,” alisema Anna kwa sauti ya chini huku akiendelea kumfuta machozi Jafet.

Tayari walishawasili nyumbani kwa akina Jafet, ikabidi mwenyeji ndiyo awe wa kwanza kuteremka kwenye gari na kuwaongoza wageni. Kwa bahati nzuri, mama yake Jafet tayari alikuwa amesharejea kutoka kwenye shughuli zake za kulima vibarua kwenye mashamba ya watu ili apate chochote cha kuilisha familia yake.

“Jafet! Ni wewe mwanangu? Mmerudi salama? Ooh ahsante Mungu,” alisema mama yake Jafet kwa sauti ya juu, akamkimbilia mwanaye na kumkumbatia kwa nguvu huku machozi ya furaha yakimtoka.
Muda mfupi baadaye, baba yake Anna na mkewe nao waliteremka kwenye gari wakiwa na binti yao, wakapokelewa kwa uchangamfu na mama yake Jafet pamoja na wadogo zake, wakaingia mpaka sebuleni. Ndani ya muda mfupi tu tangu kuwasili kwa wageni hao, nyumba nzima ilichangamka mno.

Zawadi mbalimbali walizoletewa zikaenda kushushwa kwenye gari na kuzidisha furaha ndani ya nyumba hiyo. Ilibidi baba yake Jafet akaitwe kwenye kilabu cha pombe kilichokuwa jirani. Muda mfupi baadaye akarejea akiwa tayari ameshaanza kulewa. Kitendo cha kumuona mwanaye amerejea salama, kilimfurahisha mno mzee huyo.

“Sasa si mlisema hali ya mgonjwa ni mbaya sana, mbona anaonekana yuko fiti, tena kanenepa mpaka mashavu yamemtoka?” aliongea baba yake Jafet kilevi na kusababisha watu wote waliokuwa ndani ya nyumba hiyo wacheke kwa nguvu.

Ilibidi baba yake Anna aanze kueleza kila kitu kilichotokea nchini India na jinsi Jafet alivyoenda kuwa msaada mkubwa kwa Anna, kiasi cha kuzua gumzo kubwa nchini India.

“Dawa zilishaonesha kuanza kushindwa kufanya kazi, tukawa tunajiandaa kwa ajili ya Anna kufanyiwa upasuaji wa mara ya pili wa kumbadilisha figo. Hali ilikuwa mbaya sana yaani ni Mungu tu. Cha ajabu, nilipokuja kumchukua Jafet na kwenda naye India, alipofika tu hali ya Anna ilianza kubadilika.

“Ndani ya siku chache akaanza kuonesha ahueni kubwa, jambo ambalo hata madaktari walishindwa kulitolea ufafanuzi. Yaani ni zaidi ya miujiza,” alisema baba yake Anna na kuwaacha wazazi wa Jafet wakiwa wamepigwa na butwaa.

Akaendelea kueleza yote yaliyotokea mpaka muda huo, akawashukuru sana kwa kumruhusu kuondoka na Jafet na mwisho akawaeleza walichokuwa wameamua kuhusu kuwapeleka wote wawili kwenda kusoma nchini Marekani.

“Lakini sisi hatuna uwezo wa kwenda kumsomesha Jafet Marekani, kwa nini asisome hapahapa anapolipiwa na serikali?” alisema mama yake Jafet lakini baba yake Anna akawatoa wasiwasi kwamba wao ndiyo watakaogharamia kila kitu.

“Sisi hatuna hiyana kabisa, labda mumsikilize na yeye mwenyewe anasemaje,” alisema baba yake Jafet huku mkewe naye akitingisha kichwa kuonesha kuunga mkono kilichokuwa kinazungumzwa. Jafet alipoulizwa mbele ya wazazi wake, alikubali huku akionesha kuwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake.

Kama ishara ya shukrani kwa Mungu wao na kwa wazazi wa Jafet, wazazi wa Anna waliomba washinde pamoja kutwa nzima na kulala hapohapo mpaka siku ya pili ndiyo waianze safari ya kurejea jijini Mwanza, jambo lililopokelewa kwa mikono miwili na wenyeji wao.

Tafrija ndogo ikaanza kuandaliwa ambapo mbuzi mzima alienda kununuliwa haraka pamoja na kuku wengi, wakachinjwa na shughuli za mapishi zikaanza, huku majirani wakialikwa kujumuika na familia hiyo. Kwa kuwa fedha hazikuwa tatizo kwa baba yake Anna, vinywaji vingi vilienda kununuliwa, kuanzia soda, maji mpaka bia.

Watu wakaanza kuburudika wakati wakiendelea kusubiri chakula, wanakijiji wengi wakajumuika nyumbani kwa akina Jafet. Shughuli ziliendelea kupamba moto, watu wakala, kunywa na kusaza huku kila mmoja akishangaa iweje familia hiyo ambayo ilikuwa ikisifika kwa umaskini kijijini hapo, iandae sherehe nzuri namna hiyo. Shamrashamra ziliendelea mpaka usiku, wale wanywaji wa pombe kila mmoja akawa amelewa chakari baada ya kunogewa na pombe za bure.

Wanaopenda kula nao wakala mpaka kusaza, wengine wakabeba kwa ajili ya familia zao. Ilikuwa ni siku ya furaha sana kijijini hapo. Muda wote Jafet na Anna walikuwa wamegandana kama ruba, kila alipokuwepo kijana huyo, Anna alikuwa pembeni yake. Hatimaye siku hiyo ilipita, kesho yake asubuhi maandalizi ya kurejea jijini Mwanza yakaanza kufanyika.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

5 Comments
  1. zenoo de says

    japhet ameniudhi kwa nn hana msimamo mmja huyu kijna kwa amkubalie anna tena ?ila ukiwa maskin bwana

  2. Deborah says

    Nzur iyo

  3. ALLY MASUBI says

    Inavyoonesha Hadithi Inaendea Mwisho Labda Suleikha Ageuke Adui

  4. alex rodrick says

    so amazing…….

  5. Bullah says

    mhhhhh suleikha asije tu akawa mjamzito ……muvi itaanzia hapoo

Leave A Reply