The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-40

1

ILIPOISHIA WIKIENDA
Kabla sijajibu kitu mke wangu akakata simu.
Asubuhi yake ilikuwa ni Jumapili. Nikaona lile suala ni lazima nilipeleke kwa mchungaji vinginevyo nitaumbuka.

Siku ile nilikwenda kwenye ibada ingawa siku nyingine nilikuwa sionekani. Baada ya ibada ya asubuhi nikamueleza mchungaji kuwa nilikuwa na mazungumzo naye lakini nilitaka mazungumzo hayo yafanyike nyumbani kwangu. SASA ENDELEA…

Sasa nimemaliza kumnukuu mheshimiwa waziri, simulizi inarudi mikononi mwangu mimi mchungaji.
Baada ya mheshimiwa waziri kunieleza hayo aliniomba nimsaidie aweze kuwaepuka wachawi hao waliokuwa wanataka kumchukua mtoto wake na pia nimrudishie ndoa yake kwa vile alikuwa tayari ameshafarakana na mke wake.

Kwa kweli nilimsikitikia sana lakini nilimsifu kwa ujasiri aliokuwa nao kunieleza ukweli wake bila kunificha kitu japokuwa alikuwa na heshima ya uwaziri.
Kama ni kuungama, waziri huyo alikuwa ametimiza vigezo vya kuungama, si tu kwa kukiri makosa yake bali pia kwa kuonesha kujuta.

Waumini wangu wengi wameshanieleza matatizo yao na waliofanya makosa walinieleza makosa yao kwa lengo la kuungama na kuomba toba, lakini mkasa wa waziri huyu ulikuwa wa kutatanisha sana.
Wakati wote nilipokuwa nikimsikiliza niliona kama ninayetazama sinema ya kutisha akilini mwangu. Jinsi alivyoonekana kuwa mpole ilikuwa vigumu kuamini kuwa ni yeye aliyekutwa na mambo hayo. Lakini nilijifunza kwamba upole wa nje si upole wa ndani.

Sasa niliweza kugundua ni kwa nini waziri huyo alikuwa haonekani kanisani mara kwa mara. Tatizo ni kwamba alikuwa akichezewa na shetani. Na pia niligundua ni kwa nini katika siku za hivi karibuni waziri huyo alionekana kukonda, kumbe ni kwa sababu ya mkasa aliokuwa akikumbana nao.
“Pole sana,” Ndiyo neno langu la kwanza nililoanza kumwambia.

“Asante baba mchungaji.”
“Nimeusikiliza mkasa wako kwa makini na kwa kweli nimeona kuwa unahitaji msaada tena msaada wa haraka.”
“Ni kweli.”

“Kwanza ninakusifu kwa ujasiri wako wa kuniita na kunieleza yote hayo bila kunificha kitu. Ni dalili kuwa umeanza kujutia makosa yako ili uweze kupata toba ya kweli…sasa nisikilize.”
“Ndiyo baba.”

“Matatizo yako yote yanatokana na shetani. Shetani aliyeanzia kwa babu yako ndiye aliyetaka kuichafua familia yenu yote akiwaweka nyinyi kama mawakala wake wa kuendesha shughuli za uchawi. Lakini siku zote shetani hana uwezo wa kushindana na Mungu. Na mimi nitakuombea kwa jina la Yesu Kristo ili uweze kumrejea Mungu wako leo.”

Nilipokuwa namwambia hivyo nilimuona mheshimiwa waziri akiinamisha kichwa chake. Nikahisi alikuwa amejiweka tayari kumpokea Yesu Kristo ndani yake.
“Kitu cha kwanza nataka uende ukaniletee ule mkoba wako wa uchawi ambao umekuwa ndiyo chaka la shetani,” nikamwambia kwa sauti ya kiuchungaji.

Waziri aliinuka na kwenda kunako kabati akalifungua na kuutoa mkoba huo.
“Nilikuja nao kwa kujua kuwa utauhitaji,” akaniambia akiwa ameushika mkoba huo mkononi.
“Hebu ufungue, umwage vilivyomo hapa chini,” nikamwambia.

Waziri aliufungua mkoba huo akaukung’uta. Vitu mbalimbali vya kichawi vilichomoka na kuanguka chini. Nikauona na ule mkono wa mtoto mchanga uliokuwa umekaushwa.
Nikasimama na kufanya maombi yangu kisha nikakemea uovu ule uliomwagwa chini na kuomba nguvu za Yesu kuteketeza kila kitu cha uchawi alichokuwa anamiliki waziri huyo pamoja na vile alivyovimwaga pale chini.

Nilitumia muda mrefu kumuombea yeye mwenyewe mpaka akaniambia kuwa anahisi kupata nguvu na matumaini mapya.
“Sasa toa hivi vitu uani uviteketeze kwa moto,” nikamwambia.
Mheshimiwa waziri badala ya kuvishika vitu hivyo kwa mkono alikwenda kuvaa soksi mikononi kisha akavikusanya vitu hivyo kwenye gazeti. Niliamini kuwa sasa alikuwa akiviona vitu vyake hivyo ni kama najisi.

Baada ya kuvikusanya kwenye gazeti alikwenda kuvimwaga uani akavinyunyizia mafuta ya petroli kisha akaviwasha.

Mkoba huo wa kichawi uliteketea kabisa.
Tuliporudi ndani nikamwambia ampigie simu mke wake amuite.
Waziri alisita kidogo lakini baadaye alitoa simu yake akampigia mke wake. Wakati simu yake inaita alinipa.
“Naomba uzungumze naye wewe, mimi hawezi kunielewa.”

1 Comment
  1. saidyndunge says

    sijui itakuwaje mkewe akishafika apo

Leave A Reply