The House of Favourite Newspapers

Yanga waenda Mauritius kitajiri

0

YANGA (1)Timu ya Yanga wakifanya mazoezi.

Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam
KIKOSI cha Yanga kimeondoka alfajiri ya leo Ijumaa kuelekea nchini Mauritius, ambako kinatarajiwa kukipiga dhidi ya Cercle de Joachim kwenye mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wachezaji wa timu hiyo wameondoka wakiwa na morali hiyo baada ya kukodiwa ndege pamoja na kulipwa mishahara yao na posho nyingine ambazo jumla zinaaminika kufikia shilingi milioni 200.
Taarifa ambazo zimefika mezani kwa Championi Ijumaa ni kuwa, ‘mzigo’ huo umewaongezea motisha kubwa na hivyo baada ya kutua Mauritius majira ya saa tano asubuhi ya leo, watapumzika kisha jioni watakwenda uwanjani kupasha misuli.

Yanga-training.jpg
Mbali na kutumia fedha hizo katika maandalizi ya mchezo huo, lakini pia utakuwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi dhidi ya Simba katika Ligi Kuu Bara, Februari 20, 2016 kwenye Uwanja wa Taifa.
“Leo (jana) wachezaji wamepewa mshahara, posho na marupurupu mengine waliyokuwa wanatakiwa kupewa, hiyo yote ni katika kuwapa morali katika mechi hiyo dhidi ya Cercle de Joachim na ile ya Simba,” kilisema chanzo kutoka ndani ya Yanga.

 
Aidha, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Jerry Muro, ameliambia gazeti hili kuwa, safari hiyo ilitarajiwa kuanza leo saa 11:00 alfajiri kwa ndege ya kukodi ya Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL).
Aliongeza kuwa ndege hiyo itawasubiri nchini humo na baada ya mchezo huo, moja kwa moja watapanda pipa na kuelekea Pemba kujiandaa na mechi dhidi ya Simba. Ndege watakayokwenda nayo itawasubiri.
Akizungumzia mchezo huo wa kesho Jumamosi, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, alisema:
“Mipango yangu ni kuwa kila mechi ni kushinda tu, sijali kama ni ya ligi au ya kimataifa, wachezaji nimewaandaa kwa kupambana vizuri, jambo la msingi ni kucheza kwa nidhamu ya juu.”
Kuhusu kiungo wa timu hiyo, Thabani Kamusoko ambaye alikuwa majeruhi, alianza mazoezi juzi katika Uwanja wa Polisi lakini Daktari wa Yanga, Nassor Matuzya, alisema ataongozana na timu lakini kuhusu kutumika au kutotumika hilo litakuwa ni jukumu la kocha. “Kama ni kucheza atavaa kifaa maalum cha kusaidia kumzuia kutopata maumivu ya kifundo cha mguu,” alisema Matuzya.

Leave A Reply