The House of Favourite Newspapers

Yanga Washusha Kiungo Kiboko ya Mkude

0

MABOSI wa Yanga wamekiangalia kikosi chao kilichocheza michezo nane ya Ligi Kuu Bara, fasta wakakubaliana kushusha kiungo fundi mchezeshaji mwenye uwezo wa kuchezesha timu na kutengeneza mabao zaidi ya viungo wa Simba, Jonas Mkude na Mzamiru Yassin.

 

Safu ya kiungo ya Yanga hivi sasa inaongozwa na nahodha mkongwe Mkongomani Papy Tshishimbi, Mapinduzi Balama, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Abdulaziz Makame ‘Bui’ na Issa Mohamed ‘Banka’.

 

Yanga imepanga kukifanyia maboresho kikosi chake kwenye usajili wa dirisha dogo baada ya wale waliowasajili kwenye usajili mkubwa kushindwa kuonyesha viwango vyao huku kati yao wakipangwa kusitishiwa mikataba yao.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, Yanga wanataka kumsajili kiungo huyo mchezeshaji kutokana na nusu ya viungo waliopo kuwa ni wakabaji tofauti na Balama ambaye ndiye tegemeo hivi sasa katika timu.

 

Mtoa taarifa huyo alisema katika michezo yao waliyoicheza, timu imeshindwa kucheza kutokana na viungo wengi waliopo ni wakabaji akiwemo Tshishimbi ambaye ametumika katika michezo kadhaa kucheza namba 10 kabla ya kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Charles Mkwasa kumhamishia namba 6.

 

“Tshishimbi alikuwa analazimishwa kuchezeshwa namba 10 katika michezo ya ligi ni kutokana na kutokuwepo kiungo mchezeshaji mwenye uwezo wa kuchezesha timu, pia kutengeneza nafasi za kufunga mabao.

 

“Kiungo huyo alikuwa akichezeshwa kimakosa, Tshishimbi kiuhalisia ni kiungo mkabaji na siyo mchezeshaji na mkabaji, hivyo uongozi kwa kushirikiana na benchi la ufundi wamekubaliana kusajili kiungo mwingine mmoja mchezeshaji.

 

“Hivyo, uongozi umemuachia Mkwasa suala hilo la kupendekeza kiungo mchezeshaji anayemuhitaji yeye na kikubwa katika kuisuka Yanga itakayokuwa imara,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mwasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli kuzungumzia hilo alisema: “Kamati ya Ufundi na Mashindano pamoja na kocha Mkwasa bado hawajakutana, hivyo ni ngumu kuliweka wazi hilo, tusubirie muda ukifika tutaweka wazi.”

Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

 

Leave A Reply