The House of Favourite Newspapers

Kigogo Afanya Tukio La Kutisha Dar! Adaiwa Kumfungia Mke Wake Ndani Kwa Miaka 5

 kigogo-1-copy   Karani wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Grace Mwakabuta anayedaiwa kufungiwa miaka mitano mmoja ndani na mume wake Gideon  Mwakabuta.

Imeandikwa; Hamida Hassan na  Imelda Mtema Gazeti la Amani, Januari 5-11 | 2016 Toleo Na 946

DAR ES SALAAM: Mwalimu mstaafu wa chuo kikuu kimoja, Gideon  Mwakabuta (60), amebeba shutuma nzito kufuatia madai kwamba, kwa muda wa miaka mitano amemfungia ndani mkewe wa ndoa, Grace Mwakabuta ambaye pia ni karani wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni jijini hapa.

amani_front

Mzee Mwakabuta na mkewe huyo ni wakazi wa Wazo Hill jijini hapa.Kisa cha kumfungia kinatajwa ni afya ya karani huyo kuwa mbaya akikabiliwa na ugonjwa wa ajabu ambao ulimsababishia kupooza mikono na mwili kutokuwa na nguvu hivyo kushindwa kutembea, kuongea na kushiriki shughuli zozote za ujenzi wa taifa achilia mbali za kifamilia kama mke.

kigogo-3-copy

Grace Mwakabuta akipelekwa hospitali.

MAJIRANI WAMFUNGIA KAZI

Tukio hilo la kushangaza lilibumburuka hivi karibuni baada ya baadhi ya majirani kumfungia kazi mstaafu huyo kwa nia ya kufichua uovu huo ambao kibinadamu hawakuuona kama ni sawasawa.

Jirani mmoja (jina linahifadhiwa) ana mkasa mzima wa jinsi mwanamke huyo alivyoanza kuumwa na mumewe kudaiwa kumfungia ndani:

“Unajua ni muda mrefu takriban miaka kumi huyu mama alianza kuumwa ambapo ndugu mbalimbali walifika nyumbani kwake na kumuomba mumewe wampeleke hospitali baada ya kuona anaumwa na kulala ndani tu pasipo kupelekwa hospitali.

“Haikujulikana alikuwa akiumwa nini lakini Mwakabuta pia haikujulikana alikuwa akiwajibu nini hao ndugu maana sisi tukawa tunaendelea kumwona mkewe akiwa ndani tu.”

kigogo-4-copy

Baadhi ya majirani wakimsadia Grace.

MADAI YA MUME KWA MAJIRANI

Aidha, jirani huyo alisema kuwa, mwanaume huyo alidai kwamba, anamtibia mwenyewe mke wake lakini ndugu walifika tena kwa ajili ya kumpelekea dawa za kienyeji wakiamini huenda zingemsaidia lakini hazikupokelewa kwa madai kwamba, yeye ndiye anampatia dawa.

“Kwa kweli sisi kama majirani tumekuwa tukiumia sana kwa hii hali ya mwanamke wa jirani. Ilifika mahali tukasema huenda siku moja mumewe ataamua kumpeleka hospitali, lakini tukaona siku zinapita,” aliongeza jirani huyo.

MKE AANZA KULIA, KUPIGA KELELE

Habari zaidi zenye kuibua majonzi zinasema kuwa, baada ya Grace kuendelea kuteseka kwa ugonjwa huo ambao ulikuwa haujulikani ni upi, alianza kupiga kelele akilia kwa uchungu wa maumivu.

“Mbaya zaidi ni kwamba, ugonjwa wake anakakamaa misuli na hawezi kufanya lolote zaidi ya kulala tu, amekuwa kama mtu asiye na wasaidizi. Ukimwona huwezi kuamini kwamba ni mgonjwa anayepata msaada wa kitabibu au wa kibinadamu.

“Grace alianza kuumwa tangu wazazi wake wakiwa hai, nao  walijaribu kumpigania afya yake lakini ikashindikana mpaka wote sasa wamefariki dunia, Grace bado anaumwa tu,” alisema jirani mwingine.

whatsapp-image-2017-01-02-at-7-35-10-am-1

WAANDIKA BARUA USTAWI WA JAMII

Majirani hao waliendelea kusema kuwa, baada ya kuona hali ya Grace inazidi kuwa mbaya kila kukicha kwani walikuwa wanapata nafasi ya kumjulia hali, waliamua kuandika barua ya siri na kuipeleka Idara ya Ustawi wa Jamii ambako wanashughulika na matatizo ya kifamilia.

“Ustawi wa Jamii na wao waliamua kuandaa mpango wa kuvamia nyumbani kwa Mwakabuta na kumchukua mkewe kwa nguvu kumpeleka hospitali kupata matibabu,” alisema jirani huyo.

SIKU YA TUKIO

Siku ya tukio la Ustawi wa Jamii kuvamia nyumbani kwa Mwakabuta ilikuwa Jumamosi iliyopita ambapo walimkuta mzee mwenyewe akiwa amejifunga kanga, baada ya utambulisho na kumuuliza alikiri mkewe yupo ndani anaumwa lakini akasema amekuwa akimpeleka hospitali na kwenye tiba nyingine bila mafanikio.

“Ilikuwa kazi ngumu kumchukua mkewe kumpeleka kwenye gari maana Mwakabuta alikuwa hataki. Na hata wakati wa kumtoa mkewe chumbani ili aandaliwe, alikataa kusaidiwa akisema kazi hiyo ataifanya mwenyewe kwa sababu ni mkewe mpendwa anayempenda sana.

Hata hivyo, kazi ikafanyika, mke akaingia kwenye gari na mumewe akiwemo na kupelekwa Hospitali ya Mwananyamala.

“Mimi nahisi pana tatizo kwani si rahisi kwa mke unayempenda ukamwacha aumwe vile ndani siku zote. Na hata madai yake Mwakabuta kwamba amekuwa akimtibia mkewe yanatia shaka kwani hali ya mkewe si ya mtu anayefanyiwa uangalizi kwa ugonjwa,” aliongeza jirani huyo.

MUME MIKONONI MWA POLISI

Habari zaidi ni kwamba, baada ya kuvamia nyumbani kwa mzee huyo na mkewe kuchukuliwa akiwa hoi, mbele ya safari, Mwakabuta aliishia mikononi mwa Polisi wa Kituo cha Kawe ambako alikuwa anashikiliwa hadi wakati gazeti hili linakwenda mitamboni.

MKE ANAENDELEA NA MATIBABU

Juzi, Amani lilifika Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kumjulia hali mwanamke huyo na ikibidi kupata picha akiwa amelazwa hapo, lakini halikuweza kumwona na kuambiwa anaendelea vizuri na matibabu na hatakiwi kusumbuliwa.

NENO LA MHARIRI

Ushauri ni kwamba pamoja na mume kukamatwa lakini bado na yeye anahitajika kuchunguzwa huenda hata yeye hayuko sawa kutoka na mawazo au jambo lingine lolote ambalo hajawahi kulisema kwa jamii.

Tukio hili ni la kushangaza sana na la kufungulia mwaka lililowaacha watu na maswali mengi. Je, Grace hakuwa na watoto? Je, ni kwa sababu gani  mumewe alimfungia? Ili kupata majibu ya maswali hayo, endelea kufuatilia magazeti ya Global.

Ili kupata tamko la serikali, jana Amani lilimpigia simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Suzan Kaganda ili kumsikia anasemaje kuhusu madai hayo ambapo alithibitisha kushikiliwa kwa Mwakabuta kwenye Kituo cha Polisi cha Kawe.

“Ni kweli, tukio hilo la Mwakabuta kukamatwa lipo kwetu, tunamshikilia. Alikamatwa Jumamosi. Lakini mkewe alipelekwa Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu.

“Sisi bado tunamshikilia Mwakabuta kwani upelelezi unaendelea ili kubaini usahihi wa madai dhidi yake. Kwa mujibu wa ndugu na baadhi ya majirani, Grace aliumwa, akawa anatibiwa lakini baadaye mumewe akaacha kumtibia na kumfungia ndani tu. Hayo ndiyo madai yaliyopo.

“Upelelezi ukikamilika ikaonekana ni kweli alifanya tendo lile, hatua itakayofuata ni kumpeleka mahakamani,” alisema Kamanda Kaganda.

Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa maelezo ya kituoni, Mwakabuta anafanya shughuli zake binafsi na mkewe Grace alikuwa mwajiriwa mpaka anakumbwa na ugonjwa.

“Kwa maelezo ya kituoni, Mwakabuta kwa sasa anafanya shughuli zake. Sasa kama ni mstaafu mimi sijajua. Mkewe alikuwa mwajiriwa lakini kutokana na matatizo ya maradhi nadhani isingewezekana kuendelea kufanya kazi. Sasa sijajua kama ajira ilikoma au vipi,” alimaliza kamanda huyo.

MKE ANAENDELEA NA MATIBABU

Aidha, jana Amani lilifika tena hospitalini hapo na kuzungumza na ndugu mmoja ambaye alifika kumwona Grace, alisema anaendelea na matibabu ambapo madaktari wanachofanya kwa sasa ni kuchukua vipimo mbalimbali ili kubaini hasa tatizo lake.

“Mimi mwenyewe nimekuja kumwangalia Grace, lakini nimetoka kwa kuwa madaktari wameingia, wanasema wanaendelea kumfanyia vipimo mbalimbali ili kubaini tatizo lake la msingi ni nini,” alisema ndugu huyo bila kuwa tayari kutaja jina lake.

Akielezea maisha enzi za afya yake, ndugu huyo alisema kuwa, Grace alikuwa na afya njema tu na alikuwa mwanamke mwenye kujali wengine na kushirikiana na watu kama kawaida.

“Sijajua hasa nini kilimpata. Lakini alikuwa kawaida sana. Kuhusu umri, sina kumbukumbu sawasawa ila nadhani anaweza kuwa kwenye miaka 45 mpaka 50. Lakini sina uhakika sana,” alisema ndugu huyo.

Kuhusu kuwepo au kutokuwepo kwa watoto, ndugu huyo alisema hawezi kulisemea zaidi ya mzee Mwakabuta mwenyewe.

Jionee Hapa Polisi Wakabiliana Vikali na Majambazi Mikocheni


halotel-strip-1-1

Comments are closed.