The House of Favourite Newspapers

Msanii Wa Kidedea Afa Kwa Kipigo, Mumewe Ahojiwa Polisi

msanii-wa-kidedea-2 msanii-wa-kidedea-1

Msanii aliyewahi kuwika kwenye Kundi la Sanaa la Kidedea na kupata jina la sanaa la Zamzam, Kijakazi Pazi Shaban akionyesha majeraha enzi za uhai wake.

Na Hamida Hassan na Gladness Mallya, Gazeti la Amani, Januari 5-11 | 2016 Toleo Na 946
DAR ES SALAAM: Msanii aliyewahi kuwika kwenye Kundi la Sanaa la Kidedea na kupata jina la sanaa la Zamzam, Kijakazi Pazi Shaban amefariki dunia mjini Musoma, Mara lakini nyuma ya kifo chake, kipigo kinatajwa kusababisha.

amani_back
Kwa mujibu wa chanzo, mumewe ambaye inasemekana ni polisi aliyejulikana kwa jina la Hamad Ally ndiye aliyeufikisha mwili huo  Temeke jijini Dar  es Salaam ambako ni kwa wazazi wake.
Akizungumza na Amani msibani Temeke juzi, ndugu mmoja wa marehemu, alisema:
“Taarifa zilitufikia kwamba, Zamzam amefariki dunia. Tukaambiwa kwamba, alikuwa akiumwa vidonda vya tumbo. Sasa mumewe alisema anakwenda kumzika mkewe Kilimanjaro. Kwa hiyo kama ni utaratibu ilibidi familia iende Kilimanjaro.

msanii-wa-kidedea-4

Mume wa Zamzam.

“Lakini sasa siku chache nyuma, Zamzam mwenyewe alituma picha kwa baadhi ya marafiki zake na nduguze akionekana ana majeraha kadhaa usoni na mwilini. Akasema amepigwa sana kwa hiyo alituma picha zile ili ushahidi uonekane.
“Sasa kusikia amekufa kwa kuumwa, ikabidi familia itoe tamko kwamba, wanakubali kifo cha mtoto wao lakini hawawezi kwenda msibani mpaka mwili huo upitie kwanza Dar es Salaam ndipo upelekwe Kilimanjaro kwa mazishi.

zamzam

Zamzam enzi za uhai wake.

“Mume akakubali, mwili umeletwa Dar. Lakini ulipofika, ikabidi familia iuchukue mwili mpaka Hospitali ya Temeke. Madaktari wakaupima, wakabaini kwamba, Zamzam alifariki dunia kwa kipigo. Ikabidi watu wamuulize mumewe ambaye anaweza kuwa anajua.
“Hivi ninavyoongea na wewe leo (Jumanne), mumewe anaulizwa nini kilitokea
Kwa kweli hili tukio nalo limetushangaza sana lakini zaidi sana, mama wa marehemu, Asha Omari ameumia sana, analia muda mwingi kwa kushangaa kifo cha Zamzam kwani mara ya mwisho alipoongea naye alikuwa mzima hakumwambia anaumwa wala amepata ajali kama mwili unavyoonekana na majeraha.”
Kwa mujibu wa taarifa za kifamilia, marehemu Zamzam alitarajiwa kuzikwa jana Jumatano kwenye Makaburi ya Temeke.

Jana Jumatano, Amani lilifika tena msibani, Temeke Sokota na kukuta sintofahamu kubwa ambapo ndugu walikuwa wakitaka kujua hatima ya kifo cha msanii huyo. Amani lilipoulizia alipo mume wa marehemu, ndugu walisema yupo Kituo cha Polisi Chang’ombe kwa mahojiano.
Aidha, taarifa zaidi zilisema kuwa, Polisi Temeke walishangaa kusikia marehemu alikufa kwa kipigo na mumewe alitakiwa kuulizwa kama anajua lolote halafu akapewa gari la polisi kutoka Mara kubeba maiti mpaka Dar badala ya kuulizwa kulekule.
“Inasemekana polisi wa Temeke walimuuliza Kamanda wa Polisi Mara ambaye alisema hakujua kama mke huyo wa mtumishi wake alikutwa na majeraha ila alitoa gari kwa sababu aliambiwa mtumishi wake amefiwa na mke,” kilisema chanzo.
Amani jana lilimpigia simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, ACP Ramadhan Ng’anzi ili kumuuliza kuhusu sakata hilo ambapo alisema:
“Mimi sijui yaliyotokea huko Dar. Mimi nilitoa gari kama ambavyo wewe hapo ukifiwa, mwajiri wako anaweza kukupa usafiri. Kama kuna tofauti ya kifo cha mkewe sijui lolote.”
Amani likampigia simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, ACP Giles Muroto ambapo alisema kuwa, hajui lolote kuhusu sakata hilo kwa vile alikuwa kwenye ziara ya kikazi jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
“Mimi sijui lolote, nilikuwa katika ziara hapa Dar na Waziri Mkuu,” alisema kamanda huyo.
Kwa mujibu wa familia, mpaka gazeti hili linaondoka eneo la msiba jana, mwili wa marehemu bado ulikuwa Hospitali  ya Temeke na ulitarajiwa kuzikwa baadaye kwenye Makaburi ya Kijiji cha Kikwete, Kisarawe, Pwani.

Polisi Wakabiliana Vikali na Majambazi Mikocheni

Comments are closed.