Kuachika/ Kuachwa si Mwisho wa Maisha

Na DAYNA NYANGE| GAZETI LA AMANI| SINDANO ZA MASTAA

BILA shaka mpenzi msomaji uko poa kabisa! Nikukaribishe tena kwenye Sindano za Mastaa. Wiki iliyopita mlikuwa na staa wa sinema za vichekesho Bongo, Crispin Masele ‘Chapombe’.

Wiki hii mko naye staa wa Bongo Fleva, Dayna Nyange ambaye anafunguka mambo mengi kuhusu kuachika au kuachwa kuwa siyo mwisho wa maisha. Msomaji na shabiki wangu, inawezekana wewe ni miongoni mwa waathirika wa mapenzi baada ya kuachwa, kuachana na hata kutelekezwa na mwenza wako.

JIKUBALI

Kama unaamini kuwa matatizo umeumbiwa wewe kama mwanadamu, basi kwa yote yaliyokupata ya kuumiza moyo wako. Jifunze kuukubali ukweli, jikubali mwenyewe kuwa unaweza pamoja na changamoto mbalimbali unazokutana nazo.

SONGA MBELE Ukilikubali tatizo na ukajikubali, hapo akili yako inakuwa imeona mwanga wa mafanikio, kwani akili yako utaipa nafasi ya kusonga mbele kwa ajili ya mapambano mengine mapya ya mafanikio na siyo kubaki palepale kwenye tatizo.

KUACHIKA/KUACHWA

Kama uhusiano wako una mgogoro, hakikisha unalipigania penzi lako, lakini kama ikishindikana, ukaachika au ukaachwa, usikate tamaa, bali anza maisha mapya.

Cha kufanya, anza kupigana kwa uchungu hasa ili kufikia malengo kwa ajili ya maisha yako ya leo na siku zijazo. FUNGUKA KIAKILI Umekuwa ukiteseka na kunyanyasika kwa sababu ya mapenzi. Kwa sababu uliyempenda amekuacha au kuachika kwenye penzi au ndoa yako. Ndugu yangu uliyeachwa au kuachika, funguka na tambua kuwa kuachika au kuachwa siyo mwisho wa mapenzi, maisha yapo na lazima yaendelee kama kawaida.

UMEACHIKA/KUACHWA KWA SABABU

Inawezekana umeachika ili uepukane na mambo mabaya makubwa ambayo yangekutokea siku zijazo. Amini kuwa umeachika au kuachwa na mwenza wako ili ujitambue. Wakati mwingine kuna mambo kwenye maisha yako ya kila siku yanatokea ili iwe fundisho kwako au kwa wengine, wewe uwe mfano na mwalimu wa wengine.

USIKUBALI MAPENZI YAKUHARIBIE

Hakuna kitu kinachokatisha watu wengi tamaa kama migogoro ya mapenzi. Mtu anafika sehemu na kujihisi labda hakustahili kuzaliwa katika dunia hii. Au labda anahisi kuwa yeye ni mbaya wa muonekano, ukosefu wa fedha, elimu na maisha mazuri ndiyo hasa yaliyochangia yeye kuachwa au kutelekezwa.

ANZA KUFANYA MABADILIKO

Kama wewe ni miongoni mwa watu waliokata tamaa kwa sababu ya kuachika au kuachwa, basi usomapo makala haya anza kubadilika, kwani akili hiyo ya kuhisi kuwa wewe huna thamani, ndiyo hiyo inakufanya ushindwe kufikia malengo yako, ushindwe kufanya maendeo kwa ajili ya maisha yako na kizazi chako cha baadaye.

USIJICHIMBIE KABURI

Ukiendelea kujiuliza kwa nini fulani alikuacha, basi ujue unajiumiza mwenyewe, kutafakari mambo ya nyuma yaliyokuumiza ni sawa na kujichimbia kaburi lako mwenyewe.

Fanya hivi, yale yote ya kale uliyokutana nayo kwenye uhusiano wako, tupa kule na acha moyo usukume damu na si mateso ya mapenzi. Kwa leo naomba niishie hapa, nakupenda sana msomaji wangu, kwa ushauri na maoni, tembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Amani, Insta:@ mimi_na_uhusiano au jiunge na M&U WhatsApp kwa namba 0679979785


Loading...

Toa comment