The House of Favourite Newspapers

Msiogope Kupigania Demokrasia ya Kweli – Sumaye

Waziri Mkuu Mstaafu wa serikali ya awamu ya tatu, Frederick Sumaye, akizungumza na wanahabari.

WANAMAGEUZI nchini wametakiwa kuendelea kupigania demokrasia ya kweli ambayo ndiyo itawapa ushindi na kuwapatia Watanzania kwa ujumla fursa ya kupata viongozi bora kutoka upande wa upinzani.

Waziri Mkuu Mstaafu wa serikali ya awamu ya tatu, Frederick Sumaye, akizungumza na wanahabari.

Hayo yamesemwa na waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, wakati wa mkutano mfupi uliohusu utaratibu wa kutolewa kwa Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali. Kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo  (Chadema) aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela na Mahakama ya Wilaya ya Kilombero ambapo juzi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilimwachia huru baada ya kushinda rufaa yake.

Sumaye alisema Chadema hakitasita kuendelea kuzunguka nchi nzima  kuzungumza na wananchi ili kuwaeleza namna demokrasia ya kweli inavyopatikana, mateso wanayoyapata katika kipindi hiki kuwa ndiyo yatawafanya wawe  imara kwa chama chao na hatimaye kushika dola.

Mbunge Lijualikali akikumbatiana na Sumaye baada ya kuachiwa.

Uamuzi wa kuachiwa huru mbunge huyo ulitolewa na Jaji Ama-Isario Munisi baada ya kukubaliana na hoja za warufani kwamba hati ya mashtaka dhidi yao ilikuwa na upungufu mkubwa usioweza kurekebishika katika hatua ya rufaa.

“Upungufu katika hati ya mashtaka ni mkubwa hivyo mahakama inatengua adhabu za kifungo alichopewa mshtakiwa na inaamuru aachiwe huru,” alisema jaji huyo siku aliyosikiliza rufani hiyo.

Lijualikali alikuwa amefungwa kwa kesi tatu ambazo ni kufanya vurugu na kusababisha taharuki wakati wa mkutano wa uchaguzi wa mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Ifakara ambapo alitiwa hatiani na kuhukumiwa kwa kesi namba 338 ya mwaka 2014, kesi namba 220 ya mwaka 2014 na kesi namba 340 ya mwaka 2014.

Mama mzazi wa Wema Sepetu akitoka katika ofisi za Chadema zilizopo Ukonga-Mombasa palipofanyika mkutano mfupi na wanahabari baada ya Lijualikali kuwa huru.

Na Denis Mtima/GPL

Comments are closed.