Kutokana na hali hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad, aliagiza wale vote waliohusika na ubadhirifu na udanganyifu wa mabilioni ya fedha, wachukulie hatua kali.“Ukaguzi umejiridhisha kwamba, uongozi, wafanyakazi, watoa huduma na wazabuni wameshiriki kwa namna moja au nyingine katika ubadhirifu na udanganyifu kwenye matumizi ya fedha katika mradi wa kuboresha vitambulisho vya taifa,” alisema.
Kwa hali hiyo, CAG amependekeza kampuni ya uwakala wa bima irejeshe Sh bilioni 1.2 zilizolipwa zaidi isivyostahili; na hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya Astery Ndege na kampuni hii kwa kufanya udanganyifu na kujipatia fedha kutoka mamlaka.
Ubadhirifu mwingine alioutaja ulikuwa ni manunuzi ya bima ya vifaa vya usajili na magari yaliyotumika katika mradi wa vitambulisho vya Taifa ya jumla ya Sh milioni 494, yaliyofanyika bila kukihusisha Kitengo cha Manunuzi.
CAG pia ameshauri hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya watumishi waliohusika katika udanganyifu, uliobainishwa na kutozingatia sheria za manunuzi ya umma na kuisababishia Mamlaka gharama zisizo na tija sanjari na kuhakikisha kuwa wahusika wanafidia hasara iliyopatikana, kisha kuhakikisha udhibiti wa vifaa.
Uhakiki wa leja za mafuta, pia ulibaini kuwa lita 1,110 za mafuta ya dizeli yenye thamani Sh milioni 2.2 zilitumika kwa shughuli zisizo za Mamlaka.
Pia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilikopa Sh milioni 455.3 kutoka NIDA kwa ununuzi wa magari manne mwaka 2014, ambazo hadi ukaguzi unafanyika Oktoba 2016 fedha hizo hazikuwa zimerejeshwa.
Uhakiki wa fomu zenye ‘Barcode’ zilizotengenezwa kupitia mpiga chapa binafsi M/s MFI Solution, ulibaini kuwa fomu 7,762,907 zenye thamani ya Sh bilioni 2.5 zilizopokelewa na mamlaka hazikutumika.
Kadhalika, ilibainika kuwa fomu 8,220,000 zenye thamani ya Sh milioni 519.6 zilizochapishwa tangu mwaka 2011/2012 hadi 2013/2014 hazikutumika; hivyo kutelekezwa katika stoo za TANITA.
“Hali hii ilitokana na mamlaka kutokuwa na Mpangokazi, hivyo kuingia hasara ya Sh milioni 932.8,” ilisema ripoti hiyo.
Aidha, kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 mpaka 2015/2016, Mamlaka ilifanya matengenezo ya magari kupitia gereji binafsi yaliyogharimu Sh bilioni 1.3.Nida pia ilifanya matengenezo yaliyogharimu Sh bilioni 1.1 yaliyofanyika na kulipwa na Mamlaka bila kufanyika ukaguzi unaothibitisha kuwapo kwa ubovu wa gari na mahitaji ya matengenezo husika.
Pia kulikuwa na matengenezo yaliyogharimu Sh milioni 197.2, yaliyofanyika na kulipiwa na Mamlaka bila kufanyika ukaguzi wa awali wala ukaguzi baada ya matengenezo.
Ripoti imeeleza kuwa ukaguzi ulibaini malipo ya Sh milioni 42.7 yalifanyika zaidi ya madai stahili kutokana na udanganyifu wa kuongeza tarakimu katika hati za madai na kutumiwa kwa hati moja ya madai zaidi ya mara moja katika malipo ya kuanzia mwaka 2012/2013 hadi 2015/2016.
NIDA imegundulika kuwa ilikiuka sheria katika ajira za muda na za kudumu, zilizofanywa na mamlaka kuanzia mwaka 2012 hadi 2015, ambapo vibarua 1,071 walipatikana kwa kupigiwa simu bila kutangaza mahali popote kinyume na Sera ya mamlaka hiyo. Ukaguzi ulibaini kuwa NIDA iliomba kupatiwa vibarua kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Chuo cha Utumishi wa Umma wapatao 415.
NIDA pia inatuhumiwa kufanya malipo Sh milioni 16.6 ya kiinua mgongo kwa vibarua, kinyume na mkataba wa ajira ya muda na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004.
Ubadhirifu mwingine uligundulika kwenye matumizi ya mafuta ya dizeli na petroli, yaliyonunuliwa na mamlaka yenye thamani ya Sh bilioni 2.3, yaliyotolewa kwenye magari na majenereta, ambapo hayakuthibitika matumizi yake kutokana na sababu mbalimbali.
Upangishaji nyumba Mamlaka ilitoa zabuni ya kuipangisha Ofisi ya Mamlaka kwa Mary Mwema kupitia barua ya maombi ya tarehe 06.05.2012 ambapo tangazo la zabuni husika ni la tarehe 25.05.2012 baada ya tarehe ya kuomba.
“Zabuni husika haikupitia Kitengo cha Manunuzi na haikuwa imeidhinishwa na Bodi ya Zabuni,” inasema ripoti hiyo.
Pia ripoti ilifafanua kuwa mzabuni wa upangishaji wa jengo la ofisi ya John Masenga haukujumuishwa kwenye mchakato wa tathmini ya kitaalamu licha ya kukidhi vigezo.