The House of Favourite Newspapers

Video: Mbunge Atema Cheche Siku ya Uhuru wa Habari

0
Mhariri wa Gazeti la Uwazi, Elvan Sitambuli, akiongea katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari  Duniani katika hoteli ya Atriums, Afrika-Sana, Sinza, Dar es Salaam,  leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taporea, George Maziku, akiongea jambo.
Mbunge wa Viti Maalum (CUF) Mkoa wa Dar es Salaam, Salma Mwasa  (kushoto) akiongea na wanahabari (hawapo pichani) pembeni yake ni George Maziku.
Wanahabari wakiwa katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani katika hoteli ya Atriums leo.

Na Elvan Stambuli
DAR ES SALAAM: Mbunge wa Viti Maalum (CUF) Mkoa wa Dar es Salaam, Salma Mwasa ametema cheche leo kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa kuwaambia hawako huru kama miaka ya nyuma.
Hata hivyo aliwapa matumaini wana habari hao kwa kuwaambia kuwa yeye na wenzake bungeni wataendelea kuisimamia na kuikosoa serikali na hatimaye mambo ya habari yatakuwa mazuri kuliko ilivyo sasa.
Akizungumza na wanahabari katika ukumbini hapo wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika kimkoa hotelini hapo na kuratibiwa na Chama Cha Waandishi wa Habari za Kisiasa Tanzania (Taporea), Mbunge Mwasa alisema: “ Hali ya uhuru wa vyombo vya habari siku hizi siyo nzuri kama huko nyuma kwani mlikuwa huru zaidi kuliko sasa,” alisema mbunge huyo aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la CUF, Julius Mtariro ambaye alipangwa kuwa mgeni rasmi lakini akashindwa kuja kwa maelezo ya Mwasa kwamba yupo kwenye ziara ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamadi jijini Dar es Salaam.
Alisema anayasema hayo kwa sababu tayari wameshuhudia vyombo vya habari vikifungiwa serikali inapokosolewa na akasema hata sheria ya vyombo vya habari iliyopitishwa na bunge hivi karibuni kuna vipengere vinavyokandamiza wana habari lakini watawala wameipitisha.

“Ni jukumu letu sote kuhakikisha sheria hizo kandamizi zinarejeshwa bungeni na kufutwa, niseme kwamba tutaomba sheria irudi bungeni ili irekebishwe,” alisema Mwasa.
Akaongeza kuwa serikali ilipaswa kuwasikiliza wana habari na wadau wengine wa habari ili kuhakikisha kwamba zile sheria kandamizi zinazolalamikiwa, zinaondolewa bila kipingamizi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taporea, George Maziku alisema uhuru wa vyombo vya habari upo shakani kwani chombo kikiandika habari ya kukosoa taasisi au mashirika ya umma na hata serikali, vinatishiwa kunyimwa matangazo.
Alilaani kitendo cha mkuu wa mkoa wa Dar kuvamia chombo cha habari akiwa na askari wenye silaha za moto na kuwashambulia pia kuwatisha na kuachwa bila kukemewa na kiongozi yeyote wa serikali badala yake akapongezwa.
Maziku alimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers, Eric Shigongo kwa mchango wake katika kufanikisha hafla hiyo hotelini hapo na akawaomba wadau wengine kuiga mfano huo.

Leave A Reply