The House of Favourite Newspapers

“Shocking!” Jay Z, Gloria Carter Na Hadithi Iliyoushtua Ulimwengu

0

SIKU kadhaa zilizopita, nguli wa Muziki wa Hip Hop duniani, Shawn Carter ‘Jay Z’ aliachia albamu yake mpya, 4:44 kupitia mtandao anaoumiliki wa Tidal, ikiwa ni albamu yake ya kumi na tatu na kuvunja ukimya mrefu wa tangu mwaka 2013 alipotoa albamu yake ya Magna Carta Holly Grail.

Shawn Carter ‘Jay Z’ akiwa na mama yake.

Katika albamu hiyo, Jay Z ambaye pia ni mume wa staa Beyonce Knowles, wakiwa wamejaaliwa kupata watoto watatu, Blue Ivy na wadogo zake mapacha, Rumi na Sir amefanya jambo ambalo ama kwa hakika limeushangaza ulimwengu (shocking).

Muda mfupi baada ya kuachiwa kwake, gumzo kubwa liliibuka kuhusu mashairi yaliyomo kwenye moja kati ya nyimbo kumi zilizopo kwenye albamu hiyo. Wimbo wa Smile ambao Jay Z amemshirikisha mama yake mzazi, Gloria Carter ndiyo ulioibua utata kutokana na mashairi yake kubeba ujumbe mzito ambao pengine hakuna ambaye alitegemea kuusikia.

“…Mama had four kids, but she’s a lesbian, had to pretend so long that she’s a thespian…” (Mama ana watoto wanne lakini ni msagaji, kwa kipindi kirefu amekuwa akijifanya ni mwigizaji wa tamthiliya…).

Haya ni miongoni mwa mashairi yaliyoibua gumzo kubwa dunia nzima, hasa kutokana na ukweli kwamba mama yake Jay Z, Gloria pia anao watoto wanne, akiwemo Jay Z mwenyewe ambaye ni wa mwisho. Watoto wengine ni kaka yake Jay Z, Eric na dada zake, Andrea na Michelle.

Kwa lugha nyepesi, baada ya tetesi za chini kwa chini za muda mrefu, Jay Z amevunja ukimya na kutangaza hadharani kwamba mama yake anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

“…Don’t matter to me if it’s a him or her, I just wanna see you smile through all the hate,” (Kwangu haijalishi kama ni mwanaume au mwanamke, ninachotaka ni kukuona ukitabasamu katikati ya chuki) Jay Z anazidi kufunguka kwenye wimbo huo.

Yote tisa, kumi ni kipande cha mwisho ambapo Gloria anasikika kwa sauti yake mwenyewe, akikiri kwamba amekuwa akiishi kwenye maisha ya kujificha gizani kwa muda mrefu akihofia kusema hadharani kwamba yeye ni msagaji lakini muda umefika wa kutabasamu na kuwa huru kwa vile alivyo.

“Living in the shadows. Can you imagine what kind of life it is to live? In the shadows people see you as happy and free. Because that’s what you want them to see… But life is short, and it’s time to be free. Love who you love, because life isn’t guaranteed,”

(Kuishi gizani. Unaweza kuvuta picha ni aina gani ya maisha? Gizani watu wanakuona una furaha na upo huru. Kwa sababu hicho ndicho ulichotaka wakione… Lakini maisha ni mafupi, ni wakati wa kuwa huru. Mpende yule unayempenda kwa sababu maisha ni kigeugeu.)

 

Wimbo wa Smile unakuja kumaliza ubishi uliokuwepo kwa muda mrefu, tangu mwaka 2013 tetesi zilipoanza kuzagaa kwamba mama yake Jay Z, alikuwa akijihusisha na mapenzi ya jinsi moja na aliyekuwa mwalimu ambaye kwa sasa anafanya kazi kwenye mfuko wa kusaidia jamii wa Jay Z na mama yake, The Shawn Carter Foundation, Dania Diaz.

Smile umethibitisha kwamba Gloria na Dania wamekuwa wapenzi kwa muda mrefu sasa, huku kukiwa na picha zinazomuonesha mwanadada huyo akiwa na Jay Z. Gloria na Dania walianza kuandamwa na waandishi wa habari za uchunguzi baada ya kuwepo kwa ukaribu unaotia shaka kati yao ambapo sasa Gloria mwenyewe ameamua kuuweka wazi.

Wawili hao, kwa mujibu wa Jarida la Enstar, wamekuwa wakizisaidia jamii za watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsi moja (LGBTQ- Lesbian, Gay, Bisexual, Transgender and Queer) jijini New York.

Yote kwa yote, ujasiri waliouonesha Jay Z na mama yake, Gloria umewashangaza watu wengi mno duniani. Kwa tamaduni za Kiafrika, mtoto kuzungumzia ishu kama hiyo ya mzazi wake, ni utovu mkubwa wa nidhamu lakini Jay Z ameweza, na inaonesha walikubaliana ndiyo maana hata studio waliingia pamoja.

Kwa tamaduni za wenzetu, vitendo vya mapenzi ya jinsia moja vinaonekana kuwa vya kawaida na vinakubalika na baadhi ya mataifa, hasa Ulaya yamepitisha sheria za kutambua ndoa za jinsia moja. Kwa Tanzania, uhusiano wa namna hiyo HAUKUBALIKI kisheria wala kijamii.

IMEANDIKWA NA HASHIM | IJUMAA

Leave A Reply