The House of Favourite Newspapers

Mayanga: Cosafa itatubeba Chan

0
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga (kushoto) akiongea jambo.

KOCHA wa Taifa Stars, Salum Mayanga amesema michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa) itakisaidia kikosi chake kuelekea mchezo wao wa kusaka nafasi ya kufuzu kwa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan), dhidi ya Rwanda.

Taifa Stars ambayo ilikuwa ikishiriki michuano ya Cosafa ikiwa mgeni mwalikwa, mbio zao ziliishia hatua ya nusu fainali baada ya kufungwa na Zambia mabao 4-2. Kabla ya hapo ilianza hatua ya makundi ambapo matokeo yake yalikuwa hivi; Tanzania 2-0 Malawi, Tanzania 0-0 Angola, Tanzania 1-1 Mauritius. Jana usiku Taifa Stars ilicheza mechi ya kuwania nafasi ya tatu dhidi ya Lesotho.

 

Katika robo fainali, ikawafunga wenyeji, Afrika Kusini kwa bao 1-0 kabla ya kukwaa kisiki kwa Zambia na jana ilitarajiwa kucheza na Lesotho katika mchezo wa kuwania mshindi wa tatu.

Ikumbukwe kuwa, Julai 15, mwaka huu, Taifa Stars itaikaribisha Rwanda kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ukiwa ni mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Chan zitakazofanyika mwakani nchini Kenya.

“Kilichotokea kwenye michuano hii ni sehemu ya soka, lakini naamini vijana wangu wamepata cha kujifunza kuelekea mchezo wetu wa kufuzu Chan dhidi ya Rwanda, tunawaahidi Watanzania kuwa tutawawakilisha vizuri, lakini na wao tunahitaji sapoti yao,” alisema Mayanga.

Endapo Taifa Stars itaifunga Rwanda na kuiondosha, basi itakutana na mshindi wa mchezo baina ya Uganda dhidi ya Sudan Kusini.

OMARY MDOSE, CHAMPIONI JUMAMOSI

Leave A Reply