The House of Favourite Newspapers

Kamwamba: Nakuja Kumaliza Utawala wa Chichi Mawe

0

ISRAEL Kamwamba, raia wa Malawi ni mpinzani wa Francis Miyeyusho ‘Chichi Mawe’ ambaye anayo rekodi ya kucheza mapambano nane na yote ameshinda, matano yakiwa kwa KO, rekodi inayoonesha ni bondia ambaye ni moto wa kuotea mbali kufuatia kukaa juu ya ringi kwa raundi 34. Julai 22, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Dar live, Chichi Mawe atapanda ulingoni kukipiga na Israel Kamwamba huku mabondia wengine, Nasibu Ramadhan ‘Pac Man’ akizichapa na Tinashe Mwadziwana wa Zimbabwe wakati Idd Pialali akipanda ulingoni dhidi ya Regin Champion kutoka DR Congo, wote wakiwania mkanda wa Global TV.

Utamu wa pambano hilo ambalo litarushwa mubashara na kituo cha Global Tv Online unatokana na tofauti ya staili za miguu wanazotumia mabondia hao, Chichi Mawe ni Southpaw yaani anatanguliza mguu wa kulia mbele wakati Kamwamba ‘Israel Mweusi’ ni Orthodox yaani anatanguliza mguu wa kushoto mbele hivyo hapo ushindani wa kimataifa utaonekana kabisa kwa kuwa kila mmoja anahitaji kuchukua ubingwa.

Mapambano hayo ya kimataifa, yameandaliwa na kampuni ya kupromoti mchezo wa ngumi za kulipwa nchini, Solid Rock Tanzania na yatasimamiwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO) chini ya rais wake, Yassin Abdallah ‘Ustaadh. Akizungumza na Ijumaa, Kamwamba alifungukia pambano hilo kuwa, anajiandaa vizuri na kwamba anataka kazi yake iwe ya heshima hasa kuhakikisha anapata ushindi wa aina yake. “Natambua nakujaTanzania kwa ajili ya pambano langu dhidi ya Francis Miyeyusho, ni pambano langu la kwanza kubwa la ubingwa ndani ya Tanzania.

“Nalipa nafasi ya umuhimu na ukubwa ili nioneshe kipaji na ubora wangu lakini vilevile litaniweka katika ramani ya dunia kutokana na ubingwa ambao tutaucheza kuwa ni wa Global TV, Afrika Mashariki na Kati,” alisema Kamwamba na kuongeza: “Siyo kitu kidogo kwangu licha ya meneja wangu kufanya kazi mara kibao na mabondia wa Tanzania kama Francis na Cosmas Cheka pamoja na Jay Msangi hivyo

kwangu ni kitu cha heshima. Nina rekodi nzuri lakini mpinzani wangu kidogo amenizidi ila siwezi kumhofia.” Kamwamba pia aliwashukuru waandaji wa mapambano hayo, Global TV Online kwa hatua hiyo kubwa ya kumchagua kwani ni jambo kubwa kwake na la kujivunia. “Nasema hivi kutokana na maandalizi ambayo naendelea kuyafanya kwa kuwa mmoja kati ya mabondia ambao nafanya nao mazoezi yeye atakuwa akielekea Kosovo. Nataka

kuwaambia Watanzania kuwa nakuja kumaliza utawala wa Miyeyusho kwa sababu siogopi uzoefu wake wa muda mrefu aliokuwa nao tena asipokuwa makini nitampiga kabla ya raundi ya nane,” aliongeza Kamwamba. Kamwamba alimalizia kwa kuongelea mashabiki wa Malawi jinsi watakavyolipokea pambano hilo ambalo litarushwa live na Global TV Online.  “Hiki ni kitu kizuri kwangu na kwao kwa sababu wataweza kuona kazi nitakayokuwa naifanya ulingoni na kujua ubora wa kiwango changu.

Global TV itawasaidia ndugu zangu na mashabiki nchini kwetu kuweza kuniona wakati nikicheza na nitawaambia mapema njia yao wa kuweza kuona katika chaneli ya Global Tv ambayo inapatikana YouTube. “Nimeshawaambia kuwa wanachotakiwa kufanya ni kuhakikisha kwanza wanaingia YouTube na kutafuta Global TV Online kisha wanajiunga kwa kubonyeza neno (SUBSCRIBE), baada ya hapo wataona alama ya kengele ndogo iliopo pembeni yake na kubonyeza.

Ukishafanya yote hayo utakuwa unakumbushwa kuangalia pambano hilo mara tu litakapoanza.” Katika hatua nyingine, pambano hilo, halitakuwa na kiingilio na mashabiki wataweza kulishuhudia mubashara kupitia simu zao za mkononi na kompyuta, kwani litaoneshwa na Global TV pekee. Wadau na mashabiki watakaopata nafasi ya kuingia ukumbini wataingia kwa kadi maalum za mwaliko tu. Kama wewe umeshajiunga, basi hakikisha pia umebonyeza kikengele ili usipitwe na kila kinachoendelea Global TV. Pia unaweza kutupata kupitia mtandao wa www.globaltvtz. com, jiunge sasa na Global TV ili uwe wa kwanza kuona ndondi za kimataifa. Jiunge sasa kwa kuingia www. youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply