The House of Favourite Newspapers

Tukipanda Viongozi Kwa Rushwa Uchaguzi TFF, Tutegemee Kuvuna Soka La Rushwa

0
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF, Revocatus Kuuli (katikati) akiongea.

KWA muda mrefu nimekuwa niki­andika makala zinazohusiana na rushwa katika soka la nchi yetu kwa lengo la kuutahadharisha umma juu ya masahibu yanayoendelea am­bayo hakuna ubishi kwamba yana­haribu mfumo mzima wa kiuende­shaji wa soka kwa ngazi zote kuanzia chini mpaka timu ya taifa.

 

Duniani kote vitendo vya rushwa michezoni vimekuwa vikipigiwa kel­ele na mamlaka za soka lakini bado wahusika wamekuwa wakitumia mbinu nyingi za kuendeleza jambo hilo kwa kificho, huku wakitambua kwamba kufanya hivyo ni kosa kubwa ambalo halihitaji kusame­hewa kwa namna yoyote ile ili kulin­da hadhi ya soka.

 

Tumeshuhudia katika mataifa mengi tu duniani vitendo hivyo viki­vuruga taswira nzima ya soka kwa baadhi ya wanafamilia kupanga ma­tokeo, kuhonga waamuzi na hata kuhonga viongozi wanaosimamia michuano fulani kwa lengo la kuji­patia ushindi wasiostahili.

 

Wengine huenda mbali zaidi kiasi cha kufikia hatua ya kuzihujumu klabu zao wenyewe kwa kurubuni wachezaji kadhaa ndani ya kikosi ili wacheze chini ya kiwango ili kujifu­rahisha wao na wale waliowakusu­dia, lakini wakitambua kuwa kufan­ya hivyo hakuleti maendeleo yoyote ya kuisogeza mbele nchi yetu kufika katika viwango vya juu vya soka.

 

Ukichunguza kwa makini mzizi wa hayo yote utagundua kuwa, un­aanzia kwenu viongozi mliopewa dhamana ya kusimamia soka letu ambao mmeaminiwa na wapiga kura kwa kuwachagua kwa kura nyingi baada ya kutamba na maneno matamu ya kuleta matumaini wakati wa kampeni zenu za kuomba ridhaa ya uongozi katika chaguzi.

 

Agosti 12, mwaka huu taifa litashuhudia patashika za uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) utakaowaweka madarakani rais, makamu wake na wajumbe kadhaa walioomba ridhaa ya kuwa viongozi wa taasisi hiyo nyeti iliyo na dhamana ya kusimamia na kuratibu shughuli zote zinazohusiana na soka katika nchi yetu.

 

Sasa wakati tukisubiri uchaguzi huo kufanyika, tayari imesharipoti­wa kuwepo na vitendo vya rushwa kwa baadhi ya wagombea wa ucha­guzi huo ambapo wapiga kura wake wameanza kuwekwa kwenye kisa­hani cha kurubuniwa kwa kitu kidogo ili wawachague bila kujali uwezo wao wa kuongoza, weledi, uadilifu na nia iliyowasukuma mpaka kufikia hatua ya kujitosa kwenye kinyang’anyiro kuomba ridhaa ya kuongoza.

 

Kwa mtindo huo unaweza ukajiuliza ni kwa kiasi gani Tanzania inaweza kupiga hatua katika maendeleo ya mpira wa miguu kama watachaguliwa viongozi waliopigiwa kura kwa kutoa rushwa? Swali hili lina majibu rahisi tu kwamba Tanzania haiwezi kupiga hatua yoyote kwa kuwa mfumo mz­ima wa uendeshaji utagubikwa na vitendo vya rushwa na kukosekana kwa ushindani wa kweli unaozingatia vigezo.

 

Ifike wakati tuache kuoneana aibu katika masuala muhimu yanayobeba maslahi ya taifa zima, kama kweli tu­nahitaji kupiga hatua ya kimaendeleo ya soka kama yalivyo mataifa men­gine duniani ambayo yamedhamiria kwa vitendo kujiletea mafanikio kupitia medani hiyo, vinginevyo basi tutaishia kuwa wasindikizaji kila kukicha na kuwaacha wenzetu wakizidi kuchanja mbuga.

 

Nitumie makala haya pia kuiponge­za Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kwa kuthubutu kwa vitendo kutimiza wajibu wenu, kwani kwa muda mrefu wadau wamekuwa wakiwanyooshea ki­dole kwa kufumbia macho matukio mengi ya rushwa yaliyojitokeza am­bayo yamekuwa yakiziumiza klabu nyingi.

 

Klabu zinaweza kuwa na mikakati mizuri ya kupata ushindi katika michuano ili kufikia malengo wali­yojiwekea lakini harakati hizo zime­kuwa zikikwamishwa kwa makusudi na watu wachache ambao hawana nia njema katika maendeleo ya soka kwa taifa hili.

Madhara ya rushwa katika soka ni mengi mno ikiwemo kufifisha ndo­to za wachezaji wanaotamani ku­vuka mipaka kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, kukatisha tamaa hata watoto wadogo wenye nia ya kucheza mpira na kudumaza mawazo na mbinu za watu wenye nia ya kutuletea mafanikio ya kweli kwenye soka kwa kutumia njia zina­zokubalika duniani kote.

 

Ushauri wangu kwenu Takukuru, msije mkalegeza kamba kwenye ufuatiliaji ili kuwabaini hata wale waliojificha kwenye vichaka sugu vya rushwa, naamini kwa kufan­ya hivyo mnaweza mkawa nguzo muhimu na chachu kwa taifa kuele­kea maendeleo ya kweli katika soka.

MCHAMBUZI: OMARY KATANGA | CHAMPIONI JUMAMOSI

Ziggy: Sitaki Kuitwa Msanii Wa Bongo Movie

Leave A Reply