The House of Favourite Newspapers

VIDEO: Ustaadhi Afanyiwa Ukatili wa Kutisha

0
Ustaadhi Said Michael akionyesha majeraha yake.

 

AMA kweli dunia katili! Ustaadhi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Said Michael amesimulia ukatili mzito aliofanyiwa na watu wasiojulikana wa kuingiziwa kitu chenye ncha kali sehemu zake za siri na kumsababishia matatizo makubwa ya kiafya, Ijumaa limezungumza naye.

Akiwa ndani ya ofisi ya gazeti la Ijumaa juzi, ustaadhi huyo ambaye kwa muonekano huwezi kujua kama ana tatizo kubwa mwilini, kwanza aliomba atafutiwe sehemu ya kupumzika kwa kuwa alikuwa akijisikia vibaya na asingeweza kukaa kwenye kiti kwa muda mrefu.

 

AANZA SIMULIZI AKIWA AMELALA

Akizungumzia jinsi alivyopatwa na tatizo hilo, Said alisema: “Huko nyuma nilikuwa naishi Mwanza, nilikuwa nafanya kazi na taasisi moja ambayo nisingependa kuitaja, wakati huo nikifahamika kwa jina la Yohanna Michael. Hakika nilikuwa na maisha mazuri sana, nilijaaliwa kuwa na mali yakiwemo mabasi mawili. Nikaoa na kuyafurahia maisha.

“Shida ilikuja kuanza pale mwaka 2012 nilipoamua kutoka kwenye taasisi hiyo na kuhamia taasisi nyingine ambapo kuanzia hapo nilianza kuandamwa na majanga. Zile mali zangu zilianza kutaifishwa kimizengwe nikiambiwa zilikuwa ni mali za ile taasisi.

“Nilichokifanya wakati huo ni kujiendeleza katika dini hadi kufikia kiwango cha juu, kwa hilo namshukuru Mungu lakini sasa wakati huo nilikuwa nikizidi kusakamwa. Nilijikuta ghalfa nifilisika, mke wangu naye ambaye tulitofautiana aliamua kunikimbia na kuniachia watoto, mwaka 2014 ndipo nilipolazimika kukimbilia Dar kutafuta maisha lakini pia kujiendelea katika elimu ya dini.

 

 

Ustaadhi Said akionyesha majeraha yake.

 

“Kwa kweli maisha yalinibadilikia ghafla, ndugu walinitenga na hata Dar sikuwa na mtu wa kunisaidia, nililazimika kuomba hifadhi kwa ndugu yangu mmoja katika imani ambaye alinipa chumba kimoja pale Buguruni Kwa Mnyamani, nikawa naishi pale na watoto wangu.

“Niliendesha maisha katika hali ngumu sana, sasa kilichokuja kubadili kabisa maisha yangu na kupatwa na tatizo hili ambalo linanitesa mpaka leo kilitokea mwaka 2015 mwezi wa 6, sikumbuki vizuri tarehe.

“Siku hiyo saa sita usiku walikuja watu na kugonga mlango wakijitambulisha kuwa ni watu ninaofahamiana nao. Nikafungua mlango lakini nilipowatazama wale watu, sikuwahi kuwaona popote, kabla hata sijawauliza vizuri walinivamia na kuniingiza kwenye gari lao.

 

“Nikiwa ndani ya lile gari wakawa wananiuliza maswali ambayo sikuyaelewa, mwisho wakanifunga kitambaa na kunipeleka sehemu ambayo mpaka leo sijui ilikuwa ni wapi.

“Kufika huko wakaanza kunipa kipigo, nilipigwa sana hadi nikazimia, siku nyingine nilipozinduka nikajikuta niko vilevile nimefungwa kitambaa.

Wakawa wananipa chakula na kuendelea kuniuliza maswali ambayo bado sikuyaelewa, walifanya hivyo kwa kipindi kama cha miezi minne hivi, siku moja ndipo waliponiamulia.

 

“Wakanipiga sana na nilipokuja kuzinduka nikajikuta niko Muhimbili na wala sikujua nilifikaje pale. Wakati wananichukua siku ile nilikuwa nimevaa kanzu lakini nikajikuta nimevaa suruali ambayo ilikuwa imetapakaa damu. Nilisikia maumivu kila sehemu ya mwili hasa sehemu za siri.

“Nikiwa pale hospitalini ndipo nikasikia daktari mmoja akisema kuwa, nilikuwa nimeingizwa kitu chenye ncha kali sehemu za siri ambacho kilikwenda kuharibu mfumo mzima wa haja kubwa na ndogo.

“Niliumia sana kusikia vile, nikaanza kupatiwa matibabu pale lakini ilishindikana ndipo kwa msaada wa watu mbalimbali nikapelekwa India. Huko nilipata matibabu ambapo niliwekewa mpira flani ambao ulikuwa ukisaidia kwenye kukabiliana na ile hali.

 

“Kabla ya kuwekewa ule mpira, nilikuwa napata haja kubwa na ndogo kwa wakati mmoja na nilikuwa sina uwezo wa kuzuia. Ilikuwa ni adha kubwa.

“Baada ya kuwekewa ule mpira nikawa nimerudi Dar ambapo sasa ilikuwa natakiwa kuwa nakwenda Muhimbili kila baada ya wiki moja kwa ajili ya kubadilishiwa ule mpira na gharama yake ni shilingi 100,000.

“Kwa kusaidiwa na watu niliweza kumudu kwa kipindi flani ila ikafika wakati nikawa nakosa kiasi hicho cha pesa, hapo dipo nikaanza kuwa najizuia kwa njia za kienyeji kwa kutumia mfuko wa rambo.

 

Ustaadhi Said.

 

MAISHA YAKE KWA SASA

“Naishi maisha ya shida sana, hapa nilipo sina uhakika hata wa pa kulala. Kile chumba kule Buguruni ambacho nilikuwa nimewahifadhi watoto wangu nacho nimeambiwa nitoke. Sina pa kwenda.

“Ndugu zangu katika imani wamenisaidia sana kwa michango yao lakini bado hali yangu inazidi kuwa mbaya.

“Hali inazidi kuwa ngumu kwa sababu siwezi tena kwenda kutafuta rizki, nikipanda kwenye daladala natoa harufu mbaya na kila ninapokwenda lazima niwe nimejiwekea huu mfuko. Napita katika kipindi kigumu sana.

 

ANACHOOMBA KWA WATANZANIA

“Kwa kweli kwa hili tatizo naomba msaada kwa Watanzania wenzangu, nimeambiwa kwa matibabu ya tatizo hili angalau niwe na shilingi 1,600,000 (milioni moja na laki sita) hivyo kwa yoyote aliyeguswa na tatizo langu anisaidie kwa chochote kile kupitia namba 0653 171596, jina ni Said Michael.

 

KUTOKA GAZETI LA IJUMAA

Mwandishi wetu alipata nafasi ya kulichunguza tatizo alilonalo Said, hakika ni kubwa na linahitaji huruma yako ili aweze kupona hivyo kama Mungu amekujaalia chochote na kwa kuwa kutoa si utajiri, basi mchangie na Mungu atakulipa.

MSIKILIZE USTADH AKISIMULIA MKASA HUO

Leave A Reply