The House of Favourite Newspapers

Mafanikio Ni Kwa Kijana Na Mzee, Kwa Nini Ukate Tamaa?

0

AWALI ya yote niwasisitize tu kwamba, kama una jambo lolote linakusumbua kuhusu maisha, wasiliana na mimi ili niweze kukushauri. Kukumbuka tu kwamba, hutakiwi kujikusanyia matatizo kwenye maisha yako, kwa kufanya hivyo huwezi kuishi mwa amani na mwishowe utaona huna thamani ya kuishi. Baada ya kusema hayo sasa nigeukie kwenye mada yangu niliyodhamiria kukuandika kwa wiki hii.

 

Ni kwamba, katika maisha ya sasa, kila mtu anatamani kuwa na mafanikio makubwa. Kila mtu anatamani kuwa tajiri. Hata kama siyo utajiri mkubwa kama walivyo wale mabilionea wanaotikisa duniani lakini angalau mtu awe na pesa za kutosha benki huku akiwa na miradi yake inayomuingizia kipato kila siku.

 

Hiyo ndiyo ndoto waliyonayo wengi, ndiyo maana unashuhudia baadhi ya watu wakiwa hawalali, wanafanya kazi usiku na mchana kusaka pesa kwa njia halali wakiamini ndizo zitakazowafanya waishi maisha mazuri.

 

Cha kushangaza sasa, wapo watu wenye dhana potofu juu ya utafutaji wa mafanikio. Kuna vijana huko mtaani ambao wana nguvu za kutosha huku wakiwa wamejaaliwa maarifa lakini eti wamekata tamaa na maisha wakihisi hata wafanyeje hawawezi kufanikiwa. Hivi nani kasema mafanikio ni kwa ajili ya watu flani tu? Mafanikio ni kwa kila mmoja wetu bila kujali jinsia yake, umri wake, kabila lake wala anapoishi. Ndiyo maana kuna watu wako vijijini lakini wana mafanikio makubwa.

 

Wapo watu walikulia kwenye familia masikini lakini leo hii wanaogelea kwenye utajiri. Hiyo inadhihirisha kuwa, mafanikio yanapatikana popote, kwa mtu yoyote, mwenye umri wowote aliyedhamiria kuyapata. Kikubwa ni kujua kanuni za kufuata kwenye kuelekea mafanikio.

 

Lakini sasa, katika makala haya naomba niweke kitu kimoja wazi kwamba, usije ukakata tamaa ya kutafuta mafanikio kwa kikwazo cha umri wako.

 

Hili lipo kwa baadhi ya watu. Unakuta mtu alianza kupambana kusaka mafanikio akiwa na umri wa miaka 20, anafikisha miaka 40 akiwa bado hajafanikiwa kivile, anakata tamaa.

 

Hebu msikie huyu kijana ambaye anaonesha wazi ameyapa kisogo mafanikio kwa sababu tu anaamini kwa umri alionao, hata afanyeje hawezi kufanikiwa tena. “Mimi nilianza kutafuta pesa baada ya kumaliza darasa la saba, nilikuwa nafanya biashara ya kuuza mitumba.

 

Niliifanya biashara hiyo kwa muda mrefu kabla ya kufungua duka langu Kariakoo. Kusema ukweli ni muda mrefu nimeifanya biashara hiyo lakini mpaka leo hii siyaoni mafanikio niliyoyatamani “Ni kama nacheza ngoma ya kimasai kwani nikienda mbele kidogo, narudi nyuma.

 

Inafika wakati nakata tamaa, sasa naelekea miaka 45. Hebu fikiria tangu nina miaka 19, mpaka leo sina mafanikio ya kueleweka, navunjika moyo kwa kweli,” anaeleza Juma Shabani wa Buguruni jijini Dar. Kuna kitu cha kujifunza kutoka kwa mfanyabiashara huyu.

 

Kwamba unaweza kuwa umepambana kwa muda mrefu katika kusaka mafanikio lakini mpaka leo hujafika unapopataka. Usife moyo, endelea kupambana. Huenda pia ulizembea huko nyuma, ukawa umebweteka ila ukaja kujistukia wakati umri umekwenda, kumbuka mafanikio hayaangalii umri. Hata mzee anaweza kupata mafanikio kama kweli anadhamiria.

Makala: Amrani Kaima Maoni/ushauri simu: +255 658 798787

Usipitwe na Matukio, Install App Yako ya Kijanja na Namba Moja Tanzania ya Global Publishers

Android ===>Google Play

iOS ===>Apple Store

Leave A Reply