The House of Favourite Newspapers

Tanesco Yaonywa Ukatikaji Umeme

0

 

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.

NAIBU Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewaagiza watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha kuwa hawakati umeme bila sababu maalumu na hivyo kuwaondolea wananchi adha ya kukosa nishati hiyo.

 

Naibu Waziri aliyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa TEDAP unaohusu upanuzi na ujenzi wa vituo vya kupozea umeme na njia za umeme, ambako vituo vya kupozea umeme alivyovitembelea ni Mbagala, Gongo la Mboto, Kipawa na City Centre.

 

“Umeme ukatike pale inapostahili tu, na endapo tatizo linatokea mfano kwenye mifumo ya umeme ni muhimu mkatoa taarifa mapema kwa wananchi,” alisema Mgalu.

 

Aliongeza kuwa ukatikaji wa umeme unasababisha malalamiko kutoka kwa wananchi kwani kukosekana kwa nishati hiyo kunaathiri shughuli nyingi hasa za kimaendeleo na kiuchumi zinazowaingizia kipato. Aidha, aliwaagiza watendaji wa Tanesco wanaosimamia mradi huo wa TEDAP jijini Dar es Salaam, kuhakikisha kuwa kazi hiyo inakamilika Desemba 15, mwaka huu.

 

Vilevile alieleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea vizuri na kwamba kukamilika kwake kutaboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika Jiji la Dar es Salaam.

 

“Nawaomba Watanzania wawe na matumaini na Serikali ya Awamu ya Tano kwani inajitahidi katika ujenzi wa miundombinu ya umeme, nia ikiwa ni nishati ya umeme kupatikana muda wote,” alisema Naibu Waziri.

 

Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Usafirishaji na Usambazaji Umeme kutoka Tanesco, Emmanuel Manirabona alisema shirika hilo linafanya juhudi mbalimbali ili utekelezaji wa mradi huo ukamilike ndani ya muda ulioelekezwa.

 

Mradi wa TEDAP unahusisha upanuzi na ujenzi wa vituo vipya 19 vya kupoza umeme wa msongo wa kilovoti 132/33 na kilovoti 33/11 pamoja na ujenzi wa njia za umeme wenye msongo wa kilovoti 132, kilovoti 33 na kilovoti 11 katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Kilimanjaro.

 

Gharama za utekelezaji wa mradi husika ni Dola za Marekani milioni 43, ambazo zimetolewa na Benki ya Dunia (WB) kupitia mradi huo.

(CHANZO: HABARI LEO)

Leave A Reply