KOCHA wa Simba, Pierre Lechantre ameanza kiburi kuelekea mechi yao ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga kwa kusema amefurahi uwepo wa kiungo wake mkabaji, Jonas Mkude katika mchezo huo.
Mkude hakucheza mechi iliyopita ya Simba wikiendi iliyopita dhidi ya Lipuli FC kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa iliyoisha kwa sare ya bao 1-1. Mkude alikuwa akitumikia adhabu ya kadi tatu za njano.
Akizungumza na Championi Jumatano, Lechantre alisema anafurahi uwepo wa Mkude katika mechi hiyo dhidi ya Yanga ambayo ni ngumu ili kuhakikisha anapata ushindi na kubaki kileleni mwa ligi hiyo.
Lechantre alisema, katika mechi iliyopita timu yake ilizidiwa katika safu ya kiungo baada ya kumkosa Mkude, hivyo hana hofu katika mchezo wa marudiano dhidi ya Yanga kwani tatizo hilo halitaonekana.
“Katika timu unapomkosa mchezaji muhimu anayeendana na mfumo wako inakuwa ni ngumu timu kucheza vile ninavyotaka kama ilivyojitokeza katika mechi na Lipuli.
“Alikosekana Mkude ambaye ndiye injini ya timu anayecheza kwa kuufuata mfumo na maelekezo yangu na kusababisha kupata matokeo mabaya ya sare.
“Mkude anacheza vizuri na kufuata maelekezo yangu na niseme ninafurahia kiwango kikubwa anachoendelea kukionyesha katika mechi za ligi ambazo zinaendelea,” alisema Lechantre.
Simba kwa sasa ipo kambini Morogoro kujiandaa na mchezo huo utakaochezwa Jumapili wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam
Comments are closed.