The House of Favourite Newspapers

VUVUZELA; WAZIRI MWAKYEMBE UNAFUNIKA TATIZO, HAULIMALIZI TATIZO

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.

 

MIEZI kad­haa iliyo­pita kupitia gazeti hili la Championi niliwahi kuandika makala ambayo ilijaa kwenye kura­sa mbili nilimsifia Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kutokana na utendaji kazi wake katika wizara hiyo.

 

Nilizungumza mengi naamini waziri alipata na­fasi ya kuipitia au hata watu wake walipata nafasi hiyo, naamini alipata muda huo wa kuipitia, basi hata kama haikuwa hivyo, imani yangu inaniambia wasaidizi wake waliiona.

 

Kwa faida ya wale ambao hawakuipitia au hawakuio­na kabisa naweza nikawa­kumbusha kwa ufupi kuwa, awali wakati Mwakyembe akiteuliwa kushika naasi hiyo nilipata hofu juu ya kuweza kuimudu kwa kuwa nilijua tasnia hiyo ina up­ande mmoja amao ina vi­jana wengi ambao wame­kuwa na kasi na maisha ya kidigitali.

 

Niliona Mwakyembe ni mtendaji mzuri lakini kwa aina ya maisha ya vijana wa sasa na kwa kuwa wizara yake inadili na vijana wengi pamoja na mambo ya kidigi­tali nilipata hofu kuwa kama ataweza kuendana na kasi ya vijana hasa kwa kuwa tunajijua sisi vijana tuna mambo mengi.

 

Waziri Mwakyembe alin­ionyesha kuwa nilikosea kumuwaza ndivyo sivyo kwa kuwa utendaji wake ulikuwa wa kasi na aliweza kumudu mambo mengi katika tasnia hiyo, mfano mwepesi ni jinsi alivyoanza kwenda sam­bamba na watu wa mchezo wa ndondi ambapo huko tunajua kuna uozo mkubwa.

 

Mwakyembe amekuwa mshiriki mzuri na mzungum­zaji mzuri pia katika masua­la mbalimbali ya kimichezo, ameonyesha jinsi gani ana­vyoweza kupambana muda mwingi ili kuendana na kasi ya serikali yake na kasi ya maisha ya vijana.

 

Kuna mengi mazuri am­bayo ameyafanya na kama nilivyosema nitayazungum­za kwa ufupi, lakini tunatak­iwa kukubali kuwa hawezi kufanya kila kitu peke yake, bali anachotakiwa ni kuten­geneza mfumo au njia am­bazo zinaweza kutumiwa na wasaidizi wake kufanya kile ambacho yeye anaona ni sahihi na kitakuwa na faida kwa taifa kwa jumla.

 

Tazama jinsi Rais Dk. John Pombe Magufuli ambavyo anatengeneza baadhi ya mambo kuingia kwenye mfumo fulani ambao ana­jua hata siku yeye akiwa hayupo bado mifumo hiyo ikitumiwa sahihi inaweza kuwa faida kwa taifa, hivyo ndivyo ambavyo anavyotaka watendaji wake wafanye.

 

Awali, msaidizi wa Mwakyembe, Juliana Shonza alilivalia njuga suala la maadili katika tas­nia ya muziki, yawezekana alikuwa na nia nzuri la­kini kwa mwendo aliokuwa akienda ilionekana kama anataka kufanya maisha ya mashindano.

Kilichotokea msanii wa Bongo Fleva, akamjibu kama anamjibu rafiki yake wa mtaani, majibu ya Dia­mond hayakuwa mazuri kwa kuwa ni wazi hata naibu waziri mwenyewe alionye­sha ushindani wa ‘ujana’.

 

Mwakyembe akaingilia hilo, na kulituliza, alitumia utu uzima wake, namponge­za kwa hilo, kilichofuaia baada ya hapo nilitegemea kungekuwa na mwendelezo wa kutengeneza njia sahihi ya nini ambacho wao kama wizara wanakitaka kuliko kusubiri wasanii wakosee kisha wawafungie.

 

Kama tunavyojua wasanii wanatumia nguvu kubwa kuwekeza katika fani yao, hivyo inapotea wanafun­giwa huku kukiwa hakuna njia sahihi za kuwaonyesha njia wanazotakiwa kupita ni kuwakandamiza.

 

Hata kama kuna njia am­bazo tunataka kuwaonyesha basi ifanyike kwa kuangalia uhalisia isiwe kukomoana.

Juzi tena, Mwakyembe akaibuka na suala la mui­gizaji mkongwe, Amri Athu­man ‘Mzee Majuto’, akadai anatoa fedha zake mfukoni kumsaidia, mara akaseka kuhusu kupitia mikataba ya makapumbuni yaliyofanya kazi na mkongwe huyo kuo­na kama kulikuwa na uhalali katika suala la mapato.

 

Ni jambo zuri analofanya, lakini halitasaidia jamii kwa kuwa kunatakiwa kuten­genezwa mfumo ambao utawasaidia wasanii wote wanaoingia mikataba ya matangazo na siyo kwa mtu mmoja pekee.

Kuwa na mfumo unaoweza kusaidia wengi ni kitu kizuri kwa kuwa katika mikataba hiyo hata serikali inaweza kuwa inapata pato kupitia makato ya kodi, lakini hiki anachokifanya mheshimiwa ni sawa na kufunika tatizo na siyo kumaliza tatizo.

VUVUZELA na John Joseph | Mawasiliano +255 713 393 542

Comments are closed.