The House of Favourite Newspapers

Yanga Kushiriki Michuano ya Kimataifa Mwakani, Kwa Mbeleko ya CAF

KWA kasi ya Simba ilivyo kwenye Ligi Kuu ya Bara, uwezekano wa Yanga kushiriki michuano ya kimataifa mwakani ni kwa mbeleko ya CAF tu ambayo ina nafasi ya upendeleo ila kwa masharti.

 

Ili CAF kuipa Yanga nafasi hiyo kuna masharti magumu ambayo kama Yanga wakiyaweza watakuwa wameweka rekodi ya aina yake mwaka huu na watakuwa tajiri kuliko klabu yoyote Tanzania na Afrika Mashariki kutokana na zawadi za nafasi hiyo. Kwa mujibu wa kanuni za CAF kuna namna mbili ambazo zinaweza kuipa timu ofa ya kushiriki mashindano ya msimu ujao. Kwanza ni kuangalia viwango vya ufanisi kwenye nchi husika ndani ya miaka mitano mfululizo katika mashindano husika.

 

Nchi zilizofanya vizuri kwenye mashindano hayo ndani ya miaka hiyo kwenye hatua ya makundi hupewa pointi maalum na viwango ambavyo huziongezea idadi ya timu shiriki kuanzia mbili na kuendelea kwenye Shirikisho na Ligi ya Mabingwa. Mfumo huo wa nafasi za ziada ndiyo ambao unaweza kuipa timu ambayo si bingwa kama Yanga nafasi kushiriki mwakani.

 

Lakini kutokana na mwenendo wa timu za Tanzania tangu 2013-17
ni wazi kwamba Afrika Mashariki hakuna nchi yenye vigezo vya kupewa ofa. Kigezo cha pili ambacho ndiyo njia pekee inayoweza kuibeba Yanga ni hatua ya makundi wanayoanza kushiriki leo ugenini dhidi ya USM Algiers. Kikanuni Yanga wameonyeshwa upenyo mmoja tu na CAF ambao ni kwa kucheza fainali na kutwaa ubingwa tu ambapo watakuwa mabilionea na kuandika historia.

 

Kwa mujibu wa kifungu cha IV) cha kanuni za mashindano ya Shirikisho Afrika kipengele kigogo cha 5) kinasema; “Chama cha Bingwa mtetezi hakitaruhusiwa kuwasilisha mshiriki mwingine endapo mabingwa watakuwa na nia ya kutetea taji lao. Bingwa ndiye pekee atashiriki kama chama husika kina nafasi moja tu ya Shirikisho.”

 

“Ikitokea kama chama husika kina sifa ya kuwasilisha timu mbili, Bingwa na timu iliyofuzu kwenye nchi husika ndio pekee watakaoruhusiwa kushiriki.” Kupewa nafasi ya Singida Kwa mujibu wa kanuni hiyo inamaanisha kwamba kama Yanga akiwa Bingwa wa Shirikisho, yoyote yule atakayeshinda fainali ya FA baina ya Mtibwa na Singida inabidi achukue mkwanja wake alale mbele.

 

Kanuni zitaipa Yanga nafasi ya kushiriki michuano ya mwakani kwa vile Tanzania haina vigezo vya kuingiza timu kwenye shindano moja. Hata hivyo, Mtibwa imefungiwa kushiriki michuano hiyo hivyo kama Yanga ikishindwa kutekeleza masharti ya CAF, Singida ndiyo itapewa nafasi hiyo.

MECHI 6 ZA YANGA KIMATAIFA

USM ALGER VS YANGA Leo Jumapili

YANGA VS RAYON Jumatano Mei 16, 2018

GORMAHIA VS YANGA Jumatano Julai 18, 2018

YANGA VS GORMAHIA Jumapili Julai 29, 2018

YANGA VS USM Jumapili Agosti 19, 2018

RAYON VS YANGA Jumatano Agosti 29, 2018

STORI NA MARTHA MBOMA, SPOTI XTRA

Comments are closed.