The House of Favourite Newspapers

Yanga: Tunamshusha Mshambuliaji, Watasema Yote

0
Ally Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga.

UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa upo kwenye hesabu za kumshusha mshambuliaji wa kazi atakayeongeza nguvu katika kikosi hicho jambo litakalowafanya wapinzani wao waseme yote kutokana na tabu watakayopata.

Uongozi huo umeongeza kuwa kwa straika huyo ambaye watamshusha mabeki wa timu pinzani watajuta.

Kauli hiyo imekuja baada ya mashabiki kupendekeza kusajiliwa straika hatari atakayekuja kuiongezea nguvu timu hiyo, katika Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Timu hiyo chini ya Kocha Mkuu Miguel Gamondi ina washambuliaji wanne ambao ni Clement Mzize, Kennedy Musonda, Hafiz Konkon na Crispin Ngushi huku kasi zao kwenye kucheka na nyavu zikiwa ni za kusuasua.

Yanga imekuwa ikihaha kumpata straika zaidi ya Mkongomani, Fiston Mayele aliyetimkia Pyramids FC ya Misri.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Ally Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga alisema kuwa wana mpango wa kumleta mshambuliaji wa kazi atakayeongeza nguvu katika kikosi hicho.

Kwa mujibu wa Kamwe wamesikia kilio cha mashabiki wao na wale wa timu pinzani (Simba) ambao hawana straika tishio katika msimu huu tangu alipoondoka Mayele.

Kamwe alisema kuwa wamesikia kilio chao wapinzani huku akiwataka mabeki wajiandae na balaa litakalowakuta baada ya usajili wa straika mpya kukamilika.

Aliongeza kuwa walipanga kufanya usajili wa straika katika msimu ujao, lakini kutokana na maneno ya wapinzani wamebadili maamuzi, sasa wanamleta fasta katika dirisha hili dogo.

“Hapa kwenye ligi tunafanya yote yale huku kukiwa na zile kelele kwamba hatuna mshambuliaji mwenye kasi na anayefunga sawa, lakini nani anaongoza kwenye chati ya ufungaji wa mabao? Haya yote yanatokea bado hatujamleta mshambuliaji wa kazi unadhani akija nini kitatokea?

“Hatupigi porojo bali kazi kwa vitendo, angalieni kwenye chati ya ufungaji nani anaongoza na kipi ambacho kinafanyika uwanjani? Tunawaamini wachezaji wetu na wanafanya kazi kwa kujituma hivyo ni suala la kusubiri.

“Wenyewe wapinzani wetu wameulilia wembe, hivyo wajiandae na ujio wa straika huyo mpya ambaye anakuja kuiboresha safu ya ushambuliaji katika msimu huu.

“Hatukuwa na mpango wa kumsajili mshambuliaji katika usajili huu wa dirisha dogo, lakini kutokana na kejeli na maneno ya wapinzani, kuwa hatuna straika wa maana, basi wasubirie ujio mpya katika usajili huu wa dirisha dogo .

“Muda wowote tutamtambulisha straika huyo mpya na ndani ya siku hizi tano, tutakuwa katika wakati mzuri wa kumtambulisha baada ya usajili wake kukamilika.

“Tumepanga kumsajili mshambuliaji mwenye uwezo wa kufunga mabao zaidi ya 20 katika msimu mmoja, katika ligi na michuano ya kimataifa,” alisema Kamwe.

Kwenye chati ya ufungaji ndani ya ligi namba moja ni Aziz KI mwenye mabao 10 kama ilivyo namba ya jezi yake.

NA Lunyamadzo Mlyuka, Championi Jumatatu

EXCLUSIVE: MREMBO ALIYEBAMBIWA na HARMONIZE JUKWAANI KAHAMA AFUNGUKA-“USINIFANANISHE NA GIGY MONEY”

Leave A Reply