Yanga wajuaji wengi, TFF wenye ‘akili’ wachache
WIKI jana nilielezea kuhusu mazingira ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kuhusu utendaji kazi wao, nitazungumzia na leo tena kidogo, lakini nimeona haitakuwa sawa wiki ikipita bila kutoa maoni yangu kinachoendelea ndani ya Yanga.
Yanga kuna wajuaji wengi Wakati Yusuf Manji akiwa kiongozi wa klabu hiyo ilikuwa raha kwa wengi, Wanayanga waliamini wao ndiyo wababe wa soka la Tanzania kwa kuwa walikuwa na nguvu ya fedha, wakasahau fedha hizo ni za mtu binafsi na siyo klabu.
Mara nyingi nimewahi kusema kuwa hilo lilikuwa kosa kwa kuwa kama TFF na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) wangeamua kufanya kitu kinaitwa ‘financial fair play’ basi ingekuwa tatizo kwa Yanga. Manji aliona hilo na kwa kuwa ni mfanyabiashara ndiyo maana alitaka abadilishe aina ya uendeshaji wa klabu.
Bahati mbaya halikutimia, kilichotokea hayupo na klabu imekuwa ikipepesuka. Wale waliokuwa wakimpinga na kuona anakosea nao wameingia mitini.
Siyo kwamba wanaojifanya wajuaji wa mambo ya Yanga hawajui umuhimu wa muwekezaji, wanajua lakini kwa kuwa wanataka maslahi yao binafsi ndiyo maana kumekuwa na ugumu wa kujitokeza mtu mwingine kuwekeza klabuni hapo.
Inavyoonekana kuna aina ya watu ambao kazi yao wao ni kupinga maendeleo na wanataka klabu ibaki kuendelea kulia njaa huku wao wakifaidika, wanajua ukianza kutumika mfumo mpya wa uendeshaji basi itakula kwao.
Wakati Yanga wakiiteua ile kamati ya kina Abass Tarimba nilijua kuna kazi kubwa. Kwa akili ya kawaida tu jiulize, wakati kamati hiyo ikiteuliwa kufanya kazi kwa muda nini majukumu ya kamati ya utendaji.
Moja kwa moja kwa aina ya uongozi wa Kibongo wa kupenda sifa ilikuwa ngumu pande mbili kufanya kazi moja huku kila upande ukitaka kuonekana upo juu.
Kinachoiangusha Yanga hadi sasa ni kuwa kuna wajuaji wengi wa mambo, tena asilimia kubwa huwezi kuwaona kwenye ‘media’, wao wanajiita watu wa ndani, kwa mwendo ulivyo kunahitajika mtu au watu wenye maamuzi magumu kubadili upepo, la sivyo hali inaweza kuendelea kuwa mbaya zaidi.
TFF wenye ‘akili’ ni wachache Wiki jana nilieleza jinsi upepo ulivyoanza kwenda kombo ndani ya taasisi hiyo inayoongozwa na Wallace Karia.
Niligusia mambo kadhaa ikiwemo ucheleweshwaji wa kutolewa kwa ratiba ya msimu, uhusiano wao na waandishi wa habari katika baadhi ya mambo, kuondoka kwa Kim Poulsen, kukosekana kwa kocha wa Taifa Stars na mengine kadhaa.
Baada ya kusema hayo, hoja ya majaaliwa ya soka la vijana baada ya kuondoka kwa Poulsen sijajua itakuwaje, siyo kwamba hakuna kocha mwingine anayeweza kubeba mamlaka hayo, lakini kwa kuwa Tanzania tutakuwa mwenyeji wa michuano ijayo ya Afcon U-17 mwakani, ni vema tukawa na mwelekeo mzuri wa nini tunatakiwa kufanya mapema.
Mara likaibuka suala la TFF kumuondoa Clement Sanga katika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi kwa kile kilichoelezwa kupata barua kutoka Yanga, ukijiuliza siku zote walikuwa wapi na kwa nini maamuzi hayo yaje wakati huu! Inatafakarisha.
Karia anaweza kuibuka na hoja kuwa wao TFF wamepokea barua kutoka Yanga kuhusu kumtambua Manji kuwa bado ni mwenyekiti wao, inamaana siku zote hawakujua kama Sanga anakaimu? Nani alishughulikia barua ya Manji kujiuzulu pale TFF na walitoa majibu gani kwa Yanga?
Tunaelekea kuanza msimu mpya, timu za ligi kuu zipo 20, hadi leo mdhamini bado hajajulikana wanasema wapo katika mazungumzo na Vodacom, nini mipango ya klabu na TFF kwa jumla hadi sasa ambapo wanatarajia kutangaza ratiba huku mdhamini akiwa hajulikani.
Wakati timu zikiwa 16 kulikuwa na malalamiko kadhaa ya chinichini kuhusu mambo kadhaa ya kifedha kwa klabu, leo hii timu zipo 20, mdhamini hajajulikana, hizo bajeti za klabu zitapangwaje, ratiba zao zitakuwaje kama hawajui kiasi cha fedha watakachokuwa nacho mkononi!
Kwa mwenendo huu unavyoenda ni kama vile wale wenye ‘akili’ yaani wanaojua nini kifanyike ni wachache kuliko wengine wengi waliopo nje ya ngazi za juu au waliopo nje ya taasisi hiyo.
Comments are closed.