The House of Favourite Newspapers

KIKWETE KUMWAKILISHA JPM SHEREHE ZA KUAPISHWA RAIS WA ZIMBABEWE

Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akipanda ndege ya Rais tayari kuelekea mjini Harare, Zimbabwe, kumuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwenye kwenye sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule wa nchi hiyo Mhe. Emmerson Dambudzo Mnangagwa zinazofanyika leo Jumapili Agosti 26, 2018
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Ndg. Philip Mangula akiwa na Mwenyekiti wa United Democratic Party (UDP) Ndg. John Momose Cheyo wakiwa ndani ya ndege ya Rais kabla ya kuondoka kuelekea mjini Harare, Zimbabwe, kwenye sherehe za kuapishwa kwa Rais mpya wa nchi hiyo Mhe. Emmerson Dambudzo Mnangagwa zinazofanyika leo Jumapili Agosti 26, 2018. Katika safari hiyo viongozi hao wanafuatana na Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (hayupo pichani) ambaye atamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini asubuhi hii kuelekea Harare nchini Zimbabwe ambapo anakwenda Kumuwakilisha  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwenye  Sherehe za kuapishwa Rais Mteule wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe.Emmerson Mnangagwa zinazofanyika leo tarehe 26 Agosti, 2018 katika uwanja wa michezo waTaifa Mjini Harare.

Akizungumza kabla ya kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam,  Mhe.Rais Mstaafu  Kikwete ambaye amefuatana na  Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (Bara) Ndg. Philip Mangula na Mwenyekiti wa Chama cha UDP Ndg. John Cheyo , amesema Tanzania na Zimbabwe zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu  wa kindugu kwani katika kipindi ambacho Zimbabwe ilikuwa ikidai uhuru, baadhi ya wananchi wake  waliwahi kuishi nchini Tanzania, husasani wanachama wa Chama cha ZANU PF, na kupata mafunzo hapa nchini.

‘’Baadhi ya wanajeshi wetu wameshiriki pamoja na wanajeshi wa Zimbabwe katika harakati za ukombozi wa Zimbabwe na ndio maana kwenye Jeshi letu kuna medani ya Zimbabwe’’ amesema Rais Mstaafu Kikwete.

Rais Mnangagwa anaapishwa leo kuongoza taifa la Zimbabwe baada ya kushinda katika uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika tarehe 30 Julai, 2018

Imetolewa na: Jaffar Haniu

Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

26 Agosti, 2018

Comments are closed.