The House of Favourite Newspapers

Waarab Wamfuata Makambo Yanga

Mshambuliaji wa Yanga Mkongomani, Heritier Makambo.

 

SIKU za mshambuliaji wa Yanga Mkongomani, Heritier Makambo za kuendelea kubaki kukipiga Jangwani huenda zikawa zinahesabika baada ya baadhi za klabu za nje ya nchi kupiga hodi kuwania saini yake.

Makambo ni kati ya wachezaji waliosajiliwa na Yanga msimu huu wa Ligi Kuu Bara baada ya kocha mkuu wa timu hiyo raia wa DR Congo, Mwinyi Zahera kumpendekeza kutokana na kuvutiwa naye kwenye majaribio.

Mshambuliaji huyo hadi hivi sasa tayari amefunga mabao nane tangu ajiunge na Yanga kati ya hao mawili ya mashindano na mengine sita katika michezo ya kirafiki.


Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, tayari mawakala watano kutoka kwenye nchi tatu za Uarabuni na mbili za Ulaya ikiwemo Sweden na Norway wameshaonyesha nia ya kumtaka mchezaji huyo.
Mtoa taarifa huyo alisema, mawakala hao wamemfuata mchezaji huyo na kuwapa maelekezo ya kuzungumza na viongozi kabla ya kumfuata yeye kutokana na kubanwa na mkataba wa miaka miwili ya kuichezea Yanga.

 

“Uwezekano wa Makambo wa kudumu kwa kipindi kirefu kuendelea kuichezea Yanga ni mdogo sana ni baada ya baadhi za klabu kutoka nje ya nchi zikiwemo za Uarabuni na Ulaya kuonyesha nia ya kumsajili.
“Huo mkataba wenyewe wa miaka miwili aliosaini Yanga sijui kama ataumaliza kutokana na yeye mwenyewe ndoto alizoziweka za kupiga hesabu ya kucheza soka Ulaya.”

 

Alipotafutwa Makambo kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Mimi ni mchezaji mwenye ndoto nyingi ikiwemo ya kucheza soka la kulipwa ambayo ni lazima niitimize nikiwa Yanga.
“Zipo baadhi za klabu zinaonyesha nia ya kunihitaji kwa kunipa ofa kutoka nje ya nchi ambazo nimewaambia nina mkataba na Yanga, hivyo vema zikafanya mazungumzo nao kabla ya kuja kwangu,” alisema Makambo aliyeibuka kuwa kipenzi cha Yanga.

Halima Mdee Alivyowavuruga Mawaziri Wa Zamani Wa JK

Comments are closed.