The House of Favourite Newspapers

WAKULIMA WAKUBALI KUANZA KUUZA KOROSHO KWA BEI ISIYOPUNGUA 3000

Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye mnada wanne wa msimu wa uuzaji korosho 2018/2019.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye mnada wanne wa msimu wa uuzaji korosho 2018/2019 wakimsikiliza kwa makini waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba.

 

Wakulima wa zao la korosho wa Wilaya ya Tandahimba na Masasi wamekubali kuuza korosho zao mbele ya Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) kutokana na kuridhia na kukubaliana na maamuzi ya serikali.

Hayo yamejili katika mnada wa nne wa msimu wa uuzaji korosho 2018/2019 uliojumuisha kampuni za ununuzi 11 katika maghala tofauti uliofanyika katika kijiji na kata ya Mdimba Mkoani Mtwara.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji na kata ya Mdimba, Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba alisema kuwa bei ya zao la korosho imeonyesha mwelekeo wa kushuka katika mwaka 2018/2019 tofauti na hali ilivyokuwa katika msimu wa mwaka 2017/2018 ambapo bei ya zao hilo ilifikia shilindi 4,128

Katika mkutano huo wakulima wa korosho walikubali mbele ya waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Tizeba kuanza kuuza korosho zao kwa bei ya juu ya shilingi 3,016 huku bei ya chini ikiwa ni shilingi 3000.

“Wafanyabiashara wasipangiwe muda wa kuchukua korosho ghalani kwa ajili ya usafirishaji na wasipangiwe kutumia bandari gani, wawe huru kulingana na maagizo yaliyotolewa na Rais Magufuli’’

“Nitashangaa sana kuona mnunuzi mwenye akili timamu akitoa barua na kutaka kuuziwa korosho chini ya shilingi 3,000 au akitaka kwa shilingi 2,500” Alikaririwa Dkt Tizeba.

 

Kufuatia hali hiyo tarehe 26 Octoba 2018 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa alitangaza maamuzi ya serikali kusimamisha minada yote hadi suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi.

 

Kufuatia uamuzi huo tarehe 28 Octoba 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli alikutano na wanunuzi wa zao la korosho katika mkutano uliokuwa ukiendelea kati ya wanunuzi hao na Waziri Mkuu na kutoa msimamo wa serikali kuhusu zao hilo kufuatia kuwepo kwa mvutano wa bei ya zao hilo kati ya wanunuzi na wakulima.

 

Katika mnada huo wa nne uliohudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe Gelasius Gasper Byakanwa, Waziri wa kilimo Dkt Tizeba alisema kuwa matokeo ya mnada huo hayakuwa mabaya ukilinganisha na minada iliyopita katika msimu huu wa 2018/2019 ambapo bei ilishuka.

 

Alisema baada ya Rais Magufuli kutangaza msimamo wa serikali kuwa bei ya kiwango cha chini ya mnadani katika msimu wa 2018/2019 kuwa shilingi 3000 kwa kilo moja ya korosho, wafanyabiashara wameitikia wito kwa kuweka bei nzuri mnadani.

 

 

Aidha, Waziri wa kilimo alisema kuwa katika vikao vingi vya serikali vilivyotuama kujadili mwenendo wa zao hilo kwa mujibu wa kifungu cha 8 cha sheria ya Tasnia ya Korosho Na 18 ya mwaka 2018 ameielekeza Bodi ya korosho kupata kibali cha waziri wa kilimo na waziri mkuu kabla ya kuyafanyia maamuzi.

 

Alisisitiza kuwa mnunuzi akishalipa ushuru katika Halmashauri moja hapaswi kudaiwa kulipa ushuru huo katika Halmashauri nyingine, Bodi kutotoa bei elekezi, Tozo ya Bodi ya korosho ambayo iliongezwa kwa msimu wa mwaka 2018/2019 kufikia shilingi 17 kwa kilo irudi shilingi 10 kwa kilo kama ilivyotozwa msimu wa 2017/2018.

 

Wanunuzi wa korosho wana hiari ya kusafirisha korosho kwenda nje ya nchi kupitia bandari ya mtwara, Dar es salaam au Tanga huku wanunuzi wakiruhusiwa kwenda na magunia yao kununua korosho ya wakulima, Bodi ya korosho kuangalia utaratibu wa wabanguaji wadogo kupata/kununua korosho katika mfumo wa mnada, sambamba na dhamana ya mnada (Bill Security) kupungua.

 

Dkt Tizeba alisema kuwa baada ya maelekezo ya serikali kuhusu mwenendo wa zao la Korosho katika hatua ya kwanza ya utekelezaji Wizara yake ilianza kutathmini kuhusu mfumo mzima wa uuzaji wa korosho hatimaye kufikia uamuzi huo.

 

Aliwasisitiza wakulima kutokata tamaa na minada kwani ni kawaida kwa bei za mazao kupanda na kushuka kulingana na uzalishaji katika nchi zingine pamoja na soko la Dunia.

 

(Picha Zote Na Mathias Canal, WK)

Comments are closed.