The House of Favourite Newspapers

Yondani Arejea Yanga, Akanusha Kugoma

Nahodha wa Yanga, Kelvin Yondani

BEKI mkongwe na nahodha wa Yanga, Kelvin Yondani jana aliripoti kwenye mazoezi ya timu hiyo na kukanusha taarifa zilizozagaa kuwa ameigomea timu hiyo.

 

Mchezaji huyo wa zamani wa Simba, hivi karibuni mara baada ya kutua nchini akitokea Lesotho kucheza mchezo wa kufuzu Afcon, hakuungana na msafara wa Yanga uliokwenda kucheza michezo miwili ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mwadui FC, Shinyanga na Kagera Sugar.

 

Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera aliliambia Spoti Xtra linalotoka kila Alhamisi na Jumapili kuwa, wachezaji hao wameigomea timu hiyo kutokana na kudai malimbikizo ya fedha zao.

 

Lakini Yondani mwenye alisema jana kuwa Wanayanga wazipuuze taarifa za yeye kugomea kucheza mechi huku akisema kuwa alishindwa kuungana na timu hiyo kutokana na kusumbuliwa na majeraha.

 

Yondani alikiri kuidai Yanga lakini akasema kuwa hajagoma kama taarifa zinavyoenea na anashukuru jana asubuhi aliripoti kwenye mazoezini yaliyofanyika Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini jijini Dar es Salaam na kuzungumza na Zahera na Daktari Mkuu wa timu, Edward Bavu.

 

“Ilikuwa ngumu kwangu mimi kusafiri na timu nikiwa nina majeraha na isitoshe mazingira mabaya ya viwanja hivyo tulivyokuwa tunakwenda kuvichezea mechi ni lazima ningejitonesha na kusababisha majeraha kuwa makubwa zaidi.

 

“Siwazuii watu kuongea, waache waongee tu lakini ukweli ninaujua na sababu iliyonifanya nishindwe kusafiri na timu kanda ya ziwa, mimi nilijitonyesha enka nikiwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa lakini nashukuru hivi sasa naendelea vizuri baada ya kuanza matibabu.

 

“Nikiri ni kweli kabisa mimi ninawadai Yanga, lakini sijagoma na unanijua vizuri jinsi ninavyokuwa nikiwa ninadai haki yangu na ningekuwa nimegoma, basi nisingetokea mazoezini leo (jana), hivyo niwaondoe hofu mashabiki wa Yanga.

 

“Kama Mungu akipenda nitakuwepo kwenye mchezo ujao wa ligi kama maendeleo yangu yakiwa mazuri, lakini ninaamini huu ndiyo muda muafaka wa wadogo zangu akina Ninja (Juma Shaibu) nao kuonekana kwania wana uwezo wazuri,” alisema Yondani.

STORI: SAID ALLY NA MARTHA MBOMA KHADIJA MNGWAI

Comments are closed.