The House of Favourite Newspapers

Kesi ya ‘Uchochezi’ Inayomkabili Zitto Kabwe Yaahirishwa

 

Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (kushoto).

 

MAHAKAMA  ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imekwama kuanza kusikiliza ushahidi wa kesi ya uchochezi inayomkabili, kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe,  kwa sababu shahidi amepata dharura.

 

Kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, lakini Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga amesema shahidi amepata dharura.

 

Katuga ameieleza mahakama kuwa walipanga kuwa na shahidi lakini kwa bahati mbaya amepata matatizo ya kifamilia, hivyo aliomba ahirisho fupi.

 

Baada ya kueleza hayo, wakili wa Zitto, Jebrah Kambole,  aliiomba mahakama iahirishe kesi hiyo hadi Februari 27 mwaka huu, akisema mtuhumiwa alijipanga kusikiliza kesi hiyo licha ya kuwa anakabiliwa na majukumu mengine.

 

Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 27, mwaka huu.

Zitto alifikishwa Mahakama ya Kisutu kwa mara ya kwanza, Novemba 2, 2018 kujibu mashtaka matatu ya uchochezi katika kesi ya jinai namba 327/2018.

Katika kesi ya msingi, Zitto anadaiwa kutenda makosa hayo, Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT-Wazalendo.

Katika shtaka la kwanza, inadaiwa kuwa siku hiyo,  kwa nia ya kuleta chuki miongoni mwa wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la Polisi alitoa maneno ya uchochezi.

Inadaiwa kuwa maneno hayo yalikuwa ni uchochezi na yenye kuleta hisia za hofu na chuki.

HABARI NA DENIS MTIMA | GPL

Comments are closed.