The House of Favourite Newspapers

Mbelgiji wa Simba amuota straika Mbenin

Patrick Aussems

KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems, amesema bado anahitaji huduma ya mshambuliaji, Sadney Urikhob raia wa Benin kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

 

Mshambuliaji huyo hivi karibuni alitua nchini kwa ajili ya majaribio ya kuichezea timu hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kurejea nyumbani kwao kutokana na kanuni za usajili za Caf kumzuia kusaini Simba.

 

Mbenin huyo alikuwepo kwenye sehemu ya kikosi cha timu hiyo kilichoshiriki michuano ya SportPesa Super Cup, iliyofanyika hivi karibuni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Aussems alisema tayari ameanza maandalizi ya kukisuka kikosi chake kipya atakachokitumia kwa ajili ya msimu ujao wa ligi huku jina la Mbenin likiwa la kwanza kwenye orodha yake.

 

“Nipo kwenye mipango thabiti ya kukiimarisha kikosi changu katika kuelekea msimu ujao wa ligi, kama unakumbuka walikuwepo baadhi ya wachezaji waliokuja na wengine niliowaleta kwa ajili ya kuwaongeza katika usajili wa Caf.

 

“Kati ya hao yupo yule mshambuliaji raia wa Benin ambaye nilimleta mimi kwa ajili ya kumfanyia majaribio na lengo ni kuwaonyesha viongozi baada ya mimi kuridhishwa na kiwango chake kutokana na kumfahamu.

 

“Alicheza mechi moja ya SportPesa Super Cup na akafanya mazoezi kwa siku mbili, lakini baada ya hapo alirudi kwao na mimi ndiyo niliyemwambia arudi kutokana na kanuni za usajili wa Caf kutubana ilitakiwa kwanza acheze ligi kabla ya kucheza michuano hii mikubwa Afrika,” alisema Aussems.

STORI; Wilbert Molandi

Comments are closed.