The House of Favourite Newspapers

MABINTI WANAHADAIKA NA PETE ZA UCHUMBA

WEWE msomaji wa Boyfriend and Girlfriend ni kiungo muhimu sana katika maisha yangu. Hebu fikiria, vipi kama nitaandika tu halafu hakuna wa kusoma? Nadhani yote yasingekuwa na maana, lakini kwa sababu unasoma na nina uhakika huo, basi acha nijivunie. 

 

Rafiki zangu, leo tutajifunza kitu kipya kabisa. Naamini utabadili namna ya kufikiri mara mada hii itapofika ukingoni. Nazungumzia kuhusu pete za uchumba. Hizi zimekuwa maarufu sana katika jamii yetu siku hizi. Watu wanakutana disko, wiki mbili baadaye wanavalishana pete!

 

Tayari ameshachumbiwa na amekuwa chini ya miliki ya mtu. Uko wapi usahihi wa pete za uchumba? Vijana wamechanganyikiwa kwelikweli! Wanataka pete tu!

 

Inawezekana wewe msichana unayesoma mada hii sasa hivi umevaa pete ya uchumba au pengine uko njiani kuvalishwa… vizuri! Lakini unaelewa nini kuhusu pete ya uchumba?

 

Unautumiaje uchumba wako na mpenzi wako? Hii ndiyo safu pekee, ndiyo mahali utakapoweza kutolewa matongotongo kuhusu suala la pete. Nikuambie kitu? Usiniache please, twende pamoja tuone ukweli.

NI NINI HASA?

Linatokana na neno la Kingereza linaloandikwa engagement ring lenye maana nyingine ya commitment ring. Kwa Kiswahili rahisi ni pete ya ahadi. Msichana kuvalishwa pete ya uchumba, maana yake amevalishwa alama ya ahadi. Jambo moja unatakiwa kusafiri nalo hapa ni kwamba, ahadi inaweza kutekelezwa au isitekelezwe. Ni uamuzi wa mtoa ahadi.

 

KUHALALISHA PENZI

Awali kulikuwa hakuna kabisa utaratibu huu wa pete za uchumba. Mvulana akimpenda msichana, taratibu za kawaida zilifuatwa kwa maana ya posa na baadaye mahari kisha ndoa. Hizi ni tabia za Kimagharibi ambazo zimekuja hivi karibuni.

 

Utaratibu huu umepokelewa vibaya (hasa na wasichana), wengi wamekuwa na shauku sana pete. Imani yao ni kwamba ukivalishwa tu, basi ndoa inanukia. Akipata mpenzi, anamlazimisha amvalishe pete.

 

Kwani kazi basi?! Aaah wapi! Jamaa anakwenda zake kwa sonara anatengeneza pete ya laki tatu anamvalisha baa!

 

Tayari wachumba! Hakuna mzazi wala mjomba anayejua. Hapo sasa ndiyo kwenye ukichaa – mwanamke atajiachia vyovyote atakavyo mwanaume huyo. Wanaume nao wanashangilia. Tatizo si pete?

Anakuvalisha halafu anakutumia kwa nafasi, akiridhika anakuacha tena wengine huchukua na pete zao kabisa, halafu anatafuta mwingine anamvalisha. Mchezo unaendelea.

UCHUMBA SI NDOA

Dada zangu wapendwa fumbukeni macho, uchumba si ndoa. Utakuta mwanamke amevalishwa pete ya uchumba, basi kashakuwa mke. Atakwenda kwa huyo mwanaume, atafanya usafi, atafua, atapika na penzi atatoa!

 

Mwanaume anaridhishwa na kila kitu. Hapo unakuwa huna jipya tena. Hata kama anakupenda kiasi gani, hawezi kuwa na haraka ya ndoa, maana kila kitu anachotakiwa kupata mwanandoa unampa!

 

Ya nini ajisumbue? Ya nini aanze kufikiria mambo ya vikao? Presha za nini? Haoni sababu na wakati muda ukizidi kwenda, anaendelea kukuchoka na kutafuta mwingine anayejitambua na kumuoa. Una lipi jipya utakalomwonesha ndani ya ndoa wakati kila kitu tayari anakijua?

 

Mabinti muwe makini. Kwa bahati mbaya sana, siku hizi wanaume wanakimbia kuoa mapema, ukijirahisi kwa pete utazivaa sana, lakini si ile ya madhabahuni. Utatumika na kuachwa.

 

Usikose sehemu ya mwisho ya mada hii wiki ijayo.  Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa vinavyopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

Comments are closed.