The House of Favourite Newspapers

Man City Out UEFA, LIVERPOOL VS BARCA NUSU FAINALI UEFA

LIVERPOOL itaivaa Barcelona na nyota wake Lionel Messi kwenye mtanange wa aina yake wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuitoa Porto kwa jumla ya mabao 6-1 kwenye robo fainali ya michuano hiyo.

Wakati Tottenham Hotspur itakabiliana na Ajax Amsterdam kwenye mechi nyingine ya nusu fainali baada ya kuitupa nje Manchester City kwa sheria ya goli la ugenini baada ya timu hizo kufungana jumla ya mabao 4-4.

 

Mechi za kwanza za nusu fainali zinatazamiwa kupigwa Aprili 30, mwaka huu wakati zile za marudiano zitafanyika Mei 7.

 

Fainali ya mwaka huu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itapigwa Juni 1 kwenye Uwanja wa Wanda Metropolitano jijini Madrid nchini Hispania. Mechi kati ya Liverpool na Barcelona inatazamiwa kuwa gumzo na ya kihistoria kutokana na rekodi ya timu hizo ambazo zote zimetwaa taji la Ligi ya
Mabingwa Ulaya mara tano.

Liverpool ilisonga mbele kwa jumla ya mabao 6-1 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Porto nchini Ureno jana. Liverpool ilishinda mchezo wa kwanza mabao 2-0 wakati timu hizo zilipokabiliana kwenye mechi ya kwanza ya robo fainali, wiki iliyopita.

 

Mane ndio alipachika bao la kuongoza la Liverpool katika dakika ya 26 wakati Mohamed Salah aliongeza bao la pili katika dakika ya 65 na Eder Militao alipachika bao la kufutia machozi la Porto mnamo dakika ya 69 kwenye mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Estadio de Dragao nchini Ureno.

 

Huku mabao mengine ya Liverpool yakipachikwa na Firmino mnamo dakika ya 77 na jingine likifungwa na Virgil van Dijk kwenye dakika ya 84.

City ilitupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Tottenham Hotspur kwenye mechi kali ya marudiano ya robo fainali iliyopigwa jana kwenye Uwanja wa Etihad.

 

Tottenham imesonga mbele kwa sheria ya goli la ugenini baada ya timu hizo kuwa zimefungana jumla ya mabao 4-4 kutokana na kushinda mchezo wa kwanza bao 1-0 walipocheza wiki iliyopita kwenye Uwanja wa White Hart Lane. Manchester City ilianza kwa kasi mchezo huo na kupata bao la mapema dakika ya nne likipachikwa na Raheem Sterling na alifunga bao jingine dakika ya 21.

Mabao mengine ya City yalipachikwa na Bernado Siva na Sergio Aguero wakati yale ya Spurs yakipachikwa na Heung-Min Song mawili na Fernando Llorente.

Comments are closed.