The House of Favourite Newspapers

SIKU CHACHE BAADA YA UCHAGUZI…BILIONEA MPYA AIBUKA YANGA

BILIONEA maarufu hapa nchini, Rostam Azizi imeelezwa kuwa amekusudia kuisaidia Yanga kwa kuipa misaada ya kifedha pale inapowezekana.

 

Hii inakuja siku chache tu baada ya Yanga kufanya uchaguzi na kupata viongozi wapya chini ya mwenyekiti, Dk Mshindo Msolla na makamu wake, Frederick Mwakalebela aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

 

Rostam amekuwa akitajwa mara nyingi na baadhi ya wadau wa soka kuwa anatarajia kuwekeza ndani ya Klabu ya Yanga baada ya kuondoka aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji.

 

Klabu ya Yanga kwa sasa ipo katika mikakati ya kuboresha kikosi chake ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ndani ya klabu hiyo ili kuifanya timu hiyo iwe ya kisasa zaidi, ikiwemo suala zima la usajili.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Katibu wa Rostam, Abbas Gulamali (huyu ni mtu mwingine, siyo yule marehemu), amesema kuwa, bilionea huyo alikuwa na mpango wa kuwekeza ndani ya klabu hiyo lakini muingiliano wa watu wengi uliojitokeza ndani ya klabu ndiyo uliosababisha kumrudisha nyuma.

“Kweli Rostam alikuwa anahitaka kuwekeza ndani ya Klabu ya Yanga, lakini aliamua kuachana na suala hilo baada ya kuona kuna muingiliano wa watu wengi, hivyo ameamua kukaa pembeni.

 

“Lakini atakuwa anatoa misaada kama kawaida watakayokuwa wakiihitaji Yanga, hakutakuwa na shida yoyote, na yeye ni mwanachama halali wa Klabu ya Yanga,” alisema Gulamali.

 

Tangu kuondoka kwa Manji kumekuwa na anguko kubwa la kiuchumi ndani ya Yanga hadi kufikia hatua ya kuanza kutembeza bakuli lakini inaonekana uongozi mpya uliochaguliwa Jumapili iliyopita, umekuja na neema.

 

Kwa mamilioni ya msaada ambayo Rostam anatarajiwa kuyatoa kwa Yanga, inawezekana kabisa ukawa ni mwisho wa Yanga kujiendesha kwa mtindo wa kutembeza bakuli.

 

Rostam Novemba 2018 aliweka wazi mbele ya Rais John Pombe Magufuli kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa Yanga.

 

Rostam ni bilionea mwenye mchango mkubwa sana katika michezo na mambo yake mengi amekuwa akiyafanya kimyakimya bila kutaka kujulikana.

Stori: Khadija Mngwai

Comments are closed.