The House of Favourite Newspapers

Simba Vs Azam Taifa, Lazima Mpigwe

Simba wakijiwinda.

azam

Na Mwaandishi Wetu, CHAMPIONI

KATIKA usajili wa dirisha dogo uliopita, Azam FC ilitumia Sh milioni 509 kuwasajili wachezaji saba, sasa klabu hiyo imesema ni lazima wachezaji hao waisaidie kupata ushindi dhidi ya Simba leo Jumamosi. Simba inakutana na Azam kwa mara ya 18 katika Ligi Kuu Bara leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa mara ya kwanza zilikutana Oktoba 4, mwaka 2008 ambapo Azam ilishinda mabao 2-0.

Tangu wakati huo, Simba na Azam zimekutana mara 17 ambapo Simba ilishinda mechi nane, Azam ikashinda nne na zimetoka sare tano, pia mabao 42 yamepatikana katika mechi hizo 17. Kabla ya mchezo wa leo, Kocha Msaidizi wa Azam, Idd Nassor ‘Cheche’, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, anaamini usajili wao wa dirisha dogo, ukichanganya na wachezaji waliopo tangu zamani utawasaidia kuifunga Simba leo.

“Tunajua Simba ni timu nzuri, lakini sisi tunataka kuendeleza ushindi kwao tangu tuwafunge kwenye Kombe la Mapinduzi na vijana wangu wana hamu ya ushindi. “Hii morali ya ushindi hatutaki kuipoteza na tunadhani inatuongezea kujiamini katika michezo ya ligi hii, najua ni mechi ngumu kwetu lakini nawaamini vijana wetu wanaweza kupambana,” alisema Cheche.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Azam, Jaffar Idd, Cheche atalazimika kukaa katika benchi la Azam kwani kocha mpya wa timu hiyo, Aristica Cioaba raia wa Romania bado hajapata kibali cha kufanya kazi nchini. Cheche leo ataiongoza Azam katika mechi yake ya nane kama kocha mkuu tangu mwishoni mwa Desemba mwaka jana alipokabidhiwa timu baada ya kabu hiyo kumfuta kazi Kocha Zeben Hernandez raia wa Hispania.

Katika mechi hizo nane, Cheche ameshinda sita na kutoka sare mbili, miongoni mwa mechi alizoshinda ni ile ya hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi alipoifunga Yanga mabao 4-0 halafu katika fainali aliifunga Simba bao 1-0. KIKOSI CHA SH MILIONI 500 Katika usajili mdogo uliopita Azam ilisajiliwa wachezaji saba huku mmoja ikianza kumtumia baada ya kumsajili awali, gharama za kuwasajili wachezaji hao ni Sh milioni 509.6.

Wachezaji hao ni Yakubu Mohammed (Aduana Stars dola 30,000 sawa na Sh milioni 65.4), Stephan Kingue Mpondo (Coton Sports- Cameroon, dola 30,000),  Enock Atta Agyei (Medeama alisajiliwa kwa dola 50,000 sawa na Sh milioni 109), Yahaya Mohammed (Aduana Stars, dola 30,000), Samuel Afful (Sekondi Hasaacas dola 30,000), Daniel Amoah (Medeama, dola 50,000) na mzawa Joseph Mahundi aliyetokea Mbeya City ambaye alisajiliwa kwa dau la Sh milioni 30.

KAPOMBE, SURE BOY HATIHATI

Kwa mujibu wa Cheche, katika mchezo wa leo timu yake ipo kwenye hatari ya kuwakosa wachezaji Shomari Kapombe na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambao afya zao hazipo sawa. Cheche alisema Kapombe na Sure Boy walikuwa majeruhi hadi jana ambapo walikuwa wanasubiria jibu la mwisho la daktari kujua iwapo atawatumia au la kutokana na maendeleo ya afya zao.

“Leo (jana) tumefanya mazoezi ya mwisho ya kujiandaa na mchezo huo kila mchezaji anaonyesha kuwa na morali ya hali ya juu kuelekea mchezo huu ambao tumepanga kushinda. “Tuna majeruhi wawili ambao ni Sure Boy anayeumwa fangasi mguuni pamoja na Kapombe ambaye anasumbuliwa na malaria na wote wanaendelea na matibabu, tunasubiri taarifa ya daktari leo (jana) jioni ili kuweza kujua iwapo watakuwa fiti kucheza ama la,” alisema Cheche. Cheche alisema wachezaji wengine wote akiwemo Himid Mao aliyefunga bao pekee la Azam katika mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi, wapo fiti na wanasubiri mchezo huo. Himid alifunga bao hilo dakika ya 13 kwa shuti kali la moja kwa moja akiwa nje ya eneo la hatari.

OMOG ATAMBA SIMBA

Kuelekea mchezo wa leo, Kocha wa Simba, Joseph Omog alisema hana hofu hata kidogo kwenye mechi dhidi ya Azam kwani anaamini anakutana na timu moja kati ya zile 15 wanazopambana nazo kwenye ligi. Omog ambaye katika mchezo wa kwanza kwenye ligi msimu huu Septemba 17, mwaka jana, kikosi chake kilishinda bao 1-0 lililofungwa na Shiza Kichuya aliliambia Championi Jumamosi kuwa; “Mara ya mwisho walitufunga kwenye Kombe la

Mapinduzi, hatutaki  kurudia makosa yaliyotokea awali. “Mashabiki wana presha na mechi hii lakini mimi naona ni mchezo wa kawaida kama ilivyo michezo mingine, tutapambana ili tuweze kushinda.” Omog alisema anashukuru mastraika wake kikosini wakiwemo Ibrahim Ajib na Laudit Mavugo wameonyesha kurudi katika makali yao hivyo watafanya vizuri leo. “Mastraika wangu wapo vizuri na naamini watafanya vizuri leo, huko nyuma tulitengeneza nafasi nyingi bila kufunga lakini sasa wapo vizuri,” alisema Omog.

BANDA NJE

Wachezaji wa Simba wanaotarajiwa kuukosa mchezo huu ni mabeki wa kati Abdi Banda, Method Mwanjale na kiungo Mohamed Ibrahim ‘MO’. Akizungumza na Championi Jumamosi, Daktari wa Simba, Yassin Gembe alisema Banda ataukosa mchezo huo kutokana na majeraha ya nyonga aliyoyapata kwenye mazoezi ya juzi Alhamisi jioni. Gembe alisema, beki huyo leo (jana) anatarajiwa kupelekwa hospitali kwa ajili ya vipimo zaidi, hiyo ni baada ya kushindwa kufanya mazoezi ya mwisho na wenzake siku moja kabla ya mechi.

Alisema kuwa, Mohamed yeye ataukosa mchezo huo baada ya jana kushindwa kufanya mazoezi kutokana na kujitonesha enka iliyokuwa imemuweka nje ya uwanja kwa muda wa wiki mbili. Aliongeza kuwa, Mwanjale yeye ana asilimia ndogo za kucheza mechi hiyo, baada ya mazoezi ya jana kushindwa kumalizia kufuatia kujitonesha nyonga. “Kama ulivyoona kwenye mazoezi ya leo (juzi Alhamisi) jioni Banda amepata maumivu ya nyonga na kusababisha ashindwe kuendelea na mazoezi na leo (jana) asubuhi tena ameshindwa kabisa kufanya mazoezi na wenzanke,” alisema Gembe.

 Waandishi: Khadija Mngwai, Ibrahim Mussa, Wilbert Molandi.

Comments are closed.