The House of Favourite Newspapers

Insane (Mwendawazimu)-12

ILIPOISHIA

Ukawa mwanzo, wakaanza hivyo. Theo hakutaka kuacha, alichoamua kilikuwa ni kumpoteza kabisa Fabian moyoni mwa msichana huyo. Hiyo, haikuwa kazi nyepesi kwani wakati mwingine alimfurahisha Esther lakini alipopita Fabian, msichana huyo alinyamaza na kumwangalia mwanaume huyo, alitamani kumuongelesha lakini aliamua kunyamaza tu.

“Kuna nini?” aliuliza Theo huku akijua kabisa kilichokuwa kikiendelea.

“Naomba tuondoke hapa!”
“Kwa nini?”
“Nataka kuwa na furaha! Naomba tuondoke hapa,” alisema msichana huyo. Theo hakuwa na jinsi, akakubaliana naye na kuondoka mahali hapo.

SONGA NAYO

Moyo wa Fabian ulikuwa kwenye maumivu makali mno. Hakuamini kama kweli yeye ndiye aliyeamua kumuacha msichana huyo kwa sababu tu alipigiwa simu ya vitisho kutoka kwa mtu ambaye hakuwa akimfahamu.

Usiku hakuwa na raha, hakusoma, alikuwa na mawazo tele na muda mwingi alikuwa akikaa peke yake akisononeka. Alibaki akiziangalia picha za Esther katika simu yake, zilimkumbusha mbali na ndizo ambazo zilimfanya kulia kila wakati.

Siku zikakatika na kumuona Esther akiwa na mwanaume mwingine, Theo. Alimchukia mwanaume huyo kwa kuwa alikuwa na maisha ya kujidai sana, kwake, kula bata na kutembea na wanawake mbalimbali ndiyo ilikuwa furaha yake.

Aliumia moyoni mwake kwani aliona kabisa kwamba Esther alimpata mwanaume ambaye hakuwa sahihi katika maisha yake. Hakutaka kuvumilia, hakutaka kuona akimuacha msichana huyo kiwepesi namna hiyo, alichokifanya ni kuanza kumtafuta.

Baada ya miezi mitatu ya shida na mawazo tele ndipo alipompigia simu. Ilianza kuita lakini haikupokelewa mpaka ilipokata. Hakukata tamaa, akampigia tena na tena na mwisho wa siku kuipoke.

“Unasemaje?” ilisikika sauti ya Esther kwenye simu.

“Naomba nikuone…”
“Kuna nini?”
“Kuzungumza na wewe!”

“Kuniona mimi? Kuzungumza na mimi! Ili iweje?” aliuliza msichana huyo kwenye simu.

“Nakuomba. I want to talk to you, pleaseee…” (tafadhali, nataka kuzungumza nawe) alisema Fabian.

“Sitaki! Naomba uniache…”

“Esther…nakuomba…”

“Nimesema hivi! Naomba uniache, ukinisumbuasumbua, nakublock,” alisema msichana huyo na kukata simu.

Maneno hayo yaliuchoma moyo wa Fabian, hakuamini kilichokuwa kikiendelea, alimpenda sana msichana huyo na hakuwa tayari kumuona akiondoka moja kwa moja mikononi mwake, hakutaka kukubali hata kidogo, alichokifanya ni kuendelea kumuomba nafasi ya kuzungumza naye.

Wakati hayo yakiendelea, huku upande wa pili, Esther alikuwa kwenye mazoezi mazito na Theo, kila siku waliendelea kuwa pamoja huku mwanaume huyo akijitahidi kwa nguvu zote kumpa furaha ambayo aliamini asingeweza kuipata sehemu yoyote ile.

“Esther…”

“Abeee…”

“Nakupenda sana…unajua hilo?” aliuliza Theo.

“Najua. Nakupenda pia kaka yangu!” alisema Esther, Theo akanyong’onyea.

“Sihitaji unipende kama rafiki, ninahitaji unipende kama mpenzi wa maisha yako. Ninakupenda kutoka moyoni mwangu, sipo tayari kukupoteza, umekuja kwangu kipindi kizuri nilichokuwa nikitafuta msichana wa maisha yangu. Esther, ninakupenda mpenzi,” alisema Theo huku akimsogelea msichana huyo pale walipokaa, akaanza kwa kumshikashika mkono.

“Theo…”

“Nipo mpenzi…”
“Naomba unipe muda, bado moyo wangu upo kwenye wakati mgumu sana,” alisema msichana huyo.

“Wakati gani mpenzi?”

“Ninahitaji kujifikiria katika kupanga maamuzi yangu, wanaume nyie mnakuja kwa sura ya upole lakini mtaishia kwa kuwa na sura ya simba,” alisema Esther.

“Hapana Esther! Umeniona tangu siku ya kwanza nilipokuja kwako, sikuja kwa kukutamani tu, nimekuja kwa sababu nahitaji nikufanye mwanamke mwenye furaha kubwa maishani mwako. Ninakupenda, tena zaidi ya unavyofikiria,” alisema Theo.

Hilo halikubadilisha moyo wa msichana huyo, bado alihitaji kuwa peke yake. Ni kweli Theo alimuonyeshea mapenzi ya dhati kutoka moyoni mwake lakini halikumfanya kumkubali na kumpa moyo wake.

Alimkumbuka Fabian, mwanaume huyo alimuwekea chapa ya moto moyoni mwake, hata kama angekuwa na mwanaume yupi, bado moyo wake ulimkumbuka mno Fabian na hakutaka kumtoa kabisa moyoni mwake.

Mwanaume huyo alimsumbua kwa kumpigia simu na kumuomba waonane sehemu lakini hakutaka kuonana naye. Si kwamba hakumpenda, alimpenda na alitamani sana kuwa naye kama zamani lakini hakutaka kuonyesha udhaifu.

Kasi aliyokuwa akirudi nayo Fabian ndiyo iliyompa wakati mgumu Esther kumkubalia Theo, aliendelea kumwambia kwamba alihitaji muda wa kupumzika na wakati ukweli ni kwamba alikuwa akimwangalia Fabian angeishia wapi.

Fabian hakukoma, alipigwa mikwara lakini hilo halikubadilisha msimamo wake, bado alimhitaji msichana huyo. Alikumbuka alvyopigiwa simu na kuambiwa kwamba aachane na msichana huyo vinginevyo angetekwa na kuuawa.

Hakutaka kuogopa tena, kifo kilikuwa sehemu ya maisha yake, kila binadamu ilikuwa ni lazima afe hata kama angekuwa mjanja kiasi gani. Alijitolea, kwa wakati huo alikuwa tayari kwa lolote lile.

Aliendelea kumsumbua msichana huyo mpaka siku ambayo akakubaliwa kuonana naye, alifurahi na hivyo wakapanga ni sehemu gani ilikuwa nzuri kuonana, wakachagua katika Mgahawa wa Brothers uliokuwa Magomeni.

Wakaonania huko, wakakaa na kuzungumza sana, kila mmoja alionekana kumuhitaji mwenzake. Walikumbukana, kwa kile kilichokuwa kimetokea kilionekana kuwa ni jaribu ambalo lilitaka kuliyumbisha penzi lao, jaribu lililotaka kulikomaza penzi lao.

“Sikuamua kukuacha, nilipigiwa simu na kuambiwa kwamba nikuache,” alisema Fabian.

“Nani alikupigia simu?”
“Simjui. Alikuwa mwanaume, aliniambia kwamba wewe ni mpenzi wake, kama ningeendelea kuwa nawe, basi angeniteka na kwenda kuniua msituni,” alijibu Fabian.

“Mwanaume yupi?”

“Namba yake ilipotea, ila aliniambia hivyo. Niliogopa sana na kufanya maamuzi hayo ambayo daima nimekuwa nikiyajutia,” alisema Fabian huku akimwangalia Esther.

“Pole sana mpenzi! Sikujua hilo, nilichanganyikiwa mno, naomba unisamehe kwa maneno yangu makali,” alisema Esther.

“Wala usijali. Nilikusamehe hata kabla ya leo hii!” alisema Fabian huku akionekana mwenye furaha tele.

Walizungumza kwa muda wa saa mbili na ndipo wakaondoka kurudi chuoni. Mapenzi yakaanza upya, ilikuwa ni zaidi ya ilivyokuwa kipindi cha nyuma. Wakasahau kila kitu kilichokuwa kimetokea.

Wakati ukaribu wao ukirudi kama zamani, Theo alikuwa na maumivu makali, hakuamini alichokuwa akikiona, alimpenda sana Esther, alikuwa kwenye harakati za mwisho kumchukua msichana huyo lakini ghafla akarudiana na mpenzi wake wa zamani.

Hilo lilimkasirisha, hakutaka kumtumia meseji za vitisho tena, alichokifanya ni kumfuata Fabian na kuanza kumtukana kwamba alimchukua mpenzi wake. Fabian hakujibu japokuwa alitukaniwa sana wazazi wake, ili kumuonyeshea Theo kwamba hakukasirika, uso wake ukawa na tabasamu pana.

Watu wote waliomsikia Theo akitukana walishangaa, hawakujua kitu gani kilikuwa kikiendelea kwani mwanaume huyo alimfuata ghafla sehemu ya kulia chakula na kuanza kumtukana.

Hapo ndipo Fabian alipogundua kwamba hata ujumbe ule wa simu aliokuwa ametumiwa na mtu asiyemfahamu, alitumiwa na mwanaume huyo.

“Imemaliza?” aliuliza Fabian huku akimwangalia Theo usoni.

“Sijamaliza…”
“Basi endelea kutukana, ukimaliza naomba uondoke,” alisema Fabian huku akivuta chupa yake ya soda na kuendelea kula.

Maneno hayo yalimtia hasira zaidi Theo, aliona kama alidharauliwa, akamsogelea Fabian pale alipokaa na kumnyanyua. Alikuwa na mwili mkubwa hata zaidi ya mwanaume huyo, kilichofuata ni kuanza kumpiga.

Upole wake, ukimya wake ndiyo ulimfanya kutokumshambulia Theo kwani alijua kama angefanya hivyo ilikuwa ni lazima kupigana na yeye kuhusika katika ugomvi huo.

Alipigwa mpaka watu wakagombelezea, damu zilikuwa zikimtoka puani na mdomoni, uso ulivimba, hakuzungumza kitu zaidi ya kulia. Aliumia sana, alipigwa kwa ajili ya Esther, hilo hakujali sana.

Huo haukuwa mwisho, bado Theo aliendelea kumfanyia Fabian vurugu. Kila siku ilikuwa ni lazima kumfuata na kisha kumtukana na pale ilipobidi kumpiga, alifanya hivyo.

Watu walimuogopa kwa sababu walijua kwamba alikuwa mtoto wa tajiri mkubwa ambaye angeweza kumfanya kitu chochote mtu ambaye angemkasirisha mtoto wake wa pekee.

Ugomvi huo uliendelea kwa miezi sita, yalikuwa maisha ya mateso chuoni, kila alipokuwa, Theo alikuwa akimfuata na kumpiga. Chuoni hakukuwa na amani kwake, kila siku alipokuwa akifika, alijificha kwa kumuogopa Theo kwani kila alipomuona, alimtukana kisha kumpiga kama kawaida.

Esther hakutaka kuona hilo likiendelea, alijaribu kumfuata Theo na kumuombea msamaha Fabian lakini hakutaka kukubaliana naye, alimpenda sana msichana huyo, alimthamini mno na kitendo cha kupokonywa tonge mdomoni kilimuumiza mno.

“Esther, unajua ni jinsi gani ninakupenda.”
“Najua…lakini naomba usimfanyie fujo Fabian. Nakuomba…” alisema Esther, alikuwa amepiga magoti mbele ya mvulana huyo.

“Nimsamehe yule. Siwezi. Mapenzi yana nguvu kuliko mauti, nipo tayari kufanya lolote kwa ajili ya kumkomesha. Nimepoteza muda wangu mwingi kwa ajili yako, kwa nini amenipokonya wewe?” aliuliza Theo.

“Basi nipige mimi! Mimi ndiye niliyekuacha…”
“Hapana! Wewe hukutaka kuniacha, yeye ndiye aliyekulaghai kwa maneno yake mpaka kuniacha. Haiwezekani Esther, nitaacha kumfuatilia kama tu utakubali kuwa nami,” alisema Theo.

“Theo! Naomba umsamehe.”
“Upo tayari kuwa na mimi?”
“Siwezi Theo, najua unalifahamu hilo. Ninampenda Fabian, siwezi kuwa na wewe. Naomba unisamehe, siwezi kabisa kuwa na wewe,” alisema msichana huyo huku akilia.

Maneno hayo yalikuwa kama mkuki moyoni mwa Theo, aliumia zaidi na chuki yake dhidi ya Fabian ikaongezeka zaidi. Alimwangalia Esther huku akiuma meno yake kwa ghadhabu kubwa.

Alitetemeka huku kijasho chembamba kikimtoka. Hakukaa mahali hapo, akaondoka, hasira zake zilikuwa kwa Fabian tu. Bado aliamini kwamba yeye ndiye alistahili kuwa na Esther na si mwanaume mwingine.

Akaamua kupanga mipango kwamba ni lazima Fabian atekwe, apelekwe sehemu na kuuawa. Hakutaka kumuona akiendelea kuishi, alitaka kumfuta katika dunia hii na baada ya kumuua, ilikuwa ni lazima amuue na Esther kwani msichana huyo naye alikuwa chanzo cha kumchukia Fabian.

“Ni lazima nimuue, ni lazima nimuue na huyu malaya,” alisema Theo huku akirudi nyumbani kwao. Alikuwa na hasira mno, hakutaka kukubali kuona akishindwa, alidhamiria kumuua mwanaume huyo kisa tu alikuwa na msichana aliyekuwa akimpenda, alijifanya kusahau kwamba kabla ya kuwa na msichana huyo, wawili hao walikuwa pamoja.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Alhamisi hapahapa.

Comments are closed.