The House of Favourite Newspapers

Ukikosea Acha Ubishi, Kubali Kukosolewa

0

Na Gabriel Ng’osha | IJUMAA WIKIENDA| UHUSIANO

MWENYEZI Mungu asante kwa siku hii njema uliyoifanya kwangu na wanadamu wote. Ninaamini kila kinachotokea katika maisha yangu na wewe msomaji wangu ni kwa sababu yalishaandikwa. Kinachofanyika ni kutimiza tu maandiko.

Karibuni wasomaji wangu kwenye somo lingine murua kabisa la kuachana na ubishi pale unapokuwa umemkosea mwenzi wako au umekosea jambo ambalo linaonekana kwa wazi kabisa, lakini wewe kwa sababu ya ubabe na kiburi chako unajifanya kubisha au kukataa kwa makusudi. Ieleweke kuwa kwenye kukosea, kujishusha pekee hakutoshi bila kuomba msamaha.

Nakushangaa wewe mwanaume au mwanamke ambaye hutaki kukosolewa pale unapokosea. Hivi kweli katika dunia ya sasa, kuna mtu ambaye amekamilika kwa asilimia zote? Kama hakuna, kwa nini wewe huamini kama huwa unamkosea mwenza wako?

Acha ubishi, unapokosea kubali kukosolewa ili ujifunze na uwe mume au mke bora kwa familia yako, lakini unapokosa na kukataa kukosolewa tena kwa ubishi au kusudi unakuwa hujamtendea haki mwenza wako, unamfanya aone kama yeye ndiye mwenye makosa siku zote.

Umuhimu wa wapenzi kujishusha kwenye uhusiano wao hasa pale mmojawapo anapokuwa amebaini kuwa amemkosea mwenza wake au amefanya jambo la kuleta mfarakano kwenye uhusiano wao.

Wapenzi wengi wamekuwa wabishi mno kukubali kukosolewa na wenza wao na kwa uchunguzi wa kawaida tu, wanaume ndiyo wanaonekana kuongoza kwa kukataa makosa yao, tena makosa yanayoonekana wazi kabisa.

Kama ulikuwa hujui, unapokosea na kutumia uanaume wako kumgandamiza mpenzi wako ni kutokumtendea haki, ni kumfanya kujiona dhaifu, ni kumuumiza, kumnyanyasa, kumtesa kwa sababu atashindwa kuhoji mambo mengine ya msingi kwa sababu ya nidhamu ya woga ambayo atakuwa ameshajijengea akilini mwake kutokana na tabia yake.

Nikuambie tu msomaji, mwanadamu ameumbwa kukosea na kujirekebisha, lakini unapokosea na kukataa kujirekebisha unakuwa siyo muungwana na hata unaporudia kosa lilelile mara kwa mara, basi una tatizo kubwa ambalo unapaswa kujiuza zaidi.

Unapokuwa mbishi kwenye ukweli haipendezi zaidi ya kuuvunja moyo wa mwenza wako na kumfanya aamini kuwa yuko kwenye uhusiano na wewe kimakosa. Hii ni kwa sababu anaona kama unampelekapeleka unavyotaka wewe.

Mapenzi matamu ni ya wawili kukubaliana, kushauriana, kupendana, kusaidiana na kusameheana mnapokoseana, lakini inapoonekana mmoja ndiye kila siku wa kuomba msamaha tu kwa mwenzake, inakuwa si sawa.

Mpe nafasi mwenza wako, awe huru kukushauri, kukusaidia, kukufariji hasa unapokuwa na mambo magumu ya kiofi si au maisha ya familia.

Kwa nini unataka kumfanya mwenza wako akuone mumewe au mkewe kama ni adui yake wakati mnakula na kujifunika shuka moja? Jiulize kwa mara nyingine na mfanye mwenza au mpenzi wako awe sehemu ya ubavu wako kama ambavyo vitabu vitakatifu vinasema.

Kwa maoni na ushauri tembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Ijumaa Wikienda kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Insta:mimi_na_uhusiano au unaweza kujiunga na M&U WhatsApp kupitia Na. 0679979785.

Leave A Reply