The House of Favourite Newspapers

Ukitaka Uchekwe Mjini, Mgeuze Mkeo Kuwa Pambo la Nyumba!

AWALI ya yote napenda kuwatahadharisha wanaume wanapenda sana kuwaona wake zao wakikaa nyumbani tu bila kujishughulisha na kusema, eti wao ni pambo la nyumba. Nikuhakikishie tu kwamba, endapo utashindwa kumpa uhuru mkeo wa kuchakarika na kutafuta pesa za kuweza kusukuma maisha yenu, hasa kwa hali ilivyo sasa, lazima maisha yawe magumu.

Nimeanza kusema hayo kwa sababu leo nataka kuzugumzia jinsi suala la kazi linavyochukuliwa kama kigezo muhimu kwa walio wengi kabla ya kuoa au kuolewa. Ni jambo la kawaida mwanaume anapomtamkia msichana kwamba anataka kumuoa, swali la kwanza litakuwa je, unafanya kazi gani?

 

Licha ya kwamba mara nyingi wanawake ndiyo wamekuwa wa kwanza kudadisi juu ya hilo, sasa hivi baadhi ya wanaume nao huchunguza kwamba wale ambao wamewapenda wanafanya kazi au hawafanyi?

Kwa hali ilivyo sasa, kazi imekuwa ni kigezo cha msingi sana ili ndoa ziwepo. Hata hivyo, wakati wengine wakijitahidi kutafuta wachumba wanaofanya kazi, wapo wanaume wasiopenda kuoa wanawake wanaofanya kazi huku wakitoa sababu ambazo kwa kiasi kikubwa hazina uzito bali ni imani potofu tu walizonazo.

 

Huko nyuma wanawake walikuwa wakichukuliwa kama mama wa nyumbani tu wasiostahili kufanya kazi nje ya nyumba. Wao walionekana ni viumbe wanaostahili kufanya kazi za nyumbani kama kuosha vyombo, kufua, kupika, kulea watoto na zaidi ya yote kuwastarehesha waume zao.

Dhana hiyo katika kipindi hicho iliwaathiri wanaume wengi na baadhi kujikuta wakikataa kuoa wanawake wanaofanya kazi. Hata ikitokea kumpenda mwanamke anayefanya kazi, atamshauri kuacha ili amuoe.

 

Mawazo hayo mpaka sasa yapo kwani wapo wanaume wasiotaka kuoa wanawake wanaofanya kazi huku kila mtu akitoa sababu zake.

Si hivyo tu, dhana hii pia imewaathiri wanawake walio wengi, baadhi hawataki kabisa kufanya kazi huku wakibweteka, wakiamini wataolewa na wanaume wanaofanya kazi na kuyafurahia maisha.

Mimi siwezi kuingilia uamuzi wa mtu ila ni vizuri tukashauriana katika mambo yenye manufaa kwetu.

 

Ifahamike kwamba, wanawake pia wana haki ya kufanya kazi, hawakuumbwa kwa ajili ya kukaa nyumbani tu na kuwategemea waume zao kwa kila kitu.

Kwa hali ilivyo sasa, wanaume kwanza wamekuwa makini sana kiasi kwamba kabla hawajachukua uamuzi wa kuoa wanahakikisha wana kazi ambayo itawafanya waweze kuendesha maisha vizuri ndani ya familia.

 

Ninaamini hakuna mwanaume anayeweza kudiriki kuoa huku akiwa hana kazi na ikitokea hivyo, basi mwanaume huyo atakuwa na matatizo.

Wapo wanaume ambao, licha ya kuwa na kazi, lakini pia wanapooa mwanamke ambaye hana kazi, hujitahidi kuwatafutia kibarua angalau wasaidiane kuboresha maisha yao.

 

Hata hivyo, wanawake wengi sasa hawataki kabisa kuwa tegemezi kwa waume zao na wamekuwa wakipigania haki sawa hivyo wengi wao wamekuwa wakikataa ile dhana ya mwanamke ni mama wa nyumbani.

Cha kufurahisha ni kwamba, hivi sasa ukiingia kwenye ofisi mbalimbali, utakuta wanawake wengi wakiwa katika nafasi za juu, tena wengine wakiwa mabosi wa wanaume.

 

Lakini sasa, kila kitu kinakuwa na hasara na faida zake. Tunapozungumzia faida za wanandoa wote kufanya kazi, kwanza tunadhihirisha usawa uliopo kati ya mke na mume kwamba, wote wanastahili kufanya kazi na kuchangia katika maendeleo ya familia na ya taifa kwa jumla.

Zaidi ya yote, wanandoa wanaweza kusaidiana katika kuchangia matumizi ya ndani ya familia kutokana na kila mmoja kuwa na kipato. Maisha ya sasa ni kusaidiana na si kumtegemea mmoja, labda ziwepo sababu za msingi za mume kutegemea kipato cha mke au mke kutegemea kipato cha mume.

 

Tunapogeukia katika upande wa pili, tunakutana na hasara ambazo zinaweza kupatikana kwa wawili kuoana wote wakiwa wanafanya kazi.

Utafiti umebaini kuwa, ni wanandoa wachache sana wanaofanya kazi na wanafurahia maisha yao ya ndoa. Baadhi wamekuwa wakishambuliwa na misuguano ya hapa na pale, hali inayosababisha mazingira ya shari ndani ya nyumba.

 

Baadhi ya wanaume wanaeleza kwamba, kuoa mwanamke anayefanya kazi kunaweza kukukosesha heshima ambayo mwanaume anastahili kuipata kutoka kwa mke wake kutokana na kwamba, mwanamke anapokuwa na uwezo wa kupata kila kitu anachotaka bila msaada kutoka kwa mumewe kama ilivyojengeka, inaweza kusababisha kushuka kwa heshima.

 

Cha msingi kwa wanandoa wote ni kufahamu kwamba ndoa ni heshima na ili heshima hiyo idumu milele, lazima kuwepo kwa ushirikiano, uaminifu, maelewano na majukumu kwa kila mtu.

Tukumbuke ndoa siku zote ni makubaliano baina ya wawili waliotokea kupendana. Kwa maana hiyo hata mkioana wote mkiwa hamna kazi ni sawa na hakuna anayeweza kawaingilia.

Amran Kaima, +255 658 798 787.

Comments are closed.