The House of Favourite Newspapers

HUKUMU YA KIFO YA NAURA, RUTH NA SHERIA ZETU

Picha inayohusiana
Ruth Kamande

RUTH Kamande na Naura Hussein wote wamehukumiwa na mahakama kunyongwa hadi kufa kwa kosa la mauaji ya wapenzi wao.

Ruth alimchoma kisu mpenzi wake na kumsababishia mauti huku Naura akiripitiwa pia kumuua mumewe kwa kumchoma visu mara 25. Ukihukumu mapema unaweza kusema ni unyama wa aina yake na kukubaliana na uamuzi wa mahakama kwamba stahiki ya ukatili huo ni kifo.

Lakini leo pamoja na ukatili walioufanya wasichana hao dunia inapiga kilele, inakosoa kwa sauti kubwa uamuzi wa mahakama; inalazimisha jicho la tatu litazame upya hukumu hiyo. Shirika la Kutetea Haki za Binadamu Ulimwengu (Amnesty International- AI) na washirika wake, hivi karibuni waliungana kumtetea Naura raia wa Sudan kumuokoa katika kitanzi.

Wakili wa msichana huyo mwenye umri wa miaka 19, Abdelaha Mohamed alipambana nyuma ya nguvu za AI kumuokoa Naura na hukumu ya mahakama ya Kiislam nchini humo na kufanikiwa kumtoa katika hukumu ya kifo hadi kifungo cha miaka mitano jela. Wakati ushindi huo wa Naura ukishangiliwa na watetezi wa haki za binadamu, nchini Kenya hivi majuzi kisa cha msichana mwingine kuhukumiwa kunyongwa kimeibua mhemko mpya na kelele za “Asinyongwe” zimetanda angani.Tokeo la picha la ruth kamande

KISA CHA NAURA KUUA KIKOJE?

Wakati unatazama visa vya wasichana hawa kuwaua wapenzi wao usisahau kuwa ipo dokezo ya kuangalia funzo la hukumu yao na makengeza ya baadhi ya sheria ya nchi yetu ambayo nitakuangazia hapa nchini. Naura miaka kadhaa iliyopita akiwa na umri wa miaka 16 aliozwa na wazazi wake kwa Abdulrahman Mohamed Hammad ambako akiwa msichana mdogo asiyejua mambo ya unyumba alikutana na kisa cha kuingiliwa kingono kwa nguvu.

Kutokana na utoto wake hakujua namna ya kumhudumia mume kingono, jambo ambalo lilisababisha mumewe awaite binamu zake waje wamsaidie ili amudu kumwingilia Naura. Siku ya kwanza akiwa katika uthibiti wa wanaume wingine aliingiliwa na mumewe kwa nguvu.

Akaachwa bila pole na hakuwa na wakumlilia kwani alikotoka, yaani nyumbani kwa wazazi wake alashaagwa kwamba yeye sasa ni mali halali ya mumewe; akajitume huko na aoneshe ukomavu. Suala la umri wake kuwa mdogo kukabili changamoto za ndoa wazazi wake hawakulitilia maanani; maadamu posa imeingiaa na mtoto wao kaolewa kwao ilitosha kujipongeza.

Fikra zinanituma kuamini kwamba baada ya kitendo kile Naura aliumia, alijiona dhalili kwa kuingiliwa kimwili huku wanaume wengine wasiokuwa waume zake wakimtazama na kumshurutisha kufanya ngono. Uamuzi aliouchukua msichana huyo siku ya pili ambayo mumewe alitaka tena ashiriki naye tendo la ndoa unanihakikishia kuwa mawazo yangu yako sawa!

Akiwa na kumbukumbu ya kilichomkuta Naura alikuwa amejiandaa kujitetea mwenyewe kwa ukatili aliokuwa anafanyiwa; nadhani ni baada ya kukosa wa kumsaidia. Mumewe alipotaka kurudia kosa ingawa alikuwa peke yake siku hiyo; Naura alikumbuka machungu ya jana yake; alichukua kisu na kumchoma mara 25 mume wake sehemu mbalimbali za mwili wake na kumuua.

Naura alipokamatwa na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria alikiri kufanya kosa hilo, lakini alijaribu kuileza mahakama itazame unyama aliokuwa amefanyiwa akiwa na umri mdogo na ione haja ya kutomhesabia makosa; HAIKUWEZEKANA.

Alihukumiwa kunyongwa hadi kufa mpaka rufaa yake iliposomwa na mahakama kuu ya rufaa ya nchi hiyo na kumpunguzia adhabu msichana huyo jambo ambalo mama yake mzazi alilipokea kwa kusema:

“Angalau mwanangu ametoka katika hukumu ya kifo.” Furaha ambayo AI inapambana kuona inafikia kwenye hatua ya Naura kuachiwa huru.Picha inayohusiana

RUTH ALIUAJE NA KUHUKUMIWA KIFO?

Ifahamike kuwa mbali na urembo aliokuwa nao, Ruth ni msomi, maana wakati anakamatwa mwaka 2015 alikuwa ndiyo kajiunga na Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) kusomea kozi ya biashara.

Akiwa na uhusiano wa kimapenzi na Farid Mohammed mitaa ya Buruburu, jijini Nairobi Kenya alijikuta ameua baada moyo wake kufadhaika sana kutokana na kile Farid alichomfanyia.

Ungana nami wiki ijayo kwenye gazeti hili la Uwazi ili kuhitimisha makala haya

MAKALA: RICHARD MANYOTA NA Mitandao

Comments are closed.